• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Kenya yakusudia kuchanja raia 5m kufikia Desemba

Kenya yakusudia kuchanja raia 5m kufikia Desemba

SERIKALI inalenga kutoa chanjo ya corona kwa watu milioni tano kati ya sasa na Desemba, mwaka huu, huku kaunti za Nairobi na Kiambu zikiongoza kwa kuchanja idadi kubwa.

Serikali imepanga kuchanja watu milioni 10 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa jumla ya watu 5,029,901 wamepewa chanjo. Kati yao, 3,545,060 wamepata dozi moja huku 1,484,841 wakiwa wamepata dozi zote mbili.

Watu 1,012,457 wamepata dozi ya kwanza ya chanjo ya corona jijini Nairobi huku 511,615 wakiwa wamepata dozi zote mbili. Serikali inalenga kuchanja watu milioni 3 wa kuanzia umri wa miaka 18 na zaidi jijini Nairobi.

Watu 139,943 na 322,519 wamepata dozi mbili na moja mtawalia katika Kaunti ya Kiambu.Kaunti ya Nyeri imechanja asilimia 14.7 ya watu wanaolengwa, Kiambu (asilimia 8.6), Uasin Gishu (asilimia 7.7), Nyandarua (asilimia 7.4), Kisumu (asilimia 6.9) na Mombasa (asilimia 6.5).

Katika eneo la Pwani, Kaunti ya Mombasa inaongoza kwa idadi ya watu waliochanjwa dozi zote mbili. Watu 52,379 wamechanjwa dozi mbili jijini Mombasa, Kilifi (15,506) na Taita Taveta (14,679).Kaunti za kaskazini mashariki mwa nchi na sehemu za Bonde la Ufa, hata hivyo, zinajikokota katika utoaji wa Chanjo ya Corona.

Ripoti ya wizara ya Afya iliyotolewa jana inaonyesha kuwa Kaunti za Pokot Magharibi, Mandera, Wajir, Garissa na Marsabit zimechanja chini ya asilimia moja. Kenya imepokea jumla ya dozi 8,006,820 za aina mbalimbali za chanjo ya corona, ikiwemo AstraZeneca, Johnson & Johnson, Moderna, Pfizer na Sinopharm iliyotengenezwa China.

Hiyo inamaanisha kuwa Kenya imesalia na takribani dozi milioni 3.Kenya inatarajia kupokea sehemu ya dozi milioni 50 za chanjo ya Moderna ambazo Amerika ilitangaza jana kuuzia Umoja wa Afrika (AU).

Amerika italeta dozi hizo barani Afrika kati ya sasa na mwishoni mwa mwaka ujao. Amerika ilikubali kuuzia AU dozi milioni 50 baada ya Rais Uhuru Kenyatta kukutana na kiongozi wa nchi hiyo Joe Biden katika Ikulu ya White House, Washington DC.

Rais Biden pia aliahidi kutoa msaada wa dozi milioni 17 za chanjo ya Johnson & Johnson.Jana, watu 151 walithibitishwa kuambukizwa virusi vya corona humu nchini na kufikisha jumla ya visa 252,839 tangu Machi mwaka jana, kisa cha kwanza kiliporipotiwa nchini.

Takwimu zilizotolewa jana na waziri wa Afya Mutahi Kagwe, zinaonyesha kwamba visa vipya vya maambukizi ya corona viliripotiwa katika kaunti 26. Kaunti ya Nairobi iliongoza kwa visa 30, Bomet (18), Meru (17) na Makueni (13).Watu watatu walifariki jana kutokana na matatizo yanayohusiana na maradhi ya corona na kufikisha jumla ya 5,263.

Asilimia 60 (watu 3,052) ya waliofariki kutokana na maradhi ya corona ni wazee wa kati ya umri wa miaka 60 na zaidi. Watoto wa chini ya miaka 10 waliofariki kutokana na corona humu nchini ni 58, wa kati ya miaka 10 -19 ni 38, 20-29 (141), miaka 30-39 (379), 40-49 (610) na 50-59 (985).

Watu 488 wamelazwa katika hospitali mbalimbali nchini wakitibiwa corona.

You can share this post!

Ndume 3 ulingoni kwa ndondi za Serbia

CHAKISTA mwenge thabiti wa Kiswahili katika Shule ya Upili...

T L