• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
DINI: Katika hali zote zinazokupata kumbuka kila kitu hutendeka kwa kusudi la Mungu

DINI: Katika hali zote zinazokupata kumbuka kila kitu hutendeka kwa kusudi la Mungu

Na PADRE FAUSTIN KAMUGISHA

YANAYOKUPATA unayapokeaje?

Ukipata mateso ni asilimia kumi, unavyoyapokea ni asilimia tisini. Unayapokeaje?

Ukiyapokea kwa imani na uvumilivu, unamtukuza Mungu.

Ukikata tamaa, haumtukuzi Mungu. Kushindwa, hakumtukuzi Mungu.

Kutoyakabili matatizo, hakumtukuzi Mungu.

Kuamua kulala na kutofanya lolote, hakumtukuzi Mungu.

Eliya alipopata matatizo aliyapokea kwa kukata tamaa. Tunasoma hivi katika Biblia: “Eliya ajiombea roho yake afe. Akasema, ‘yatosha sasa’.

Malaika akamgusa akamwambia, ‘Inuka ule’.” (1 Wafalme 19:4-9)

Eliya maana yake ni: Mungu ametukuzwa.

Kuna wakati Eliya hakuishi kuambatana na maana ya jina lake. Alikata tamaa.

Eliya hakuamini kuwa Mungu atamwepusha na mpango wa mauaji kutoka kwa Yezebeli, mwanamke Katili.

Eliya alimfufua mwana wa mjane wa Sarepta. Kwa maombezi ya Eliya pipa la unga la mjane huyo halikupungua wala chupa ya mafuta haikuisha.

Istoshe, aliwashinda manabii wa uongo wa Baali aliyeabudiwa kama muungu wa mlima Karmeli.

Eliya angehesabu mafanikio hayo kwa mkono wa Mungu asingekata tamaa.

Lakini baadaye imani yake kwa Mungu ilihuishwa, akasonga mbele.

Matatizo yanapokupata yapokee kwa imani.

“Bwana amefanya kila kitu kwa kusudi lake.” (Mithali 16: 4).

Yanapokupata kuna kusudi la Mungu. Amini tu anakupeleka mahali pazuri.

Kila hali uliyomo Mungu yuko kazini. Amini!

Kila linalokupata Mungu yuko kazini. Hashitukizwi.

Kila tatizo lina mlango wa kutokea.

Mkweaji alidondoka kutoka kwenye mwamba uliochongoka.

Alivyoanguka ghafla kwa vurumai alishikilia tawi la mti, miguu ikielea kwenye korongo.

Alipiga kelele: “Kuna mtu juu huko anisaidie?”

Sauti ilisikika, “Nitakusaidia mwanangu, kwanza kuwa na imani na mimi.”

Mkweaji alijibu: “Nakuamini.”

Mungu alimjibu, ‘Achia tawi’.”

Palikuwepo na kimya cha muda mrefu.

Baadaye, mkweaji alisema: “Hakuna mwingine wa kunisaidia huko juu?”

Hakuachilia tawi. Kuna tawi watu hawataki kuachilia. Tawi linaweza kuwa imani katika nguvu za giza.

“Kila amwaminiye Bwana ana heri.” (Mithali 16:20).

Baadhi ya watu wanaamini katika Mungu lakini hawamwamini Mungu. Yajapo majaribu mwamini Mungu.

Usiamini tu mafundisho juu ya Mungu, mwamini Mungu mwenyewe.

“Imani haijui kamwe inapopelekwa, lakini inapenda na kumjua yule anayeongoza,” alisema Oswald Chambers.

Kutokujua Mungu anapokupeleka ni sehemu ya imani. Wewe mwamini anayekupeleka. Mwache awe namba moja. Mengine yatajiweka sawa.

“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe; katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:6).

Yanapotokea yakapindisha mapito yako, yeye atayanyosha.

“Yeye ni ngao yao wamwaminio” (Mithali 30: 5). Punde tu ukiamini, tayari unamfanya Mungu ngao yako. Yajapo mapito yapokee kwa busara. Sir Harry Lauder, mchekeshaji wa Kiskoti alimpoteza kijana wa kiume wakati wa Vita ya Kwanza ya Dunia.

Habari za kuvunja moyo zilipomfikia alisema: “Nyakati kama hizi mtu ana namna tatu za kupokea mambo. Kwanza, anaweza kukata tamaa na kuwa mkali kwa dunia na kuwa mlalamikaji. Pili, anaweza kumaliza huzuni yake katika kunywa pombe au maisha ya ukaidi na uovu. Tatu, ni kumrudia Mungu. Kumrudia Mungu ni busara.”

Biblia Takatifu inashauri: “Busara itakulinda” (Mithali 2: 11).

Yapokee matatizo kwa busara. Yapokee majaribu kwa busara. Yapokee mateso kwa busara. Eliya alipokata tamaa hakutenda kwa busara. Alitamani kufa. Alilala na kuacha kufanya kazi. Alikaa na tatizo muda mrefu. Alilipokea kama udongo wa mfinyanzi, ambao hukaa na maji muda mrefu.

Laiti angelipokea kama udongo wa mchanga, ambao hukaa na maji kwa muda mfupi tu.

“Busara ni sanaa ya kujua jambo la kutotilia maanani” (William James).

Naye mwanafalsafa Epictetus anaongeza: “Ni mtu mwenye hekima ambaye halilii vitu ambavyo hana, bali anafurahia vitu alivyo navyo.”

Mpendwa msomaji, mabaya usiyafanye “miungu” kwa kuyaabudu na kuyaongelea sana.

You can share this post!

Huzuni tele ajuza waliouawa kwa madai ya uchawi wakizikwa

Mbinu za Uhuru kuzima Ruto

T L