• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Senior Chief Koinange, Kiambu

VYAMA: Chama cha Kiswahili katika shule ya upili ya Senior Chief Koinange, Kiambu

NA CHRIS ADUNGO

LICHA ya uchanga, Chama cha Kiswahili cha Senior Chief Koinange Girls (CHAKIKO) kinazidi kupata umaarufu miongoni mwa wanafunzi na walimu katika shule hii iliyoko Kaunti ya Kiambu.

Zaidi ya kupiga jeki Idara ya Kiswahili, chama hiki kilichoasisiwa mnamo Mei 2021 kinalenga pia kutambua, kukuza na kulea vipaji vya wanafunzi katika ulingo wa uanahabari wakielekezwa na walimu Felly Nyamboki, Mwanahamisi Mutsy na Okeri Bikundo.

Zaidi ya kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, madhumuni mengine ya CHAKIKO ni kustawisha makuzi ya lugha, kuwapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kuzamia uandishi wa kazi bunilizi, kuboresha matokeo ya KCSE na kuzidisha maarifa ya utafiti katika fani zinazofungamana na Kiswahili.

“CHAKIKO ni chombo madhubuti kinachopania kuchochea wanafunzi kukichapukia Kiswahili. Kinalea vipaji vyao katika sanaa mbalimbali na kuwakuza pia kimaadili. Wanachama wengi wameamshiwa hamu ya kuwa wanahabari, walimu na wahariri,” anasema Bi Nyamboki.

Ili kuwapa wanafunzi wote nafasi ya kushiriki shughuli za chama kikamilifu, CHAKIKO sasa kinalenga kuanzisha kitengo cha uigizaji kitakachorahisisha ujifunzaji na ufundishaji wa Fasihi Andishi.

Kupitia CHAKIKO, wanafunzi wa Senior Chief Koinange Girls sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji wakubwa wa gazeti la Taifa Leo kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE).

Wanafunzi wa Senior Chief Koinange Girls sasa ni mabalozi halisi wa Kiswahili na wasomaji wakubwa wa gazeti la Taifa Leo kupitia mradi wa Newspapers in Education (NiE). PICHA | CHRIS ADUNGO

Chama pia kinaazimia kuchapisha jarida la Kiswahili kila mwaka.

Kufaulu kwa mpango huo chini ya Bi Susan Kariuki (Mwalimu Mkuu), kutawapa wanachama nafasi murua ya kutononoa vipaji vyao vya uhariri na uandishi wa kazi za kitaaluma.

You can share this post!

KAULI YA WALLAH BIN WALLAH: Tufaane na kutendeana wema kwa...

Hila ya Ruto kumtetea Kalonzo

T L