• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:16 PM
KAULI YA PROF IRIBE: Kiswahili kingetaja maazimio haya 2022 lau kingepewa fursa

KAULI YA PROF IRIBE: Kiswahili kingetaja maazimio haya 2022 lau kingepewa fursa

Na PROF IRIBE MWANGI

MWAKA wa 2021 ambao umekuwa na panda shuka nyingi hasa kutokana na Uviko-19 umefika ukingoni.

Jumamosi itakuwa tarehe 1–1-2022. Wengi wana maazimio ya mwaka mpya. Wengi wanaomba salama na mafanikio mwaka 2022. Baada ya kusoma mawazo yao, nimejiuliza, kama Kiswahili kingezungumza kingetaja maazimio yapi? Yalionijia akilini ni mengi.

Nafikiri Kiswahili kingeazimia kubuniwa Baraza la Taifa. Baraza hili lingekisaidia sana katika kusanifishwa, kukua na kuenea. Kingekuwa chombo ambacho kingerejelewa katika kukuza ustadi wa Kiswahili. Nafikiri Kiswahili kingetaja pia ruwaza ya kuwakilishwa ifaavyo katika asasi zote za elimu tangu shule za msingi hadi kwenye vyuo vikuu. Hivyo, kingeishia kuwa rafiki ya wengi na wala sio adui asiyeeleweka. Kingeazimia sana kuwa katika ngazi zote za mafunzo ya CBC hata katika Gredi za 10, 11 na 12. Kingetamani kifunzwe vyuoni kwa madaktari, wahandisi, maafisa wa kilimo na wengine wengi, kwani si wote hawa huwasiliana na wateja wao kwa kukitumia?

Japo katika maazimio yake Kiswahili kingeisifia Bunge kwa bidii yake katika kuweka mikakati kuona kuwa kinatumika bungeni, lakini kingeazimia kupata matumizi zaidi ili kuwa sambamba na Kiingereza. Kingetaka Bunge kuweka sheria kuhakikisha kuwa kinatumiwa katika afisi za serikali, kwenye shughuli rasmi na kwenye mikutano yote ya kitaifa na kimataifa.

Kiswahili kingetaka wahubiri waache kutumia lugha za kigeni na kisha kutafsiri kwa kukitumia, watumie Kiswahili tu.

Kingetaka kuwe na magazeti zaidi yaliyoandikwa kwake. Kingetaka kitumiwe kwa namna sanifu katika vyombo vya habari. Naamini kingetaka kuwe na waandishi na wachapishaji zaidi wa Kiswahili.

You can share this post!

Ploti ya Onyesho la Kwanza tendo la tatu katika tamthilia...

TAHARIRI: Sokomoko bungeni ni dalili hatari uchaguzini

T L