• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 4:40 PM
KAMAU: Tanzania ijue kuingilia uhuru wa wanahabari ni kusaliti raia

KAMAU: Tanzania ijue kuingilia uhuru wa wanahabari ni kusaliti raia

Na WANDERI KAMAU

UANAHABARI ni tasnia ambayo imekuwepo duniani tangu mwaka 59 BC (Kabla ya Kuzaliwa Yesu Kristo).

Ni fani iliyoanza kupitia jarida lililoitwa Acta Diurna, ambalo lilinakili hotuba zilizotolewa na viongozi na matukio yaliyotokea kila siku katika Falme ya Roma.

Baadaye, fani hiyo ilikua na kusambaa kote duniani katika miaka iliyofuata.

Kando na kusambaa, uanahabari ulikumbatiwa pakubwa na jamii, kwani uliibuka kama jukwaa lililoipa sauti kuwafikia watawala wake.

Hivi leo, uanahabari ni miongoni mwa tasnia muhimu sana kote duniani kutokana na majukumu unaotekeleza. Tasnia hiyo huorodheshwa kama ‘nguzo ya nne ya jamii’ kutokana na umuhimu wake.

Cha kushangaza ni kwamba, wakati fani hii inaendelea kukua, kusambaa na kustawi pakubwa katika nchi za Magharibi, hali ni kinyume katika nchi nyingi zenye chumi za kadri.

Barani Afrika, viongozi wa kisiasa wameiteka tasnia hiyo na kuigeuza kuwa chombo cha kuendesha jumbe za kujisifu na propaganda kuhusu utendakazi wao.

Ingawa uanahabari unapaswa kuwa chemichemi ya ukweli, hali imekuwa kinyume—umegeuka kuwa msingi wa uwongo, upotoshaji na majisifu.

Mtihani mkuu wa vyombo hivyo umekuwa vile vimekuwa vikiangazia mwelekeo wa janga la corona.

Kama kawaida, vyombo katika baadhi ya nchi kama Amerika vimekuwa vikiweka wazi hali ilivyo bila kuficha lolote.

Hapa nchini, serikali imekuwa katika mstari wa mbele kushirikiana navyo kuwapa Wakenya maelezo ya kweli kuhusiana na ugonjwa huo.

Hii ni hatua ya kuridhisha, ambayo imewawezesha Wakenya wengi kuchukua tahadhari hadi sasa, kuhusu njia za kujikinga dhidi ya kumbukizwa virusi hivyo.

Hata hivyo, inasikitisha kuwa baadhi ya nchi, hasa Tanzania, zimekuwa zikificha ukweli kuhusu hali ilivyo nchini humo.

Serikali ya Rais John Magufuli imelaumiwa kwa kuwahangaisha wanahabari ama vyombo ambavyo vinaeleza hali halisi ilivyo katika taifa hilo.

Majuzi, serikali hiyo ilinukuliwa “ikivionya” vyombo vya habari nchini Kenya dhidi ya “kuipotosha dunia” kuhusu maambukizi ya corona yalivyo katika taifa hilo.

Hili ni kosa kubwa kwa serikali ya Rais Magufuli, hasa ikizingatiwa Tanzania inaendelea kushuhudia maafa mengi kutokana na janga hilo.

Ni kosa kuviingilia ama kuvidhibiti vyombo hivyo na “kuvielekeza” vile vitakavyoripoti. Kiundani, huu ni usaliti wa serikali dhidi ya raia wake!

Daima, vyombo vya habari vinapaswa kuwa huru katika utendakazi wake.

[email protected]

You can share this post!

TAHARIRI: Dawa ya tatizo la michezo ni ufadhili

Timu ya Kenya ya marathon ya Olimpiki yapigwa jeki na Sh1m...