• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Kanisa Katoliki laingilia biashara ya kuongeza maziwa thamani kusaidia wafugaji Kiambu 

Kanisa Katoliki laingilia biashara ya kuongeza maziwa thamani kusaidia wafugaji Kiambu 

NA SAMMY WAWERU

KANISA la Katoliki limezindua kiwanda cha kuongeza maziwa thamani eneo la Limuru, mradi huo ukilenga kupiga jeki wafugaji wa ng’ombe wa maziwa katika Kaunti ya Kiambu.

Dhehebu hilo kupitia Caritas Nairobi, shirika la kutoa misaada na maendeleo Jimbo Kuu la Nairobi, limewekeza katika biashara ya usindikaji maziwa inayopaniwa kuwafaa zaidi ya wakulima 5, 000.

Kaunti ya Kiambu inahudumu chini ya Jimbo Kuu la Nairobi.

Kulingana na kanisa hilo, Caritas Nairobi Dairy Unit inakusudiwa kuwezesha wafugaji wa mapato ya chini kujiendeleza, ikiwa ni pamoja na kuangazia kero ya upungufu wa chakula na utapiamlo.

“Kama kanisa, hatujukumiki kulisha washirika chakula cha kiroho pekee, bali pia kuwakuza kiuchumi na kimaendeleo,” akasema Askofu Mkuu wa Nairobi, Philip Anyolo mnamo Novemba 16, 2023, wakati wa uzinduzi rasmi wa kituo hicho katika Shamba la Caritas, Limuru.

Askofu Mkuu huyo alielezea kujitolea kwa Kanisa la Katoliki katika kusaidia kuboresha sekta ya kilimo na ufugaji, kupitia mipango yake ya maendeleo.

“Kuangazia njaa na usalama wa chakula ni jukumu letu sote. Uzinduzi wa mradi huu sio tu kuhusu kuanzisha kiwanda cha usindikaji maziwa, bali pia unalenga kuleta maendeleo katika jamii,” Askofu Anyolo akasema.

Akaongeza, “Katika ulimwengu ambapo mamilioni ya watu bado wanateseka kutokana na njaa na utapiamlo, hatua hii itasaidia wakulima katika kukabiliana na changamoto zinazozingira jamii.”

Huku akiahidi kwamba Caritas Nairobi itaendelea kusaidia wafugaji wa maziwa Kaunti ya Kiambu, Askofu Anyolo aliitaka serikali kuwa na mipango itakayosaidia kupunguza gharama ya chakula cha mifugo cha madukani.

Wafugaji wanaendelea kulemewa na gharama ya juu ya chakula, jambo ambalo linatishia sekta ya maziwa nchini.

Aidha, Kenya huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 70 ya malighafi inayotumika katika kutengeneza chakula cha mifugo.

Kiwanda cha Caritas Dairy Unit kina uwezo kusindika lita 20, 000 za maziwa kwa siku, Mtawa Mary Mbachi, Mkurugenzi wa Caritas Nairobi, akifichua kuwa kituo hicho kiligharimu zaidi ya Sh150 milioni kukiunda.

“Kwa sasa, tunakusanya maziwa kutoka kwa wafugaji, tunayachemsha, tunaypoesha na kisha tunayatafutia soko,” Mtawa Mbachi akaelezea.

Aliongeza kuwa, hivi karibuni kiwanda hicho kitaanza kusindika bidhaa za maziwa kama vile maziwa ya mtindi (yoghurt) na yaliyochacha (mala).

Kupitia mipango ya Caritas Nairobi, wakulima wanapokea chakula cha mifugo kwa bei nafuu na mafunzo jinsi ya kuunda silage, kuvuna maji ya mvua, na uzalishaji wa bayogesi, chini ya mipango inayolenga kuangazia athari za mabadiliko ya tabianchi ili kuwasaidia hasa wakati wa kiangazi.

Kiwanda hicho kibuni nafasi za kazi zipatazo 50, na wengine 60 kunufaika kupitia ukusanyaji na usambazaji wa maziwa na kazi za ofisi.

Kituo hicho kimejengwa kwenye ardhi yenye ukubwa wa ekari tatu.

Sekta ya maziwa ina mchango mkubwa katika kusaidia kukuza na kuboresha uchumi wa nchi, ikikadiriwa Kenya huzalisha zaidi ya lita bilioni 5.2 za maziwa kila mwaka kutoka kwa wafugaji milioni 5.1.

Aidha, inapaniwa kuletea taifa mapato ya Sh230 bilioni kwa mwaka.

Afisa Mtendaji Mtendaji Benki ya Caritas, Bw David Mukaru, alitangaza kwamba shirika hilo la kifedha linalomilikiwa na Kanisa Katoliki limetenga zaidi ya Sh500 milioni kusaidia wafugaji wa maziwa Kiambu kupitia huduma za mikopo.

Washirika wakuu waliofanikisha kuanzishwa kwa Caritas Dairy Unit ni pamoja na Caritas Italiana, Italian Agency for Development Cooperation (AICS), CELIM, na Missio Invest.

Mradi huo ulianzishwa na Kadinali John Njue, ambaye kwa sasa ni Askofu Mstaafu, mwaka 2010 kama Mradi wa Kuwawezesha Kiuchumi Wanawake wa eneo la Mataara (MWEEP), Limuru, uliolenga kupunguza umaskini miongoni mwao.

  • Tags

You can share this post!

Kenya kupoteza mnada wa majani chai kwa Tanzania kwa sababu...

Gavana Nassir ataka kujua ziliko pesa za El-Nino

T L