• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
KIKOLEZO: Wa-totos na pesa

KIKOLEZO: Wa-totos na pesa

Na THOMAS MATIKO

KUWA mwanamitindo ni jambo moja, ila kufanikiwa kwenye tasnia hiyo ya ulimbwende ni suala lingine tofauti kabisa.

Wapo maelfu ya modo wanaofanya vizuri tu katika tasnia hiyo ila kuna masupa-modo wachache sana.

Hili ni tabaka la modo waliofanya juhudi za ziada kujiongezea mafanikio na kwenye harakati hizo wakaishia kuwa matajiri kupindukia. Kwa mujibu wa Celebrity NetWorth, hii hapa listi ya wanamitindo matajiri kupindukia duniani, wengi wao wakiwa ni masupa-modo.

NAOMI CAMPBELL, 51 (Uingereza)

Utajiri: Dola 80 Milioni (Sh8.8B)

Kwenye listi hii, pengine Naomi ndiye modo maarufu zaidi anayefahamika na Wakenya wengi. Supa-modo huyu Mwingereza aliweza kufanikiwa licha ya kuibuka miaka ya 90 nyakati ambazo ubaguzi wa rangi ulikuwa mbaya sana.

Kipaji chake kilitambuliwa na mwasisi wa kampuni ya fasheni ya Versace, Gianni Versace. Gianni aliyeuawa 1997, ndiye aliyemfunza masuala mengi tu kuhusu ulimbwende. Ndio sababu alipata umaarufu sana kwa kutokea kwenye shoo nyingi za fasheni. Ni mmoja wa masupa-modo sita tu duniani.

Sita hawa walipewa taji hilo kutokana na mchango wao mkubwa kwenye tasnia ya ulimbwende. Naomi ni tajiri mkubwa na anaaminika kumiliki jumba la kifahari kule Malindi. Pia ndiye balozi wa utalii nchini Kenya kupitia brandi ya Magical Kenya.

LINDA EVANGELISTA, 56 (Canada)

Utajiri: Dola 40 Milioni (Sh4.4B)

Ni moja kati ya sura zilizokuwa maarufu sana miaka ya 90 kwenye tasnia ya uwanamitindo. Ni miongoni mwa masupa-modo wachache waliopo.

Katika taaluma yake, raia huyu wa Canada alifanikiwa kuzivaa jalada za majarida maarufu, zaidi ya 700. Kwa asiyeelewa, suala la staa kuvaa jalada la majarida maarufu huambatana na malipo makubwa mno. Linda anashikilia rekodi ya kuvaa jarida la Vogue Italia mara kadhaa.

Aliondokea kuwa kipenzi cha Vogue Italia kutokana na mauzo waliopata kila alipovaa jalada lao. Aliwahi kunukuliwa akisema kuwa, kazi ya pekee inayoweza kumtoa kitandani ni inayomlipa zaidi ya dola 10,000 (Sh1 milioni). Kumbuka ni enzi hizo.

Alistaafu 1998 na kisha kurejea tena miaka mitatu baadaye. Bado anajihusisha na uwanamitindo ila sio kwa bidii kama zamani.

CHIRISTIE TURLINGTON, 52 (Marekani)

Utajiri: Dola 40 Bilioni (Sh4.4B)

Ni supa-modo mwingine aliyesumbua sana miaka ya 90. Toka 1989 hadi 2014 kampuni ya mavazi ya dizaina ya Calvin Klein ilimtumia sana kutangaza bidhaa zake.

Pia aliwahi kuwa balozi wa bidhaa za kampuni ya vipodozi Maybelline.

Mwaka 2014 aliorodheshwa miongoni mwa watu 100 maarufu duniani na jarida la Times 100.

Alizivaa jalada za majarida kibao likiwemo Vogue. Baada ya miaka mingi kwenye gemu, alistaafu na kuwa mke nyumbani. Kaolewa na mwigizaji Edward Burns na kwa pamoja wana watoto wawili.

KATE MOSS, 48 (Uingereza)

Utajiri: Dola 70 Milioni (Sh7.7B)

Jina lake la utani ni ‘Kate The Great’. Talanta yake ilitambuliwa alipokuwa katika uwanja wa ndege wa JFK kule Marekani. Alikuwa na umri wa miaka 14 pekee. Kate anatajwa kuwa kitinda mimba wa nyakati za masupa-modo akijipatia umaarufu kwenye kipindi cha lala salama katika miaka ya 90.

Umaarufu wake ulichangiwa na ubalozi wake wa bidhaa za ‘heroin chic’.

Alifanya kazi pia na Calvin Klein. Kadumu kwenye gemu kwa zaidi ya miaka 25. Lakini pia alijizidishia umaarufu kutokana na maisha yake ya kupenda starehe na anasa. 2005, kampuni kadhaa za uwanamitindo ziliacha kufanya kazi naye kufuatia madai kuwa ni mtumizi wa dawa za kulevya.

Alijitetea na kufanikiwa kurudi kwenye gemu. 2012 jarida la Forbes lilimworodhesha miongoni mwa wanamitindo wanaopiga mkwanja mrefu kwa mwaka.

Kwa mfano mwaka huo, alikadiriwa kuingiza dola 9.2 milioni.

ALESSANDRA AMBROSIO, 40 (Brazil)

Utajiri: Dola 80 Milioni (Sh8.8B)

Alianza shughuli zake za uwanamitindo 1999 na mpaka sasa hajastaafu. Umaarufu wake aliupata kutokana na kutangaza mavazi ya ndani al-maarufu ‘lingerie’ ya kampuni ya Victoria Secret.

Alifanya kazi nao toka 2004 hadi 2017. Lakini pia amefanya kazi na kampuni zingine za bidhaa za kidizaina kama vile Christian Dior, Ralph Lauren na Next.

Forbes ilimworodhesha katika nafasi ya tano kwenye listi ya modo wanaotengeneza mkwanja mrefu. Kwa mwaka, Ambrosio anakadiriwa kuingiza dola 6.6 milioni.

TRYA BANKS, 47 (Marekani)

Utajiri: Dola 90 Milioni (Sh9.9B)

Alipoanza taaluma yake ya uwanamitindo, kampuni tano kubwa za uwanamitindo zilimkataa kule Los Angeles. Baada ya kukataliwa hakufa moyo. Alipata mchongo wa kwenda kufanya uwanamitindo kwingineko na ndivyo alivyohamia Milan, Italia.

Huko ndiko kipaji chake kilinoga na hata zile kampuni za Marekani zilizokuwa zimemkataa awali, zikaanza kufanya kazi naye.

Mwaka 2003, alianzisha shoo yake ya America’s Next Top Model kusaka vipaji vipya.

Ni shoo iliyoshika kasi na kumwongezea umaarufu. Kando na kuwa mwanamitindo, Tyra alijibadilisha na kuwa Mcee, mwigizaji na pia produsa wa vipindi.

TANBIHI: Modo wengine matajiri ni pamoja na Mjerumani Heid Klum, Cindy Crawford, Gisele Bundchen, Kathy Ireland na Christie Brinkley. Kila mmoja wao ana utajiri usiopungua dola 100 (Sh10.1B). Hata hivyo wengi wao utajiri wao haukuchangiwa tu na shughuli za uwanamitindo.

You can share this post!

Wazee wakemea mzozo wa ugavana Wajir

Wafyonzaji wa mafuta kutoka kwenye bohari wakamatwa jijini