• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mshairi anayeishi na ulemavu wa ngozi ajizolea sifa ndani na nje ya Lamu

Mshairi anayeishi na ulemavu wa ngozi ajizolea sifa ndani na nje ya Lamu

NA KALUME KAZUNGU

ALIDINDA kabisa kusalia ndani ya nyumba sawa na walemavu wengi ambao mara nyingi huishia kufichwa chumbani kutokana na dhana potovu ya baadhi ya jamii zinazowakandamiza na kuwazuia walemavu hao wasionekane, wakiamini kufanya hivyo ni kuzuia kicheko au aibu.

Kutana na Bw Khalid Omar Ali almaarufu ‘Kanjenje’ ambaye ni mlemavu wa ngozi.

Licha ya ulemavu wake, Bw Kanjenje,51, amejizatiti na kuibuka kuwa malenga bora ndani na nje ya kisiwa cha Lamu.

Mashairi yake mengi anayotunga na kughani huhusisha maudhui mbalimbali yanayogusa akina baba, wazee, akina mama, vijana na hata watoto.

Miongoni mwa masuala anayoyapa kipaumbele kwenye tungo zake ni mazingira, siasa, dawa za kulevya, pombe haramu, itikadi kali, ndoa na mimba za mapema, elimu, amani, umoja, na uzalendo.

Upekee wa malenga huyu ambao unamtofautisha na washairi wengine ni jinsi alivyo mwepesi katika utunzi wake.

Huku wengi kwa kawaida wakitegemea kughani mashairi majukwaani huku mikononi wameshikilia karatasi za kusoma wanayokariri, Bw Kanjenje yeye hufanya yote bila kudurusu popote.

Hali hiyo imemfanya mshairi huyo kupendwa na wengi, ikiwemo viongozi mbalimbali serikalini na kijamii.

Gavana wa Lamu Issa Timamy (kulia) akiwa na Bw Khalid Omar Ali Kanjenje (kati), mshairi tajika wa Lamu mwenye umri wa miaka 51 ambaye licha ya ulemavu wa ngozi, yeye anasifika nje na ndani ya Lamu kwa umahiri wake katika kutunga na kughani mashairi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Kisiwani Lamu, Bw Kanjenje ni kipenzi cha wanasiasa wote, hasa Gavana wa Lamu Issa Abdallah Timamy kutokana na weledi wake katika kutunga na kughani mashairi.

“Nashukuru Mola kwa kunipa kipaji hiki cha umalenga. Mimi huwa nakariri mashairi yangu bila kuangalia popote. Cha msingi ni mwenye hafla kunieleza shughuli yake inahusu nini, majina ya wahusika, maudhui ya hafla basi. Nikifika jukwaani najua cha kufanya katika mashairi yangu. Sijafeli popote. Wengi hubambika na mimi,” akasema Bw Kanjenje.

Taifa Jumapili ilipomuuliza kuhusu siri ya ubabe wake katika ushairi, Bw Kanjenje alisema ametoka mbali kiasi kwamba yale aliyopitia maishani kupitia tasnia ya umalenga yamempa uzoefu si haba.

Gavana wa Lamu Issa Timamy akiwa na Bw Khalid Omar Ali Kanjenje, mshairi tajika wa Lamu mwenye umri wa miaka 51 ambaye licha ya ulemavu wa ngozi, yeye anasifika nje na ndani ya Lamu kwa umahiri wake katika kutunga na kughani mashairi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alianza kupenda ushairi akiwa Darasa la Sita katika Shule ya Msingi ya Matondoni, Lamu Magharibi.

Anasema kichocheo kikuu ni babu yake, Bw Mohamed Baishe ambaye alikuwa mtunzi sufufu wa mashairi wakati huo.

“Babu yangu ndiye aliyenisukuma kupenda kutunga na kughani mashairi. Alikuwa mtunzi mahiri wa mashairi kijijini kwetu Matondoni. Hakuwa anaimba ila alitafutwa na wa mbali na karibu kuwatungia mashairi na waliridhishwa na kazi yake. Babu yangu ndiye aliyenifunza ushairi katika udogo wangu, hivyo kunifanya kujitosa kwenye usanii huu mzimamzima hadi leo. Napenda kutunga na kughani mashairi,” akasema Bw Kanjenje.

Pia hawezi kusahau jitihada za mwalimu wake wa Kiswahili, Bw Ali Omar, ambaye anasema alimsaidia pakubwa kupalilia kipaji chake cha ushairi, hivyo kuibuka malenga bora ndani na nje ya Lamu.

“Mwalimu wangu alikuwa akinipa nafasi kutumbuiza wakati wa hafla za elimu shuleni, mikutano ya wazazi na sherehe nyingine. Yeye ndiye aliyenifanya kuwa jasiri zaidi, hasa wa kusimama majukwaani nikighani mashairi wakati wa enzi za udogo wangu. Kwa sasa niko na uzoefu na sitetemeki ninaposimama kwenye jukwaa lolote lile, hata kuwe na viongozi wakuu au umati mkubwa namna gani. Nimezoea,” akasema Bw Kanjenje.

Ushairi umemsaidia pakubwa, ikiwemo kumwezesha kushiriki majukwaa pamoja na watu wa tabaka mbalimbali.

Yeye ashawahi kumtumbuiza Rais Mstaafu, Uhuru Kenyatta, kiongozi wa upinzani, Raila Odinga na wanasiasa wengine tajika nchini.

Ni kupitia ushairi ambapo yeye hujikimu kimaisha kwani hana kazi nyingine mbadala ya kumpatia kipato.

Miongoni mwa mashairi ambayo Bw Kanjenje ametunga na kusifika nayo ni: ‘Tutunze Mazingira’, ‘Wa Lamu Tupendane’, ‘Kenya Nchi Yetu’, ‘Tudumisheni Umoja’, ‘Tuondoe Ukabila’, ‘Ulemavu Si Kilema’, ‘Jamii Tuwapende’, ‘Kuwaenzi na Kuwaendeleza Walemavu’, ‘Mihadarati Si Chakula’, na ‘Elimu ni Ufunguo’. Yapo mengi.

Mbali na kujipatia mtaji, ushairi pia umemwezesha Bw Kanjenje kuzuru sehemu mbalimbali za Lamu, Pwani na nchini kwa ujumla.

“Nimetembea visiwa vyote vya Lamu na kila kona ya eneo hili kupitia ushairi. Magavana wetu wote sita wa Pwani nimewahi kushiriki nao jukwaa moja kupitia ushgairi, hasa mwaka 2014 wakati nikitumbuiza hafla ya magavana wa Pwani eneo la Fort Jesus mjini Mombasa. Pia nimefika Nairobi na Kisumu kupitia ushairi wangu,” akasema Bw Kanjenje.

Anaisifu jamii ya Lamu kwa jinsi ilivyomshika mkono katika kukipalilia na kukiendeleza kipaji chake cha ushairi licha ya kuwa mlemavu wa ngozi.

“Kwanza nilifikiria kuwa ulemavu wangu wa ngozi ungefanya jamii kunibagua na kutoamini nilichokifanya. Nashukuru kwa kunikumbatia. Sijashuhudia unyanyapaa wa aina yoyote dhidi yangu. Kila ninapoenda mashabiki wangu hunipokea vyema,” akasema Bw Kanjenje.

Wosia wake kwa jamii ni kwamba wasiwabague au kuwaficha walemavu, akisisitiza kuwa kila mlemavu yuko na talanta yake sawa na watu wengine wowote wale.

“Walemavu wanaweza. Wazazi wangu wangenificha singefika nilipo. Watu lazima wajue kuwa ulemavu si kilema. Ayawezayo alie mkamilifu wa viungo pia sisi wapungufu wa viungo tunayaweza kivingine. Haina haja ya unyanyapaa dhidi ya wapungufu wa viungo vya mwili,” akasema Bw Kanjenje.

Aidha anaiomba serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuwazingatia sana wasanii wa mashairi, akisema wamesahaulika.

“Mahali kama hapa Lamu sisi washairi hatuna promota yeyote. Itakuwa bora serikali kuizingatia sana hii tasnia ya umalenga. Tumeachwa nyuma au kusahaulika kabisa na hiyo ni changamoto kubwa kwetu kujiendeleza maishani,” akasema Bw Kanjenje.

Bw Kanjenje alizaliwa mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu mwaka 1972.

Bw Khalid Omar Ali Kanjenje, mshairi tajika wa Lamu mwenye umri wa miaka 51. Licha ya ulemavu wa ngozi, yeye anasifika nje na ndani ya Lamu kwa umahiri wake katika kutunga na kughani mashairi. PICHA | KALUME KAZUNGU

Alilelewa kijijini Matondoni.

Ni wa pili katika familia ya watoto 11.

Alisomea Shule ya Msingi ya Matondoni kisiwani Lamu kati ya 1981 na 1988.

Hakuweza kuendeleza masomo yake ya sekondari kutokana na umaskini katika familia.

Yeye ni baba wa mtoto mmoja.

  • Tags

You can share this post!

Ex wa Diamond Hamisa Mobetto kufanya kazi na hasimu wa...

Mama wa Taifa Rachel Ruto alisha watahiniwa wa KCPE

T L