• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
TALANTA YANGU: Dogo mnyumbuaji viungo aliyekolea

TALANTA YANGU: Dogo mnyumbuaji viungo aliyekolea

Na WYCLIFFE NYABERI

LENAH Kebaya, 9, ni mwanafunzi wa Gredi ya Tatu katika shule ya msingi ya Manga Highway Complex, kaunti ya Nyamira.

Katika umri wake mdogo, Lenah ni mwanasarakasi anayenyumbua viungo vya mwili wake na kujipinda kuunda maumbo mbali mbali.

Kila asubuhi, utamkuta Lenah akifanya mazoezi katika kiwanja cha shule yao kabla ya kujiunga na wenzake darasani kwa masomo ya kawaida.

Amekuwa akifanya hivi tangu atambue ana kipaji na ndoto yake ni kuwa mwanabondia wa mchezo wa karate atakapokuwa mtu mzima.

Hana mkufunzi wa kumnoa na kwa hivyo mamake anayejulikana kama Bi Rose Kwamboka, ndiye anayetekeleza jukumu hilo la ukocha kwa kumsaidia kufanikisha mazoezi yake.

Mamake ni mfanyabiashara na hana ujuzi wowote katika fani ya ubondia wa karate.

Kulingana na Bi Kwamboka, aligundua mwanawe ana kipaji maalum alipokuwa na umri wa miaka mitatu.

“Nilishangazwa alipojikunja siku moja na kuwa kama kinyago. Ilikuwa asubuhi na tangu siku hiyo amekuwa akiendelea hivyo. Hali hiyo ilinisukuma kusaka ushauri kutoka kwa marafiki na jamaa zangu kuhusu kilichokuwa kikijiri,” Bi Kwamboka anasema.

Bi Kwamboka anaongeza kuwa aliamua kumsaidia mwanawe kufikia viwango vyake vya ubora alipogundua kuwa ilikuwa talanta kweli.

Kunapotokea sherehe za kutoa tuzo katika shule jirani, Lenah huitwa ili kuwatumbuiza wageni waalikwa ambao husisimka na kufurahia sarakasi zake.

“Ikiwa nitapata kocha mzuri wa kunielekeza vilivyo, nitafanya mazoezi hadi niwe mwanakarate wa kulipwa. Ninaazimia kuyashinda mataji makubwa makubwa katika mchezo huo,” Lenah anasema.

Jambo ambalo hatalisahau mwanafunzi huyo ni pale alipopata fursa ya kuwatumbuiza wageni kwenye jukwaa kuu la uwanja wa michezo wa Gusii, katika sherehe za mashirika ya vyombo vya habari na mawasiliano zinazojulikana kama (KECOSO) miaka michache iliyopita.

Lenah Kebaya, 9, mwanafunzi wa Gredi ya Tatu katika shule ya msingi ya Manga Highway Complex iliyoko katika Kaunti ya Nyamira, afanya mazoezi. PICHA | WYCLIFFE NYABERI

Waziri wa Michezo Bi Amina Mohammed, alikuwa mmoja wa waliotumbuizwa na Lenah na waziri huyo aliahidi kumsaidia mwanafunzi huyo kufanikisha ndoto yake.

“Nafurahia kukutana na Lenah ambaye ni mwanasarakasi anayeibuka. Kama serikali tutafanya hima kukuza vipaji,” waziri Amina akasema.

Kinachompa hofu Lenah, ni kukosekana kwa akademia zinazotoa mafunzo ya mazoezi ya mwili. Anaipa serikali changamoto ya kuunda vituo vya kukuza talanta mashinani.

You can share this post!

WANTO WARUI: Walimu wana kibarua kuandaa watahiniwa kwa...

PAUKWA: Titi anyemelewa na arobaini zake

T L