• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Wafyonzaji wa mafuta kutoka kwenye bohari wakamatwa jijini

Wafyonzaji wa mafuta kutoka kwenye bohari wakamatwa jijini

Na SAMMY KIMATU

WASHUKIWA kumi wamekamatwa na polisi kwa kudaiwa kufyonza mafuta katika bohari moja katika Eneo la Viwanda, Kaunti ya Nairobi mnamo Alhamisi.

Aidha, mafuta lita 25,000 yalitwaliwa wakati wa operesheni kali iliyoongozwa na mkuu wa polisi wa Jinai eneo la Makadara, Bw Steven Mutua.

Bw Mutua alishirikiana na maafisa wa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta Nchini (EPRA).

Akithibitisha kisa hiki, mkuu wa polisi katika divisheni ya Makadara, Bw Timon Odingo aliambia Taifa Leo kwamba msako huo ulifanyika katika kiwanda kimoja bandia mkabala wa barabara ya Ragwe.

Kando na hayo, Bw Odingo alisema magari sita likiwemo moja la serikali, jenereta tano, mitungi 97, pipa nne za diseli, mapipa saba ya mafuta taa huku pipa sita zikijaa mafuta ya taa na pipa moja likiwa limejaa nusu yake.

Isitoshe, Bw Odingo aliongeza kwamba maafisa wake walinasa mitungi 17 ya lita 20 kila moja bila kuwa na chochote ndani.

“Washukiwa wote kumi walipatikana wakijaza mafuta aina ya dizeli, mafuta ya taa na petroli katika bohari moja mkabala wa barabara ya Rangwe. Tumenasa magari yaliyohusika sawia na vifaa walivyokuwa navyo vya kufyonza mafuta,” Bw Odingo akanena.

Fauka ya hayo, Bw Odingo alisema washukiwa wote kumi wamefungiwa katika kituo cha polisi cha Industrial Area huku uchunguzi zaidi ukifanywa.

“Tunachunguza kesi hii ili kuona ikiwa tutawakamatwa wote wanaohusika katika biashara hii haramu. Tunaamini hii biashara haramu imeendeshwa chini ya maji tangu miaka 20 iliyopita,” Bw Odingo akanena.

Bw Odingo aliongeza kwamba ndani ya bohari katika upande mmoja, washukiwa waliendesha biashara ya mifuko ya plastiki.

“Wanahusika kuosha mifuko ya plastiki iliyotumika kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kisha wanaibadilisha kuunda bidhaa,” Bw Odingo akaeleza.

Magari yaliyonaswa ni pamoja na lori aina ya Mitsubishi Fuso KBC 167 (la kubebea mafuta) linalomilikiwa na Marklove Njoki, Isuzu KAJ 805 L (la kubebea mafuta) la Mwami Agencies.

Vile vile, magari mengine yaliyokamatwa ni Isuzu aina ya FRR- KBM 877B (la kubebea mafuta), pick-up KXT 492, lori la NMS-GK B 350W aina ya FAW na lori aina ya Mitsubishi Fuso KCM 240 A linalomilikiwa na Black Petal Flowers.

Malori yaliyonaswa. Picha/ Sammy Kimatu

Bw Odingo aliongeza kwamba washukiwa walihatarisha maisha yao na Wakenya wasio na hatia kwa kuwasha jenereta huku wakijaza mafuta akisema janga la moto linaweza kusababishwa kwenye eneo la tukio sawa na Eneo la Viwanda vyenyewe.

You can share this post!

KIKOLEZO: Wa-totos na pesa

MAPISHI: Weledi jikoni, vidokezo muhimu unavyopaswa kujua