• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 PM
Kiptum alenga kukamilisha Rotterdam Marathon kwa muda chini ya saa mbili

Kiptum alenga kukamilisha Rotterdam Marathon kwa muda chini ya saa mbili

Na AYUMBA AYODI

MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia mbio za kilomita 42 ya wanaume, Kelvin Kiptum atajaribu kukamilisha umbali huo chini ya saa mbili wakati wa NN Rotterdam Marathon nchini Uholanzi mnamo Aprili 14, 2024.

Mkenya huyo, ambaye alianza maisha ya marathon kama mwekaji wa kasi katika Rotterdam Marathon mwaka 2019, amesema yuko makini kurejea katika barabara za mji huo kwa kishindo.

“Nataka nirudi Rotterdam kutimka kwa kasi ya juu… Barabara ni tambarare mjini humo na zinaruhusu mtu kuandikisha kasi ya juu. Naamini mashabiki pia watatupa msukumo,” alisema Kiptum na kuongeza kuwa angependa kuwa mmoja wa majina makubwa ya kukumbukwa katika marathon.

Kiptum aliweka bayana matarajio yake mjini Rotterdam. “Nitajaribu kufuta rekodi yangu ya dunia hapa. Najua niko na uwezo wa kufanya hivyo ikiwa matayarisho yangu yatakuwa mazuri na pia hali ya anga itakuwa nzuri wakati wa mashindano,” alisema Kiptum hapo Jumatano.

“Nitajaribu kabisa kukaribia saa mbili kwa hivyo mbona nisiivizie? Inaweza kuonekana tamaa ya kutaka makuu, lakini sina uoga kuweka malengo kama haya. Hakuna kinachoweza kuzuia nguvu za binadamu,” alisema Kiptum.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 23, ambaye amerishiki marathon tatu pekee (Valencia Marathon, London Marathon na Chicago Marathon), alivunja rekodi ya dunia ya Mkenya mwenzake Eliud Kipchoge ya saa 2:01:09 ambayo bingwa huyo wa Olimpiki aliweka jijini Berlin, Ujerumani mnamo Septemba 25, 2022.

Ni mara ya kwanza rekodi ya dunia ilipatikana mjini Chicago tangu Mmoroko Khalid Khannouchi atimke 2:05:42 mnamo Oktoba 24, 1999.

Kipchoge aliweka historia kwa kuwa binadamu wa kwanza kukamilisha mbio za 42km chini ya saa mbili na dakika mbili alipofuta rekodi ya dunia ya Mkenya mwenzake Dennis Kimetto ya 2:02:57 iliyokuwa imara tangu Berlin Marathon 2014.

Kipchoge alimaliza umbali huo kwa 2:01:39 mwaka 2018 mjini humo na kuimarisha rekodi yake hadi 2:01:09 mwaka 2022 kabla ya Kiptum kuivunja kwa sekunde 34.

Kiptum anajivunia kutimka 2:01:53 akishinda Valencia Marathon nchini Uhispania mnamo Desemba 4, 2022.

Alishinda London Marathon mnamo Aprili 5 kwa 2:01:25. Yeye ni Mkenya wa sita kushikilia rekodi ya dunia baada ya Paul Tergat, Patrick Makau, Wilson Kipsang, Kimetto na Kipchoge.

Mkenya wa mwisho kutwaa ubingwa wa Rotterdam Marathon ni Marius Kipserem mwaka 2019.

Mbelgiji Bashir Abdi anashikilia rekodi ya Rotterdam Marathon ya 2:03:36 aliyoweka mwaka 2021.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Ada ya kujipatia paspoti yaongezwa huku Ruto akiwinda pato...

Kawira Mwangaza: Dada zangu wote ni ‘singo’, hakuna...

T L