• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 6:55 AM
Kilimo cha wadudu tiba ya udongo kwa zao bora

Kilimo cha wadudu tiba ya udongo kwa zao bora

NA RICHARD MAOSI

VERMICULTURE ni teknolojia ya kufuga wadudu wa aina ya earthworms kwa manufaa ya kurutubisha udongo kwa ajili ya kukuza aina mbalimbali ya mimea.

Ikumbukwe kuwa wadudu hawa hula kila aina ya mimea na hatimaye kutengeneza mbolea kwa kuvunjavunja mabaki ya vyakula, hii ikiwa ni njia mojawapo ya kuongezea thamani mabaki ya viasilia.

Kwa wakati huo, mbolea inayotokana na wadudu hatunza mazingira kwa kupunguza visa vya takataka kuzagaa.

Aidha, wakulima wanahimizwa kujifunza njia mbalimbali ya kuwafuga wadudu hawa ambao huchukua muda mfupi kabla ya kuzaana, hii ikiwa ni kwa kuwalisha aina mbalimbali ya mabaki ya vyakula kama matawi ya mboga na nyasi.

Bw Dominic Kimani, mtaalam wa kilimo biashara kutoka Seed Savers Network Kenya anasema amekuwa akiwasaidia wakulima wengi kutoka eneo la Gilgil kuendesha kilimo endelevu asilia bila kemikali.

Anasema kuna manufaa mengi kwa mkulima akijifunza kutengeneza mbolea kutokana na wadudu, kwanza ikiwa ni kujiepusha na kero la kutegemea mbolea za viwandani ambazo mara nyingi huwa zimejaa kemikali.

Pili, husaidia kulainisha udongo na kuruhusu hewa safi ya oksijeni kupenya, jambo ambalo husaidia udongo kuyabeba maji kwa muda mrefu, ikizingatiwa kuwa udongo huwa umebeba virutubishi vingi vya matawi pamoja na nyasi.

Bila kusahau mkulima anatakiwa kunyunyizia sehemu hii maji kila wakati ili kutengeneza unyevu ambao hutoa fursa nzuri kwa wadudu kuzaana mara 300 katika kipindi cha miezi miwili tu.

“Mbolea yenyewe inapotumika shambani husaidia mizizi ya mimea kupenya hadi katika kina kirefu cha ardhi na kufikia virutubishi vya ziada ndani ya mchanga,” anasema Kimani.

Wadudu hawa wanaweza kutumika wakati wa kuunda mbolea ili kurutubisha udongo na kwa wakati huo kuhakikisha kuwa mazao yanadumisha ubora na kubakisha hali yao ya asilia.

Kulingana na Kimani, mimea kama vile mihogo, vitunguu inahitaji kiwango kikubwa cha madini ya phosphorus kutengeneza mizizi na mashina ambayo ni dhabiti.

Pili, madini ya phosphorus husaidia mimea kukabiliana na uwezekano wa kuvamiwa na wadudu na maradhi ambayo mara nyingi hufanya mimea kulegea na kudhoofika.

Hii ikimaanisha kuwa mkulima anaweza kuwalisha wadudu wake kwa kuyatumia mabaki ya maharagwe, maganda ya njugu au masalia ya wanyama kama vile samadi ambayo huwa yameja madini ya phosphorus.

Kulingana na Kimani, ni rahisi kutengeneza aina hii ya mbolea ambapo katika hatua ya kwanza mkulima atahitajika kutengeneza kibanda cha kuwasitiri wadudu wake.

Pili atenegeneze makasha ambayo huwa yamejazwa udongo kisha ukachanganywa na samadi kutoa muda kwa wadudu kuzaana.

Anasema kuwa ukubwa wa eneo la kuwafuga wadudu wake unategemea mambo mengi mojawapo ikiwa ni upatikanaji wa takataka au mabaki ya viasilia yanayotumika kuwalisha.

“Eneo la kuwafugia wadudu linafaa kuinuliwa takriban mita mbili kutoka kwenye ardhi, kuwakinga wadudu dhidi ya maji hususan mvua inaponyesha,” akasema.

Kulingana na Kimani mkulima anatakiwa kufunika sehemu yenye kufugia wadudu aidha kwa kutumia neti maalum ya tandarua yenye matundu ili kutoa nafasi kwao kupumua vyema.

Pia kupitia hali hii atakuwa amewakinga wadudu wake dhidi ya kudonwa au kuliwa na ndege kama vile mwewe au tai ambao mara nyingi wanapenda kula wadudu.

  • Tags

You can share this post!

Shule ya msingi ya Jamhuri, Thika kugeuzwa iwe ya upili

Wanafunzi wateta kwa kunyimwa haki

T L