• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Ufugaji samaki wamfaidi licha ya changamoto tele

Ufugaji samaki wamfaidi licha ya changamoto tele

NA PAULINE ONGAJI

MWAKA wa 2008, Bi Faith Kanaya Buluma, 55, mkazi wa kijiji cha Nangina, Kaunti ya Busia, aliamua kuelekea katika Ziwa Victoria kununua samaki, ambapo nia yake ilikuwa kujitosa katika biashara ya uuzaji samaki.

Lakini alipigwa na butwaa alipogundua kwamba hangepata samaki endapo hakuwa tayari kuuza mwili wake ili kupokea bidhaa hizo.

Lakini kwa Bi Buluma, huo sio mkondo wa maisha ambao alikuwa tayari kufuata, na badala ya kufa moyo, aliamua kufuata mbinu nyingine ili kufanikiwa katika biashara ya samaki.

Kwa hivyo, badala ya kutegemea samaki kutoka kwenye ziwa hilo, mwaka wa 2009 kwa usaidizi wa shirika moja la kijamii, alifanikiwa kutengeneza kidimbwi cha samaki na hivyo kuanzisha rasmi shamba lake la ufugaji samaki la Mingfa fish farm.

“Baadaye nilitembelea afisi za hapa nyumbani za wizara ya uvuvi ambapo kando na kupewa mafunzo zaidi kuhusiana na biashara hii, walinisaidia kutengeneza kidimbwi kingine,” aeleza.

Kulingana na Bi Buluma, mwanzoni alinunua watoto wa samaki aina ya tilapia 1,000, waliomgharimu Sh13,000.

“Lakini sikujuta kwani mauzo yangu ya kwanza yalinipa faida ya takriban Sh79,000.”

Kufikia sasa Bi Buluma ana vidimbwi vinne vya samaki, na viwili vinaundwa, huku akitumai kwamba mara hii atavuna samaki wake mara mbili kwa mwaka.

Kando na ufugaji samaki, Bi Buluma amefungua duka la Namboboto aquashop, ambapo anauza chakula cha samaki na bidhaa nyingine za ufugaji samaki, biashara anayoiendesha mjini Busia.

Alifungua duka hilo mwaka wa 2010 baada ya kuhangaika kupata chakula cha samaki, ambapo kila wakati alilazimika kuvuka mpaka hadi nchini Uganda ili kununua bidhaa hizo.

Na hivyo, kutoka kwa akiba kidogo aliyokuwa nayo, vile vile mkopo aliopata kutoka kwa shirika la kukopesha fedha, alifaulu kufungua duka hili.

“Dukani mwangu, nauza chakula na bidhaa nyingine za ufugaji samaki, tunaunda na kukarabati vidimbwi vya kufuga samaki, na hata kuwaunganisha wafugaji na masoko ya samaki. Wateja wangu hasa ni wafanyabiashara wa samaki sio tu kutoka Kenya, bali pia Uganda,” anasimulia.

Bi Buluma anaendelea kushamiri huku biashara hii mbali na faida zingine, ikimwezesha kusomesha wanawe hadi chuo kikuu.
Hata hivyo, biashara hii haijakosa changamoto. Kizingiti kikuu kimekuwa mabadiliko ya hali ya anga kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mfugaji samaki Faith Buluma akilisha samaki katika kidimbwi chake kilichoko kijiji cha Mundika, eneo la Funyula, Kaunti ya Busia. PICHA | MAKTABA

“Sisi hasa hutegemea maji ya mvua kwenye vidimbwi vyetu, kumaanisha kuwa kusiponyesha basi tunakumbwa na matatizo.”
Lakini changamoto kuu kwake ilikuwa mwanzoni ukosefu wa rasilimali na hasa ardhi ya kuanzisha biashara hii.

“Ilimchukua mume wangu muda kabla ya kuniruhusu kutumia ardhi yake katika ufugaji,” aeleza.

Kulingana na tafiti mbalimbali, ukosefu wa rasilimali za kilimo na ufugaji kama vile ardhi ni mojawapo ya changamoto kuu zinazoendelea kuwazonga wakulima na wafugaji wanawake wanaoishi katika mataifa yaliyoko Kusini mwa jangwa la Afrika.

Kulingana na Balozi Carla Mucavi, mwakilishi wa Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) nchini Kenya, vizingiti vingine ni pamoja na masuala mengine kama vile ukosefu wa elimu, na kutokuwa na uwezo wa kufikia huduma za mikopo na fedha.

Changamoto hizi, asema Dkt Susan Kaaria, Mkurugenzi katika shirika la Wanawake Waafrika katika utafiti na ustawi wa kilimo (AWARD), zimechochewa na masuala kadha wa kadha ya kijamii na kiuchumi, ambayo yanawazuia wanawake kutoshiriki vilivyo katika sekta hii.

Na hii, aeleza kwamba, imeathiri ushiriki wa wanawake katika sekta hii, licha ya kwamba kikundi hiki kinachangia pakubwa katika sekta hii eneo hili.

Kulingana na matokeo ya utafiti kwa jina- The Status of Women in Agrifood Systems yaliyowasilishwa miezi kadhaa iliyopita na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), licha ya kuwepo jitihada za kuwapa wanawake uwezo wa kushiriki vilivyo katika sekta ya kilimo na mifumo ya vyakula, pengo la kijinsia kati ya wanaume na wanawake inaendelea kusalia humu nchini.

Ripoti hii aidha inaonyesha kwamba japo sekta hii imeajiri watu wengi barani, tangu mwaka wa 2019 idadi ya wanawake walioajiriwa katika sekta hii imekuwa ikipungua.

“Kufikia mwaka wa 2019, asilimia 36 ya wanawake waliokuwa wakifanya kazi, ndio walikuwa wameajiriwa katika sekta ya mfumo wa uzalishaji vyakula. Hii inawakilisha upungufu wa asilimia 8 tangu mwaka wa 2005,” aeleza Bw Benjamin Davis, Mkurugenzi wa kitengo cha ustawi wa maeneo ya mashambani na usawa wa kijinsia katika shirika la FAO.

Ili kuleta mabadiliko, Dkt Kaaria asema, sauti za wanawake zinapaswa kupazwa kwa kuwahusisha katika maamuzi yanayohusiana na sekta hii, ili kuhakikisha kwamba sera za kilimo na ufugaji zinazohusisha masuala ya kijinsia, zinawakilishwa vilivyo,” aongeza Dkt Kaaria.

  • Tags

You can share this post!

Kawira Mwangaza: Dada zangu wote ni ‘singo’, hakuna...

Demu mpenzi wangu ananyemelewa baa anakofanya kazi....

T L