• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 PM
Kingi apata jukwaa kupaa na kuwa kiongozi wa taifa

Kingi apata jukwaa kupaa na kuwa kiongozi wa taifa

NA PHILIP MUYANGA

JE, kuwekwa saini kwa mkataba wa ushirikiano baina ya chama cha Pamoja African Alliance (PAA) na kile cha Jubilee ambavyo viko chini ya muungano wa Azimio la Umoja kumemuinua kisiasa gavana wa Kilifi Amason Jefa Kingi?

Hili ni swali lililoibuka kuhusu iwapo Bw Kingi amejitosa katika siasa za kitaifa huku akilenga kuwa kiongozi anayesikika kutoka Pwani.

Kuwepo kwake kama mmoja wa vinara wa vyama vya kisiasa waliokaribishwa jukwaani na Rais Uhuru Kenyatta kuwahutubia wajumbe wa chama cha Jubilee katika mkutano wao, kumeonekana kusisimua mchakato wa siasa za Bw Kingi ambao ulikuwa umeonekana kufifia.

Kuwahutubia wajumbe wa chama cha Jubilee katika hafla hiyo iliyopeperushwa moja kwa moja katika televisheni kulionekana kuondoa fikra za wengi kuwa Bw Kingi alikuwa ameenda chini kisiasa kuanzia siku ambayo alitimuliwa kama mwenyekiti wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) katika Kaunti ya Kilifi miezi saba iliyopita.

Swali lingine linaloibuka ni iwapo Bw Kingi atakuwa amempiku Gavana wa Mombasa Hassan Joho kama mwanasiasa tajika mwenye usemi katika eneo la Pwani kwa wakati huu kwa kuwa sasa anacheza ‘ligi’ ya vinara wa vyama.

Baada ya kuweka saini makubaliano ya ushirikiano na chama cha Jubilee, Bw Kingi ameonekana kuchangamka kisiasa huku wandani wa chama cha PAA wakieleza kuwa wapo katika meza ya kitaifa kujadili masuala yanayowakumba wapwani.

“Kwa sasa Bw Kingi yuko katika meza ya kisiasa ya kitaifa ndiposa anaendeleza mchakato wa kutaka masuala ya Pwani yaangaziwe kitaifa,” alisema mwanachama mmoja aliyetaka jina lake libanwe.

Hata hivyo, kuimarika kwa Bw Kingi kisiasa kulionekana kutowapendeza baadhi ya viongozi Pwani ikitiliwa maanani kuwa hivi majuzi wanachama wa chama cha PAA hawakuruhusiwa kuhudhuria mikutano ya kiongozi wa ODM Raila Odinga alipozuru Pwani.

Wandani wa PAA wanasema kuwa kutoruhusiwa kwao katika ziara ya Bw Odinga kulionyesha kuwa ni mojawapo wa njia za kujaribu kumzuia Bw Kingi kutokuwa maarufu kisiasa Pwani.

“Ukweli usemwe,kama kiongozi wa PAA,Bw Kingi atajadiliana na viongozi wengine wa vyama vya kisiasa nchini kwa meza moja,”alisema mwanachama huyo wa PAA.

Aliongeza kusema kuwa gavana huyo wa Kilifi ndiye kinara wa siasa za Pwani.

Kabla ya ziara hiyo ya Bw Odinga, viongozi wa chama cha ODM Kilifi walise – ma kuwa mkutano wa Bw Odinga uliotarajiwa kufanywa siku ya Jumamosi ulikuwa umetokana na mwaliko wa chama chao pekee na sio kundi nzima la Azimio la Umoja.

“Azimio (la Umoja) lipo, linao wanachama wengi. Kwa sasa, mkutano huu unaokuja ni chama cha ODM kili – chomualika Baba,” alisema Bw Joseph Chilumo, naibu mwenyekiti wa chama cha ODM Kilifi.

Kulingana na mkataba wa ushirikiano baina ya PAA na Jubilee, chama cha PAA kinapigania utatuzi wa shida ya ardhi eneo la Pwani, uchumi wa Pwani na wapwani kupitia viongozi wao kuwa katika serikali ya kitaifa.

Chama cha PAA kiliongeza kusema kuwa iwapo masuala yote yatakubalika,basi itaweka mkataba wa kabla ya uchaguzi na vyama vyenye maono sawa na yake chini ya mwavuli wa Azimio La Umoja.

Katika ziara ya eneo la Rabai hivi majuzi, Bw Kingi alimpigia debe Bw Odinga huku akijaribu kuzima umaarufu wa naibu Rais William Ruto wa United Democratic Alliance (UDA).

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, kumpigia debe Bw Odinga kutamuinua kisiasa Bw Kingi kwani kinara huyo wa ODM bado yuko na ushawishi mkubwa katika eneo la Pwani.

Katika mkutano wa kinara wa ODM mjini Naivasha mnamo Januari 17, Bw Kingi pamoja na baadhi ya magavana wengine walisema kuwa wanamuunga mkono Bw Odinga kuchaguliwa kuwa rais.

“Sisi kama magavana kupitia mwavuli wa Azimio la Umoja, tumekubaliana tukirudi mashinani gavana baada ya gavana tutaweka mikakati katika kaunti zetu kuona kwamba tunazungumza na kuhamasisha umma katika kaunti zetu,” alisema Bw Kingi wakati huo.

Kuimarisha umaarufu wake, chama cha PAA kinatarajiwa kuweka wagombea viti katika kila nafasi isipokuwa ile ya urais.

Tayari wakili George Kithi ndiye atakayepeperushwa bendera ya PAA katika kuwania kiti cha ugavana Kaunti ya Kilifi. Kulingana na mshauri wa masua – la ya kisiasa Bozo Jenje, Gavana Kingi ni mwanasiasa wa kutumia fursa inapojitokeza na wala sio kuwa ni maarufu.

“Amejihusisha na chama cha Jubilee lakini sio lazima kuwa atafaidika pakubwa na ushirikiano huo, labda atapata faida kidogo.

“Bw Kingi ni mwanasiasa anayetafuta fursa, ambaye aliona kuwa alikuwa haendelei kisiasa, aliangalia kiujanja njia mwafaka ya kujitoa katika hali hiyo,” alisema Bw Jenje.

Aliongeza kusema kuwa umaarufu wa Bw Kingi hautafikia ule wa Bw Joho kwani naibu kiongozi huyo wa chama cha ODM yuko katika upeo wa juu wa vuguvugu la Azimio la Umoja.

Mshauri wa masuala ya mawasiliano Bw Mwakera Mndwamrombo alisema kuwa Bw Kingi kutumia chama cha PAA ndio njia pekee kwake yakuonekana katika miundo ya miungano ya siasa inayoendelea kabla ya uchaguzi wa Agosti 9.

  • Tags

You can share this post!

Serikali yatangaza mlipuko wa homa ya manjano, watu 15...

Mfalme mpya wa Tokyo Marathon Kipchoge aomba amani duniani

T L