• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
KIRDI: Sekta ya viwanda itaimarika wanafunzi wakipaliliwa mbinu kuongeza bidhaa thamani  

KIRDI: Sekta ya viwanda itaimarika wanafunzi wakipaliliwa mbinu kuongeza bidhaa thamani  

NA LAWRENCE ONGARO

WATAFITI katika sekta ya kilimo na viwanda walikongamana katika Chuo Kikuu cha Mount Kenya kwa siku mbili, kutanzua masuala ya uhaba wa chakula nchini na kero ya mabadiliko ya tabianchi.

Washikadau wapatao 40 kutoka mashirika tofauti walikusanyika katika chuo hicho, kuonesha bidhaa wanazoongeza thamani hatua hiyo ikitajwa kama njia mojawapo kufanikisha sekta ya viwanda nchini.

Kauli mbiu ya kongamano hilo la Novemba 2023, ilikuwa; Research innovation and Digital Agro Expo.

Aidha, wageni wa heshima katika hafla hiyo walikuwa Mkurugenzi Mkuu Taasisi ya Utafiti na Ukuaji wa Viwanda (KIRDI), Dkt Calvin Onyango, na Mkurugenzi wa Bodi Kutoa Fedha za Vyuo Vikuu, Bw Geoffrey Monari.

Naibu Chansela wa Chuo cha Mount Kenya, Prof Deogratius Jaganyi alisema masomo ya vyuo vikuu ni sharti viambatanishwe na utafiti na ubunifu ili kupata mabadiliko kimaendeleo.

Alidokeza kwamba chuo cha Mount Kenya kimezindua upanzi wa miti aina ya Bamboo, na Aloe Vera kwenye ardhi ya ekari 100, Green Valley Estate Campus, Mjini Thika.

“Lengo kuu ni kuzindua utafiti kutengeneza sabuni kupitia mimea tunayopanda katika eneo hilo,” alisema Prof Jaganyi.

Mhadhiri mkuu huyo alisema katika masomo ya vyuo vikuu, utafiti na bunifu ndiyo nguzo muhimu kuleta maendeleo.

Alitaja benki, wafanyabiashara, wakulima, wahandisi na watu wote katika sekta za chini kibiashara kama asasi muhimu zinazopaswa kujumuishwa katika maendeleo ya nchi.

“Tunaelewa kuwa serikali ina mambo mengi ya kutatua kiuchumi, lakini ni muhimu kuzingatia zaidi masuala ya utafiti na ubunifu kwa kufadhili wanafunzi wengi ili kupata ujuzi kamili,” alifafanua Prof Jaganyi.

Baadhi ya kampuni zilizohudhuria kongamano hilo ni Africa Bio Systems, Farmers Pride, Kozi Maize Mills, Magfre Enterprise Ltd Printing Solution na Family Bank.

Mkurugenzi wa KIRDI, Dkt Onyango alisisitiza haja ya ushirikiano wa karibu kati ya mashirika ya utafiti na taasisi za masomo.

Kuboresha sekta ya kiwanda nchini, afisa huyo aliahidi kwamba KIRDI itakuwa ikishirikiana na vyuo vikuu nchini ili kukuza maarifa ya wanafunzi.

“Tunataka wanafunzi wawe wataalamu kamili baada ya kupitia mafunzo ya utafiti, wawe wabunifu,” alisema Dkt Onyango.

Bw Monari alisema bodi ya kutoa fedha kwa wanafunzi itashirikiana na wafadhili kutoka nchi za ng’ambo, ili kuhami wanafunzi kwa maarifa jinsi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya anga, afya, na kuangazia kero ya uhaba wa chakula na njaa.

  • Tags

You can share this post!

Raila akita kambi Nyanza Kusini kuzima makali ya UDA...

Magavana wataka KNEC kusuluhisha utata wa KCPE 2023

T L