• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tufaane na kutendeana wema kwa wema tungali hai duniani

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tufaane na kutendeana wema kwa wema tungali hai duniani

NA WALLAH BIN WALLAH

KILA mmoja wetu ajiulize endapo amewahi kutenda wema au kutendewa wema wowote maishani?

Ukiwa umewahi kutendewa wema, nawe umewahi kumtendea wema aliyekutendea wema au bado? Iwapo bado, unasubiri nini? Au siku hizi wema haulipwi kwa wema?

Ndugu wapenzi ni vyema kusaidiana na kutendeana wema tungali hai duniani! Kutenda wema ni utu! Tusidanganyane kwamba tuna mapenzi rohoni kumbe ni mafamba tu! Wema hulipwa kwa wema! Haulipwi kwa maovu wala kwa maneno matupu!

Tuanzie kwa wazee wetu na ndugu zetu wazalendo waliojitoa mhanga kukikuza na kukitukuza Kiswahili wakatujengea msingi imara tulio nao sisi hivi sasa! Tumewalipa wema gani? Au tunangoja mpaka waondoke wote duniani ndipo tuwasifie?

Mbona hatuwatafuti na kuwatembelea kule wanakoishi kwa ulitima na usononi wao?

Mbona tunawataja tu vikaoni na kwenye makongamano kuwania umaarufu kwamba tunawajua?

Halafu panapotokea kuwaalika magwiji hao waliojisulubu kukikuza Kiswahili ambao bado wako hai kwenye vikao na makongamano hayo, huwa tunawabebesha dhiki ya kujisafirisha kwa kutumia nauli zao ndipo wafike watoe hotuba zao za busara kuwamegea waalishi ukumbini!

Mara nyingine hutokea waandalizi wa vikao na makongamano hayo kuwaomba wazee hao kuwapa pesa za kuchangia kufadhili vikao vya wagosi waandalizi badala ya kuwalipa wazee wenyewe waalikwa!

Naomba kuwatilia dua na kuwapongeza sana ndugu wapenzi wote waliowahi kuwatembelea ama kuwatendea wema wakiwa hai wazee wetu: Mwalimu Hassan Mbega, Sheikh Nabhany, Abdallah Mwasimba, Maulid Juma, Prof. Said Ahmed Mohamed, Prof Ken Walibora, Dkt. Muhammed Seif Khatib, Badi Muhsin, Mohamed Juma Njuguna na wengineo! Mola awajazie neema!

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: John Muli

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Senior...

T L