• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Kawira Mwangaza: Dada zangu wote ni ‘singo’, hakuna aliyeoleka

Kawira Mwangaza: Dada zangu wote ni ‘singo’, hakuna aliyeoleka

NA SAMMY WAWERU

GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza Jumatano, Novemba 8, 2023 jioni aligeuzwa kuwa gumzo la mitandao ya kijamii baada ya kufichua kuwa dada zake wote hawajaoleka.

Bi Kawira alifichua hayo mbele ya Kikao cha Bunge la Seneti, wakati akipigwa msasa na wakili wake kufuatia kesi inayomuandama kumbandua mamlakani.

Bosi huyo wa Kaunti ya Meru, Madiwan (MCA) walipiga kura ya kumng’atua mnamo Oktoba 25, 2023 kwa tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi, ubadhirifu wa mali ya umma na ubaguzi katika kuajiri.

Hatma yake ikiwa mikononi mwa Seneti, wakati akihojiwa na wakili anayemwakilisha, Kawira alikanusha madai kuwa dada yake mmoja ameolewa na afisa wa Kaunti ya Meru.

Wakili aliuliza, “Umeshutumiwa kwa ubaguzi katika kuajiri wafanyakazi wa kaunti, na inadaiwa kuwa dada yako mmoja ameolewa na afisa wa Kaunti ya Meru. Je, hii ni kweli au uongo?”

Gavana huyo alijibu upesi, akipuuzilia mbali adai hayo.

“Hakika, dada zangu wote hawajaoleka,” Kawira alifichua.

Kukiri kwake kwamba dada zake wangali singo, kulizua mjadala mitandaoni baadhi ya wachangiaji wakimtania.

Gavana Mwangaza ameolewa na Murega Baichu, ambaye amekuwa akijivunia hadharani.

Huku Kawira akiwa mhubiri, mume wake ni mwanamuziki wa injili, na Bw Baichu aliandamana naye kufika mbele ya Bunge la Seneti kuhojiwa.

Mchakato wa kuondoa Gavana Kawira mamlakani, ambaye ameponea majaribio mawili kung’atuliwa chini ya kipindi cha mwaka mmoja tangu achaguliwe Agosti 2022, ulianza Jumanne, Novemba 7, 2023, na kuendelea hadi Jumatano, Novemba 8.

Aidha, Spika wa Seneti, Bw Amason Kingi ndiye aliongoza mchakato huo.

Mbali na mashtaka ya kutumia vibaya rasilimali za umma, kutumia vibaya ofisi, na katika kuajiri wafanyakazi kwenye kaunti, Gavana Kawira pia anatuhumiwa kudhalilisha viongozi wengine katika kaunti, kufanya teuzi zisizo halali, na kuvunja sheria kuongoza kaunti.

Gavana alichaguliwa kama mgombea huru, na kabla kuwa Gavana alihudumu kama Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Meru.

Hadi wakati wa kuchapisha taarifa hii, Bunge la Seneti halikuwa limeamua hatma yake.

 

  • Tags

You can share this post!

Kiptum alenga kukamilisha Rotterdam Marathon kwa muda chini...

Ufugaji samaki wamfaidi licha ya changamoto tele

T L