• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Karua avuruga mipango ya Azimio, Kenya Kwanza

Karua avuruga mipango ya Azimio, Kenya Kwanza

NA BENSON MATHEKA

HATUA ya kiongozi wa chama cha Narc Kenya Martha Karua ya kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja imevuruga hesabu ya Naibu Rais William Ruto ambaye pia alikuwa akimrai kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza Alliance.

Wadadisi wanasema kuwa ingawa waziri huyo wa zamani wa Masuala ya Haki amepiga jeki mgombea urais wa Azimio la Umoja, Raila Odinga washirika wa Rais Uhuru Kenyatta ambaye anaunga waziri mkuu huyo wa zamani kuwa mrithi wake wameingiwa na tumbojoto.

Washirika hao pamoja na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka ambaye pamoja na Bi Karua walikuwa katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA) walikuwa wakitajwa miongoni mwa wanaoweza kuwa wagonbea wenza wa Bw Odinga.

Washirika wa Rais Kenyatta ambao wamekuwa wakipigiwa upatu kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga ni aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth na waziri wa Kilimo Peter Munya, Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi na mwenzake wa Nakuru Lee Kinyanjui.

“Hata hivyo, kujiunga kwa Bi Karua na Muungano wa Azimio la Umoja kunaweza kubadilisha mambo. Kuna hisia kwamba huenda akateuliwa mgonbea mwenza wa Bw Odinga na hivyo kufungia nje wanasiasa wengine kutoka Mlima Kenya ambao wamekuwa wakipigia debe kiongozi huyo wa ODM eneo la Mlima Kenya,” asema mchanganuzi wa siasa Obed Kamau.

Asema akiwa mwanamke, Bi Karua ambaye ametangaza azima ya kugombea ugavana kaunti ya Kirinyaga yuko katika nafasi nzuri ya kuteuliwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Mbunge mmoja kutoka Mlima Kenya ambaye aliomba tusitaje jina lake alisema kujiunga kwa Bi Karua na Azimio kumezua tumbojoto miongoni mwa wanasiasa waliokuwa msitari wa mbele kumuuza Bw Odinga katika eneo hilo.

“Martha ni johari lililomezewa mate na Azimio na Kenya Kwanza. Kujiunga kwake na Azimio kumesababisha wasiwasi miongoni mwa waliotegea wadhifa wa mgombea mwenza wa Bw Odinga ambao wanahisi kuwa wamejitolea kafara kuuza Bw Odinga katika Mlima Kenya na kuimarisha umaarufu wake. Hata hivyo, tunasubiri kuona yatakayotukia,” asema mbunge huyo.

Kabla ya kutangaza kwamba atamuunga Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti, Bi Karua alikuwa amezungumza na washirika wa Dkt Ruto ambao ni wanachama wa vuguvugu la Jukwaa la Umoja wa Mlima Kenya akiwemo kiongozi wa Chama Cha Kazi Moses Kuria na mwenzake wa The Service Party Kenya Mwangi Kiunjuri.

Duru zinasema kuwa chambo alichokuwa akirushiwa ni kuteuliwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto.

Wadadisi wanasema kuwa ingawa kujiunga kwake na Azimio ni afueni kwa washirika wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya wanaopigiwa upatu kuwa mgombea mwenza wa Naibu rais, Kenya Kwanza Alliance itakuwa na kibarua ikiwa atateuliwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

“Kwa kila hali, hatua ya Martha kujiunga na Azimio imeathiri mirengo miwili mikuu hasa kuhusiana na wadhifa wa mgombea mwenza huku Bw Odinga akifaidika zaidi. Martha na Odinga wametoka mbali katika juhudi zao za kupigania demokrasia na haki nchini,” asema Bw Kamau.

Anasema kuwa hatua ya Bi Karua kumuunga Bw Odinga bila kupitia OKA pia ni pigo kwa Bw Musyoka ambaye pia anamezea mate kuwa mgombea mwenza wa Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Ruto atikisa ngome ya Baba Pwani

Rais Uhuru alainisha baraza la mawaziri bila mbwembwe tele

T L