• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 3:31 PM
Maafisa tisa Kuppet wamezea mate siasa

Maafisa tisa Kuppet wamezea mate siasa

Na FAITH NYAMAI

UONGOZI wa vyama vya kutetea maslahi ya walimu nchini utaathirika baada ya maafisa kuonyesha nia ya kuwania nyadhifa za kisiasa katika uchaguzi mkuu ujao.

Kufikia sasa, sita kati ya maafisa tisa wa kitaifa wa chama cha kutetea maslahi ya walimu wa shule za upili na vyuo (Kuppet) wametangaza azma za kuwania viti mbalimbali katika uchaguzi huo 2022.

Aidha, maafisa watatu wa chama hicho ambao ni wabunge watatetea nyadhifa zao hali wenzao watatu wasioshikilia nyadhifa za kisiasa wakiwa wamemejitoza katika kivumbi cha mwaka ujao. Maafisa wengine wengi wa matawi ya Kuppet pia wanataka kuwania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi huo wa Agosti 9, 2021.

Katibu Mkuu wa Kuppet, Akelo Misori ametangaza azma ya kuwania wadhifa wa ugavana katika Kaunti ya Homa Bay. Katibu wa kitaifa anayewakilisha shule za upili Edward Obwocha anawania ubunge wa Kitutu Masaba katika Kaunti ya Nyamira.

Naye Naibu Mwenyekiti wa Kitaifa wa Kuppet, Julius Korir anawania kiti cha ubunge wa Soi, Uasin Gishu huku Katibu wa Kitaifa anayewakilisha vyuo Sammy Chelang’a akiwania ubunge wa Baringo Kaskazini.

Bw Misori atakuwa akiwania kwa mara ya kwanza ilhali Mbw Obwocha na Korir wanajaribu kwa mara ya pili baada ya kubwagwa katika uchaguzi mkuu wa 2017.Duru ziliambia Taifa Leo kuwa baadhi ya maafisa wa kitaifa wa chama cha kitaifa cha walimu (Knut) pia wanawazia kuwania nyadhifa katika uchaguzi mkuu ujao ila hawajatangaza waziwazi.

You can share this post!

Ujasiri wa kipekee wa Mudavadi kura ya 2022 ikikaribia

Kesi dhidi ya Ruto kuhusu unyakuzi wa nyumba kuendelea

T L