• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
UJAUZITO NA UZAZI: Kutokwa damu ukiwa mjamzito

UJAUZITO NA UZAZI: Kutokwa damu ukiwa mjamzito

NA PAULINE ONGAJI

KUNA baadhi ya wanawake ambao hukanganyikiwa wanapotokwa na damu ukeni wakiwa wajawazito.

Kuna wanaodhani ni hedhi, lakini sivyo.

Tafiti zaonyesha kwamba kati ya asilimia 20 na 25 ya wanawake hutokwa na damu ukeni wakiwa wajawazito.

Damu hii huwa nyepesi ikilinganishwa na hedhi ya kawaida licha ya kutoka kwa wakati sawa na siku za hedhi.Ni nini kinachosababisha hali hii?

•Kuvuja kunaotokana na upandikizaji (Implantation bleeding): Hali hii ya kawaida hutokea wakati yai lililorutubishwa linapojitunga kwenye ukuta wa chupa ya uzazi na kuanza kuota. Damu hii huwa ya rangi ya hudhurungi hafifu au pinki.

•Matumizi ya dawa za kupanga uzazi: Hali hii hutokea mwanamke anaposhika mimba pindi baada ya kusitisha matumizi ya tembe za upangaji uzazi. Hii hutokana na mabadiliko ya kihomoni mwilini.

•Ectopic pregnancy: Hali hii hutokea wakati mimba inapojitundika nje ya chupa ya uzazi. Ishara zingine zinazotokana na hali hii ni pamoja na maumivu makali ya tumbo, msukumo katika sehemu ya rektamu, kisunzi na kuumwa na mabega.

•Mimba kuharibika: Takriban kati ya asilimia 20 na 30 ya mimba huharibika na kutokwa na damu huwa ishara ya hali hii. Kuharibika kwa mimba huanza na chembe ndogo za damu kabla kuwa nzito na kutoka kwa wingi.

•Uchunguzi wa ‘pap smear’: Ni kawaida kwa mwanamke mjamzito kutokwa na damu baada ya uchunguzi wa pap smear au baada ya kushiriki tendo la ndoa.

Unashauriwa kutafuta ushauri wa kimatibabu mara moja unapotokwa na damu ukeni wakati wa ujauzito hata ikiwa hali hii itaisha.

Ingawa wanawake wengi hujifungua bila shida hata baada ya kushuhudia hali hii wakiwa wajawazito, unashauriwa kumwona daktari kila unapogundua kwamba unavuja damu wakati huu.

  • Tags

You can share this post!

JUNGU KUU: Hatari ya Mlima kutengwa na rais

MAPISHI KIKWETU: Kuhifadhi chakula bila friji

T L