• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 12:48 PM
TALANTA YANGU: Dogo mkali wa mitindo

TALANTA YANGU: Dogo mkali wa mitindo

NA RICHARD MAOSI

FANI ya uanamitindo miongoni mwa jinsia ya kiume inaendelea kupata umaarufu katika safu ya kimataifa, na itaendelea kufanya vyema endapo washiriki wengi watajitokeza.

Ni dhahiri kuwa yeyote ambaye analenga kushiriki katika jukwaa hili ni lazima awe mkakamavu, atumie lishe bora na kufanya mazoezi mara kwa mara.

Hata hivyo kwa kijana Clarence Maina mwanafunzi wa umri wa miaka 10 kutoka shule ya msingi ya Lions jijini Nakuru, hii ni fani ambayo imemsaidia kupata ujasiri hasa anaposimama mbele ya hadhira.

Anasema ni jukwaa ambalo alianza kushiriki akiwa mwanafunzi wa chekechea, baada ya wazazi wake kumpa hamasa na mori, wakimhimiza aendelee kushiriki, ikiwa ni baada ya kuonyesha kwamba alikuwa na kipaji cha miondoko.

Kabla ya kufikia kiwango cha kitaifa alikuwa ameshiriki katika kiwango cha mchujo na kuwabwaga jumla ya wahusika 18, wengi wao kutoka kaunti ya Nakuru.

Anasema kuwa jambo hili lilimpa msukumo akaamini hakuna kisichowezekana chini ya jua, ndiposa akaelekeza juhudi zake zote katika ulimwengu wa miondoko ya urembo na utanashati.

Mnamo Machi 2022, Maina ameteuliwa kuwa miongoni mwa wanamitindo chipukizi kutoka nchini Kenya ambao watawakilisha taifa kwenye mashindano ya Little Junior Idol nchini Thailand.

Maina anaungama kuwa hili ni shindano la taadhima kwani litampa jukwaa la kutangamana na wanamitindo wengine wengi na tena mahiri kutoka ulimwenguni.

Mwalimu wake Bi Esther Muriithi , kwa upande mwingine anasema ni hafla ambayo itamuunganisha Clarence na ulimwengu wa fani ya uanamitindo .

“Licha ya changamoto nyingi ambazo Maina pamoja na wenzake walipata msimu wa likizo ndefu 2020 wakati ambapo visa vya covid -19 vilikuwa vingi, hakukata tamaa licha ya kuwa haikuwa rahisi kupata muda wa kufanya mazoezi, ” akasema.

You can share this post!

Samia atema washirika wa Magufuli

PAUKWA: Getore afumaniwa akichoma makaa

T L