• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Dini inavyokuza maudhui katika riwaya ‘Chozi la Heri’

Dini inavyokuza maudhui katika riwaya ‘Chozi la Heri’

NA JOYCE NEKESA

JUMA hili tutarejelea suala la dini linavyoendeleza maudhui katika riwaya ya ‘Chozi la Heri’ tukirejelea swali lifuatalo:

Binadamu aliumbwa kupambana na ulimwengu na kutumia rasilimali aliyopewa na Mungu kuyaboresha maisha yake… (uk.104)

Eleza muktadha wa dondoo hili.

Ni masimulizi ya Chandachema.

Kwa Umu, Kairu, Zohali na Mwanaheri.

Walikuwa bwenini katika Shule ya Tangamano.

Wanafunzi hawa walikuwa wakimhimiza Umu kwamba aliyopitia kisiwe kikwazo kwake kukosa kusoma na kufanikiwa maishani.

Jadili nafasi ya dini katika kuijenga riwaya hii

Dini hutumika kuwatia watu matumaini. Wao huamini kwamba Mungu atawapa neema kwa kuwa ndiye mwenye nguvu na uwezo. Tulia aliamini kuwa Mungu ndiye hupanga mambo na nguvu na mamlaka hutoka kwake.

Anaamini kwamba siku moja vita vya kijamii vinavyotokana na joto la kisiasa vitafikia mwisho na watu kurudi makwao.

Kaizari na wenzake pia wanaona matumaini baada ya bwana mmoja aliyeonekana kuwa kiongozi wa kidini akizungumzia kuhusu udumishaji wa amani.

Watu wanapokumbwa na hali ngumu za kimaisha wasizoweza kuzitatua humrejelea Mola kwa usaidizi ili aweze kuwakomboa kwa hali hizo. Gari lililowabeba Kaizari na jamii yake pamoja na wakimbizi wengine lilipokwisha petroli, aliwafahamisha abiria wamwombe Mungu aweze kuwapa nafasi ya kuepuka maafa yaliyowakumba. Dereva aliamini kuwa Mungu ndiye mwenye uwezo wa kuwarekebisha wanaotekeleza udhalimu dhidi ya binadamu wenzao.

Wahusika walikimbilia dini walipoona kifo kikiwachungulia. Kaizari alipokaribia kufa kutokana na ukosefu wa chakula kambini, moyo wake unamsuta kwa kumkumbusha kisa cha Biblia kuwahusu Wanawaisraeli walioongozwa na Nabii Musa jangwani. Walimulaumu Musa kwa kuwatoa Misri lakini Mungu aliwapa chakula.

Dini ilitumiwa kutoa misaada kwa waliokumbwa na hali ngumu ya maisha. Dini za Kikristo na Kiislamu zilishirikiana kutoa misaada ya vyakula vilivyogawiwa wakimbizi wa ndani walioishi katika Msitu wa Mamba.
Dini ilitumika kuwahimiza waumini wake kuwa wavumilivu.

Kaizari na wenzake kambini walilinganisha kusubiri misaada na kusubiri kwa kurudi kwa Masiya. Walisubiri kwa muda mrefu kabla ya kuwasili kwa lori lililobeba vyakula vya wahasiriwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Nyimbo za dini humpa mtu maisha ya usalama anapokaribia kukata tamaa maishani.

Mwangeka alipokosa amani kwa sababu ya babake kuwa mbali kikazi, mamake alimwimbia wimbo wa “ni salama moyoni”.

Dini pia huwafanya watu kumshukuru Mungu kutokana na wema anaowatendea maishani mwao. Mwangeka alimshukuru Mungu kwa kumpa nafasi ya kupata mtoto kwa jina Umu kupitia kwa ushirikiano baina ya Apondi na rafikiye, Mwalimu Dhahabu.

Tathmini: Jadili dhima zaidi ya dini riwayani.

  • Tags

You can share this post!

GWIJI WA WIKI: Dkt Alexander Rotich

Polisi wazima mitambo ya Pasta Ezekiel aliyekuwa ameanza...

T L