• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
KINYUA BIN KING’ORI: Raia wanasubiri serikali ya Uhuru itekeleze ahadi zake

KINYUA BIN KING’ORI: Raia wanasubiri serikali ya Uhuru itekeleze ahadi zake

Na KINYUA BIN KING’ORI

UCHAGUZI uliopita wa 2017 Wakenya walichagua serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais Dkt William Ruto, kutokana na misingi ya sera na raia kusadiki ahadi zao.

Uchaguzi wa 2022 unakaribia, ambapo Rais uhuru atastaafu baada ya kukaa mamlakani kwa miaka 10. Lakini Rais, naibu wake na maafisa wake serikalini lazima watambue serikali yao imefelisha Wakenya na hawana budi kujikaza kutekeleza ahadi zao kwa kipindi kifupi kilichosalia

Kipindi cha kwanza waliahidi kununua vipatakilishi kwa wanafunzi wote wa shule za msingi na sekondari, kujenga viwanja vya kisasa vya michezo kwa kila kaunti, kuhakikisha wananchi wote ambao waliondolewa katika ardhi zao ili kuwezesha ujenzi wa reli wamelipwa bila kudhulumiwa miongoni mwa nyingine.

Lakini kufikia sasa hakuna vipatakilishi shuleni, baadhi ya wananchi wameendelea kulalama kukosa malipo hayo ya mradi wa SGR.

Inasikitisha kuona wananchi wakipuuzwa na viongozi pamoja na serikali. Tujue wengine walikubali ardhi yao kutumika baada ya kujua watalipwa, sasa leo hii wema wao umewaponza.

Serikali ya Jubilee imefeli kwa kupuuza ahadi zake zikiwemo ajenda kuu nne na kuanzisha handisheki na mchakato wa BBI ilikuwa njama iliyofaulu kufanya wananchi wasahau walichoahidiwa.

Lakini inaendelea kusikitikisha kuwa serikali hii inaendeleaa kutoa ahadi bila kujali ni lini zitatimizwa.

Ahadi za hivi karibuni ni ahadi zilizowekwa na Wizara ya Elimu kupitia waziri Prof George Magoha, kuhusu kusambaza madawati na barakoa katika shule za msingi na sekondari kote nchini.

Shule kote nchini zimefunguliwa Lakini msongamano unaoshuhudiwa shuleni tangu wanafunzi warejee shuleni, ni ushahidi hakuna madarasa mapya yamejengwa au kusambazwa kwa madawati ya kutosha.

Pia, barakoa zilizoahidiwa kuwafaa wanafunzi maskini hazijafikia shule mashinani au vijini.

Kumekuwa na madai ya ufisadi kuhusiana na fedha za kudhibiti msambao wa corona na ingawa tuliahidiwa kuwa hatua zitachukuliwa dhidi ya washukiwa, tungali tunasubiri kuona mwelekeo kuhusiana na hilo.

Rais Kenyatta na Dkt Ruto wajue kuwa Wakenya huenda wakose kuwasamehe ikiwa miaka 10 itaisha bila wao kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Kwa sasa, viongozi wetu wanafaa kufahamu kuwa malumbano yao kuhusiana maridhiano ya Rais Kenyatta na Bw Odinga pamoja na suala la BBI serikalini si muhimu kwa umma. Muhimu sasa ni ahadi kutekelezwa kupiga jeki uchumi na maendeleo nchini.

You can share this post!

COVID-19: Mmoja afariki, serikali yathibitisha visa vipya...

KAMAU: Kapedo: Vijana wakabili desturi zinazowadunisha