• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
KIGODA CHA PWANI: Changamoto nyingi zasubiri mawaziri wateule wa Nassir

KIGODA CHA PWANI: Changamoto nyingi zasubiri mawaziri wateule wa Nassir

NA PHILIP MUYANGA

HUKU wakitarajiwa kuhojiwa na bunge la kaunti na baadaye kuidhinishwa na kutwaa nafasi zao rasmi, mawaziri wateule wa serikali ya Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir watakumbana na changamoto si haba.

Mawaziri hao wateule wanatarajiwa kuimarisha utendakazi wa idara mbalimbali za kaunti na pia kujaribu kuweka taswira mpya ya serikali ya Bw Nassir na kuondoa ile iliyokuwa inaonekana ya gavana wa zamani Bw Hassan Joho.

Licha ya hayo mawaziri hao wateule pia wanatarajiwa kumsaidia Bw Nassir kutimiza ahadi alizotoa katika kampeni zake na manifesto yake za kuimarisha huduma ambazo serikali ya kaunti inatoa kwa wananchi.

Ujuzi wa kutosha

Swali linalojitokeza na kuwa mojawapo ya changamoto mawaziri hao wateule watakumbana nayo ni iwapo wako na ujuzi wa kutosha wa utendakazi wa majukumu ambayo wamekabithiwa.

Mawaziri wateule hao pia wanatarajiwa kukabili changamoto ya kuweza kuhakikisha huduma za kila idara wanayoiwakilisha zinafikia mwananchi hadi katika vitongoji duni na sio mitaa ya mjini peke yake.

Hii ni kwa kuwa hapo awali kulikuwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi ya kuwa baadhi ya huduma za kaunti zilikuwa hazifiki mashinani wakihoji kuwa kaunti ya Mombasa sio mitaa ya mjini peke yake.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, changamoto nyingine itakayowakumba mawaziri wateule ni matarajio makubwa wananchi wako nayo kuwahusu kwani kile wao (wananchi) wanahitaji ni huduma bora.

Wachanganuzi hao wa siasa wasema kuwa itakuwa bora kila waziri aliyeteuliwa kuweka maafisa katika kila idara wanayoisimamia ambao kazi yao itakuwa ni kutembea mitaani na vitongojini kusikiliza mahitaji ya wananchi.

“Ni vyema kwa mfano idara na masuala ya maji kuwa na maafisa wake nyanjani wa kuongea na wananchi hata kama ni siku mbili tu kila wiki ili wapate kujua shida zinazowakabili na iwapo wanapata huduma za maji,” alisema mchanganuzi mmoja wa siasa ambaye alitaka jina lake libanwe kwa sababu za kibinafsi.

Kulingana na Prof Hassan Mwakimako ambaye ni mhadhiri katika chuo kikuu cha Pwani kilicho kaunti ya Kilifi,ni muhimu mawaziri wateule wafahamu kuwa miaka kumi iliyopita utoaji wa huduma katika kaunti ya Mombasa ulikuwa umeenda chini sana.

Prof Mwakimako alisema kuwa suala hili lilikuwa limefanya wananchi kukosa imani na serikali za ugatuzi na kwamba itakuwa bora mawaziri wateule hao lazima waweke bidi kuregesha imani hiyo.

“Itakuwa muhimu kwa mawaziri wateule hao kuanza tena kuregesha imani ya wananchi wa Mombasa na serikali ya ugatuzi,wanafaa kujitahidi katika kutoa huduma bora kwa wananchi,” alisema Prof Mwakimako.

Aliongeza kusema kuwa itakuwa bora mawaziri hao wateule kuanganzia kero zinazowakumba wananchi husuan kupeanwa kwa huduma kama vile maji, usafi wa mji na nyinginezo.

Pia aliongeza kusema kuwa mawaziri wateule hao wanafaa kuangalia huduma zilizogatuliwa kama vile za masomo ya chekechea wakizingatia kuwa kaunti zingine zimefanya vizuri katika idara hiyo na itabidi waonyeshe kuwa wanajitahidi kutoa huduma hizo.

Licha ya hayo, alisema kuwa bunge la kaunti liko na jukumu la kuangalia utenda kazi wa mawaziri wateule kuhakikisha kuwa hawapiti mipaka wakati wanapotekeleza majukumu yao.

“Jukumu lingine ni kuangalia kuwa raslimali za umma zinatumika kulingana na mipango na sheria. Pia wanajukumu kubwa kuhakikisha mawaziri hao wanatenda kazi kulingana na matarajio ya kisheria,” alisema Prof Mwakimako.

Mawaziri wateule ni pamoja na Naibu Gavana Bw Francis Thoya ambaye atasimamia idara ya Mazingira na usimamizi wa taka, nafasi ambayo amekuwa akiishikilia kwa muda tangu wachaguliwe kuongoza Mombasa.

Safisha mji

Bw Thoya amekuwa akiongoza maafisa wa kaunti katika shughuli za kusafisha mji wa Mombasa na kufunga sehemu za kutupa taka zilizoanzishwa kinyume cha sheria.

Wengine walioteuliwa ni Emily Achieng (Maji, Mali Asili na Hali ya Hewa), Kenneth Muigai (Huduma ya Umma,Vijana, Jinsia na Michezo), Kibibi Abdallah (Uchumi Samawati, Kilimo na Ufugaji), Bw Mohamed Osman (Utalii, Utamaduni na Biashara), Dkt Mbwarali Kame (Elimu na Masuala ya Kidijitali), Evans Oanda (Fedha na Uchumi) Dkt Swabah Ahmed (Afya) na Daniel Otieno Uchukuzi na Miundomsingi).

Mwanaharakati wa haki za kibinadamu ambaye pia ni kasisi Bw Gabriel Dolan anasema kuwa kuteuliwa kwa mawaziri hao ni mwanzo mpya kwa kuwa wananchi wengi walitaka timu ya zamani kuondoka.

Kasisi Dolan aliongeza kusema kuwa changamoto nyingine ni kuwa mawaziri wengine hawana ujuzi na uzoefu wa kazi hizo.
Aliongeza kusema kuwa changamoto nyingine zitakazo wakumba mawaziri walioteuliwa katika serikali ya Bw Nassir ni deni la kaunti ambalo kwa sasa ni takriban Sh5 bilioni.

Nyumba

Kasisi Dolan alisema kuwa changamoto nyingine iko katika idara ya nyumba na kwamba itakuwa muhimu waziri mteule wa masuala ya ardhi na makao kuhusisha watu katika mipango ya wizara hiyo atakapoidhinishwa.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa matatizo yanayokumba Mombasa ni mengi na yanahitaji ujasiri mkubwa kutoka kwa mawaziri walioteuliwa kuweza kuyatatua kwa niaba ya Gavana Nassir.

Wanaongeza kusema kuwa mawaziri hao wateule ni lazima wajitokeze kijasiri na kuchukuwa nyadhifa zao na kuhakikisha changamoto zinazokumba jamii katika kila sekta kama vile afya, elimu, usafi na mazingira zinatatuliwa.

  • Tags

You can share this post!

MIKIMBIO YA SIASA: Pigo kwa Azimio Jubilee ikizidi kuzama...

DARUBINI YA WIKI: Toleo Nambari 21 | Januari 22, 2022

T L