• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 4:33 PM
Ruto atikisa ngome ya Baba Pwani

Ruto atikisa ngome ya Baba Pwani

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto yuko mbioni kuyeyusha ushawishi wa Azimio la Umoja Pwani kwa kushawishi vyama vya eneo hilo vijiunge na muungano wa Kenya Kwanza.

Mnamo Jumatatu Dkt Ruto alifaulu kunasa chama cha Kadu-Asili baada ya maafisa wa chama hicho kukubali kuunga mkono azma yake ya urais.

Katika kile kilichoonekana kama kukiwezesha chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) kupokonya Azimio la Umoja ushindi katika kinyang’anyiro cha ugavana Kilifi, Naibu Rais alifaulu kumshawishi kiongozi wa chama cha hicho Emmanuel Nzai kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kilifi.

Nzai ambaye ni afisa mkuu mtendaji wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani, sasa atakuwa mgombeaji mwenza wa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa ambaye anapigiwa upatu kupata tiketi ya UDA katika mchujo wa Aprili.

“Baada ya kufanya mashauriano ya kina, kukutana na wadau na wafuasi wangu, nimeamua kujiunga na UDA. Naitakia wema kaunti ya Kilifi katika safari hii ya kuipa uongozi mpya chini ya muungano wa Kenya Kwanza,” akasema alipopokewa na Dkt Ruto katika makao yake rasmi mtaani Karen, Nairobi.

Aliandamana na maafisa kadhaa wa Kadu-Asili ambayo ina wafuasi wengi katika kaunti ya Kilifi na eneo zima la Pwani.

Bi Jumwa na Bw Nzai sasa wanatarajiwa kupambana na aliyekuwa Waziri Msaidizi wa Ardhi Gideoni Mung’aro ambaye anatarajiwa kupeperusha bendera ya ODM katika kinyang’anyiro cha ugavana, Kilifi.

Wadadisi wa siasa wanasema kuwa, kwa kumvutia Bw Nzai, upande wake Dkt Ruto pia anapania kudhoofisha ushawishi wa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) kinachoongozwa na Gavana wa Kilifi Amason Kingi.

“Kwa kumnasa Bw Nzai ambaye ni mmoja wa wawaniaji ambao walikuwa wakipigizwa upatu kumrithi Gavana Kingi, Ruto amefaulu kupenya katika eneo hilo ambalo linasawiriwa kuwa ngome ya ODM. Sasa ina maana kuwa chama hicho kinachoongozwa na Rais Odinga kinalazimika kupanga mikakati mipya kuweza kushinda kiti hicho,” anasema Bw Dismu Mokua.

PAA iko ndani ya Azimio la Umoja kupitia chama tawala cha Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Duru zimeiambia safu hii kwamba wandani wa Dkt Ruto vile vile wanajaribu kufanya mazungumzo na maafisa wa cha Umoja Summit Party of Kenya (USPK) kusudi wajiunge cha muungano wa Kenya Kwanza.

Baada ya USPK kuandaa kongamano la wajumbe wake (NDC) katika mkahawa mmoja jijini Nairobi inasemekana kuwa mbunge mmoja wa UDA alifanya mazungumzo na mwenyekiti wake Matano Chengo.

“Ni kweli kwamba wandani wa Ruto walinipigia simu wakitaka tukutane kuzungumzia suala la kufanya kazi pamoja. Lakini kama muungano, hatujajadili suala hilo,” Bw Chengo akanukuliwa akisema.

Chama cha USPK ambacho kimemteua kiongozi wake Walter Mong’are “Nyambane” kuwa mgombeaji wake wa Urais ni mojawapo ya vyama tanzu katika muungano wa Ukombozi wa Majimbo.

Vyama vingine katika muungano huo ni Kadu-Asili pamoja na chama cha Shirikisho.

Hatua ya Dkt Ruto kunasa Kadu-Asili na kufikia USPK ni sehemu ya mchakato mzima wa mwanasiasa huyo kuondoa eneo la Pwani chini ya udhibiti wa Bw Odinga.Eneo hilo limesalia ngome ya ODM kuanzia uchaguzi mkuu wa 1997.

Kwa mfano katika uchaguzi mkuu wa 2017, chama hicho kilishinda viti vyote katika kaunti ya Kilifi, kuanzia ugavana hadi udiwani.

  • Tags

You can share this post!

Biden: Tutamkomesha Putin!

Karua avuruga mipango ya Azimio, Kenya Kwanza

T L