• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
Kanairo: Askari atishia kuroga aliyempora simu Nairobi

Kanairo: Askari atishia kuroga aliyempora simu Nairobi

NA SAMMY WAWERU 

ASKARI kwa jina Sammy Ondimu Ngare amelalamikia kuibwa simu jijini Nairobi, akitishia kuchukulia mhusika hatua isiyo ya kawaida.  

Bw Ondimu, ambaye ni maarufu mitandaoni amesema aliyempora hatakuwa na budi ila kumuendea kwa waganga.

Kupitia chapisho katika ukurasa wake rasmi wa Facebook, afisa huyo wa kitengo cha askari tawala (AP), alitangaza Jumamosi, Oktoba 28, 2023 aliibwa simu ambayo hakufichua thamani yake, Jijini Nairobi. 

Alidokeza kwamba aliporwa simu yake ya mkono – rununu Ijumaa usiku. 

Polisi wengi wakiogopwa na raia, Ondimu alielezea kushangazwa kwake na aliyemuiba simu. 

“Kanairo kanairo kanairo…Hata hamuogopi musikali (askari) jamani…Kanairo ilinifanyia ile kitu last night (usiku uliopita) katika shoo ya Alikiba. Niko mteja watu wangu,” askari huyo ambaye pia ni msanii aliandika. 

Kanairo, ni jina la mtaa linalomaanisha Jiji la Nairobi. 

Katika lalama zilizozua ucheshi Facebook, huku mashabiki wakimuonea huruma na wengine kumkejeli, Ondimu alishangaa atakaporipoti kisa hicho ikizingatiwa kuwa yeye ni afisa wa polisi. 

“Sasa nitareport (ripoti) kwangu ama kwa forithi mwingine (polisi mwingine)?” akauliza. 

“Nani ako na simu extra (nyingine)?” chapisho la askari huyo linaelezea. 

Bw Ondimu alikuwa amehudhuria shoo ya mwanamuziki mwenza, Alikiba ambayo kulingana na afisa huyo ilifanyika Nairobi.

“Nitaroga mwenye aliiba simu, (akimaanisha kwamba atamroga mwizi – kuenda kwa mganga),” alisisitiza kwenye safu ya maoni, akijibu mchango wa wafuasi wake. 

Alikiba ni mwimbaji mwenye asili ya Tanzania wa nyimbo za miondoko ya kisasa, hasa za kimapenzi. 

Ondimu huimba nyimbo za injili. 

Kando na kuwa askari, vilevile ni Mwanafilanthropia (philanthropist) ambaye hutumia kurasa zake za mitandao ya kijamii kusaidia wasiojiweza katika jamii. 

Haswa Facebook, afisa huyo huangazia visa vya watu wenye matatizo mbalimbali, kama vile wanaonyanyaswa kwenye mahusiano, ndoa na jamii. 

Isitoshe, hutumia kurasa zake kuchanga karo ya wanafunzi wanaotoka familia maskini na pia kusaidia watoto wa mitaani (chokoraa). 

Visa vya wizi wa simu mijini vinazidi kushuhudiwa, taarifa ya majuzi iliyochapishwa na Gazeti la Daily Nation ikionyesha Kaunti ya Nairobi inaongoza kwa wizi. 

Idara ya polisi, inasema nyingi ya simu zinazoibwa hupakiwa na kuuzwa katika mataifa jirani. 

  • Tags

You can share this post!

Murkomen amfokea Cherargei

Wanakriketi wa Nairobi kutuzwa kwa mara ya kwanza na NPCA...

T L