• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 PM
Rais Uhuru alainisha baraza la mawaziri bila mbwembwe tele

Rais Uhuru alainisha baraza la mawaziri bila mbwembwe tele

NA WANDERI KAMAU

HUENDA Rais Uhuru Kenyatta akakosa kuwateua mawaziri wengine kujaza nafasi zilizoachwa wazi na mawaziri waliojiuzulu Februari, kuwania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika kaunti wanakotoka.

‘Jamvi la Siasa’ limebaini kwamba tayari, Rais Kenyatta amejaza nafasi hizo kimya kimya, hali inayoachilia huenda akakosa kufanya uteuzi wowote mpya.

Mawaziri waliojiuzulu ni Bi Sicily Kariuki (Maji na Usafi), Charles Keter (Ugatuzi), John Munyes (Mafuta) na Adan Mohamed (Masuala ya Afrika Mashariki).

Bi Kariuki analenga kuwania ugavana katika Kaunti ya Nyandarua, Bw Keter katika Kaunti ya Kericho, Bw Munyes katika Kaunti ya Turkana huku Bw Mohamed akilenga kuwania ugavana katika Kaunti ya Mandera.

Ili kujaza pengo walizoacha, imebainika Rais Kenyatta amewateua mawaziri Eugene Wamalwa (Ulinzi) kuwa Kaimu Waziri wa Ugatuzi, James Macharia (Uchukuzi) kuwa Kaimu Waziri wa Maji, Monicah Juma (Kawi) kuwa Kaimu Waziri wa Mafuta na Madini na Betty Maina (Biashara na Viwanda) kuwa Kaimu Waziri wa Masuala ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kikanda.

Vile vile imebainika Rais hana mipango yoyote kujaza nafasi za Manaibu Waziri waliojiuzulu katika wizara za Ugatuzi, Uchukuzi, Mafuta, Mashauri ya Kigeni, Utalii, Usalama wa Ndani, Michezo na Leba.

Kulingana na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa, lengo kuu la Rais Kenyatta kutojaza nafasi hizo ni kuhakikisha kuwa anamaliza muhula wake vizuri bila mivutano ya kisiasa ambayo hushuhudiwa nyakati za kisiasa.

“Ukitathmini kwa kina, mawaziri waliopewa majukumu zaidi ni waandani wa karibu wa Rais Kenyatta. Wengi wao wamehudumu tangu muhula wa kwanza mnamo 2013. Ni watu anaoamini watamsaidia sana kukamilisha miradi muhimu aliyobakisha,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baadhi ya miradi ambayo Rais Kenyata anapania kukamilisha ni barabara ya Nairobi Expressway (inayoliunganisha jiji la Nairobi na Uwanja wa Ndege wa JKIA), Barabara ya Kenol-Marua, Barabara ya Mau Mau, Bwawa la Thiba (Kaunti ya Kirinyaga), Bwawa la Karemeno (Kaunti ya Kiambu) kati ya mingine muhimu.

Wachanganuzi wanasema Rais anawategemea pakubwa mawaziri hao, kwani kukamilishwa kwa miradi hiyo ndiko kunatarajiwa kuwa sifa kuu atakayojivunia baada ya kung’atuka uongozini.

“Kwa miaka minne iliyopita, hatua ya Rais Kenyatta kubuni handisheki na kiongozi wa ODM, Raila Odinga imezua siasa na mvutano mkubwa kati yake na Naibu Rais William Ruto. Mivutano baina yao inaonekana kuziba utendakazi na miradi inayoendeshwa na serikali yake kwa jumla,” asema Prof Ngugi Njoroge, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wachanganuzi pia wanasema hatua ya Rais Kenyatta inalenga kumpa muda wa kuendelea harakati za urithi wake.

Rais Kenyatta ametangaza wazi kwamba atamunga mkono Bw Odinga kuwa mrithi wake kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

Hata hivyo, baadhi ya wachanganuzi na wakosoaji wa Rais Kenyatta wanasema huenda ikawa vigumu kwake kutimiza baadhi ya miradi anayolenga kukamilisha, kwani baadhi ya mawaziri aliowateua bado wanaendelea kuhusika kwenye siasa.

Hasa, wanamtaja Bw Wamalwa kuwa mfano wa mawaziri wanaojihusisha kwenye siasa licha ya kushikilia wizara mbili.

“Ni vizuri Rais kutathmini utendakazi wa baadhi ya mawaziri aliowaongeza majukumu, kwani kuna uwezekano mkubwa wakamwangusha, kiasi cha kushindwa kukamilisha kutekeleza miradi muhimu aliyopanga kumaliza. Baadhi yao ni Waziri Eugene Wamalwa, ambapo licha ya majukumu mengi aliyo nayo, bado anaendelea kujihusisha na siasa za chama cha Democratic Action Party-DAP na eneo la Magharibi kwa jumla. Ni baadhi ya mawaziri ambao Rais anapaswa kuwaangalia sana ili kuhakikisha hawatamwangusha,” asema Prof Njoroge.

  • Tags

You can share this post!

Karua avuruga mipango ya Azimio, Kenya Kwanza

Baba achezea wagombeaji ODM kwa kutoa tiketi moja kwa moja

T L