• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:07 PM
MAKALA MAALUM: Kimojawapo cha vivutio 2023 ni ulainishaji wa CBC

MAKALA MAALUM: Kimojawapo cha vivutio 2023 ni ulainishaji wa CBC

MWAKA Mpya wa 2023 utakuwa wa kuendeleza mabadiliko makubwa yaliyoshuhudiwa katika sekta ya elimu mwaka 2022.

Ijapokuwa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu hajahudumu kwa muda mrefu, Rais William Ruto aliahidi kutekeleza mageuzi makubwa katika sekta hiyo, hasa ulainishaji wa Mfumo Mpya wa Elimu ya Umilisi na Utendaji (CBC).

Hilo ni kufuatia malalamishi kutoka kwa wazazi na wadau wengine kuhusu gharama ya kuuendesha mfumo huo.Mnamo Septemba, Rais Ruto alibuni jopo maalum la watu 42 kutathmini mapengo na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo huo.

Jopo hilo linaongozwa na Profesa Raphael Munavu.

Wanachama wengine ni maprofesa Kiama Gitahi na Paul Wainaina, ambao ni manaibu chansela wa vyuo vikuu vya Nairobi na Kenyatta mtawalia.

Kando na kutathmini CBC, jopo hilo pia litaangalia na kupendekeza mikakati itakayohakikisha kila mtu anapata elimu, hasa wale walio katika maeneo kame, watoto na walemavu.

Jopo pia litaangalia hali ilivyo katika taasisi za elimu ya juu kwa kutathmini na kupendekeza mfumo utakaofuatwa katika ufadhili wa utoaji mafunzo katika Taasisi za Mafunzo ya Kiufundi (TVETs), elimu katika vyuo vikuu na utafiti.

“Jukumu kuu la jopo litakuwa kutathmini na kupendekeza sheria itakayotoa mwongozo wa kuunganishwa kwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HELB), TVETs na Bodi za Kufadhili Vyuo Vikuu (UFB),” ikaeleza taarifa kutoka Ikulu.

Kufuatia uteuzi wao, jopo linahitajika kutoa ripoti kuhusu hatua ilizofikia baada ya kila miezi miwili na mwisho wa muda wa kuhudumu.

Ijapokuwa jopo hilo limepangiwa kutoa ripoti yake rasmi Machi, tayari imetoa mapandekezo kadhaa ambayo lingependa yazingatiwe katika mageuzi na ulainishani wa mfumo wa elimu nchini.

Baadhi ya mapendekezo liliyotoa katika ripoti yake ya muda ni mtihani wa Gredi ya Sita kutotumiwa kubaini ikiwa mwanafuzi anafaa kuruhusiwa kujiunga na Shule ya Upili ya Kiwango cha Chini au la.

Kulingana na jopo hilo, tofauti na mitihani ya kitaifa ya Darasa la Nane (KCPE) au Kidato cha Nne (KCSE) ambayo hutumiwa kuamua ikiwa mwanafunzi atajiunga na shule ya upili au vyuo vikuu mtawalia, mitihani hiyo inafaa kutumia kubaini uwezo wa kimasomo wa mwanafunzi husika.

“Ripoti kuhusu matokeo ya mwanafunzi inafaa kutumika kuboresha uwezo wake na walimu,” likaeleza jopo.

Jopo pia lilipendekeza kuwa madarasa ya Saba, Nane na Tisa yatakuwa katika shule ya msingi, badala ya shule ya upili kama ilivyodhaniwa hapo awali.

Pendekezo hilo lilikuwa afueni kubwa kwa wazazi, kwani wengi walikuwa katika hali ya kuchanganyikiwa kuhusu ikiwa wanao wangeendeleza masomo yao katika shule za msingi au wangejiunga na shule za upili baada ya kuukamilisha mtihani wa Gredi ya Sita au la.

Jopo hilo pia lilipendekeza serikali inafaa kujenga madarasa na maabara zaidi katika shule zitakazokuwa na madarasa hayo—Gredi 7, 8 na 9.

“Kwa wakati huu, shule za msingi zinafaa kutumia maabara yaliyo katika shule za upili zilizo karibu,” likaeleza jopo.

Prof Munavu alisema wataendelea na shughuli za kuwashirikisha zaidi wadau wote ili kuhakikisha kuwa mapendekezo ya mwisho watakayotoa yataakisi sauti na maoni ya wadau wote wa elimu, wakiwemo Wakenya.

“Kile tunafaa kubaini ni kuwa mapendekezo ya mwisho tutakayotoa yataashiria sauti za kila mmoja. Hatutaki kutoa mapendekezo ambayo yatazua malalamishi na lawama baadaye,” akasema.

Jopo hilo limepewa hadi Machi mwaka huu kuwasilisha ripoti yake ya mwisho.

Mabadiliko mengine yaliyoshuhudiwa mwaka 2022 ni kuondoka kwa Profesa Magoha.

Kwa miaka mitatu aliyohudumu kama Waziri wa Elimu, Prof Magoha alisifika kwa kutofanyia kazi afisini.

Kila mara, alikuwa nyanjani akifuatilia jinsi hali ilivyo katika shule tofauti.Msukumo wake mkuu, hata hivyo, ulikuwa jinsi shule za msingi zilikuwa zikitekeleza mfumo wa elimu wa CBC.

Licha ya malalamishi yaliyokuwa yakitolewa na wazazi, hasa kuhusu gharama yake, Prof Magoha alishikilia kuwa serikali haingelegeza kamba katika utekelezaji wake.

Licha ya juhudi zake, wizara hiyo ilikumbwa na madai ya ufisadi miongoni mwa maafisa wake wakuu mnamo 2020, waziri akishikilia kuwa ndiye “aliyefichua maovu hayo.”

Kulingana naye, uporaji huo ulikuwa ukitekelezwa kupitia kuongezwa kwa gharama ya kujenga madarasa.

“Kiwastani, kila darasa linagharimu Sh788,000. Hata hivyo, lazima tuanze kujiuliza kule Sh426,000 zaidi zinakoelekea. Madarasa mengi yalijengwa kwa gharama ya Sh1.26 milioni,” akasema waziri.

Mnamo Novemba 14, 2020, Prof Magoha alitoa malalamishi kama hayo kuhusu ununuzi wa madawati ya shule.

Alitoa mfano wa sekta ya shule za msingi, ambapo baadhi ya walimu wakuu walikuwa wameongeza idadi ya wanafunzi kutoka 8.47 milioni hadi milioni tisa ili kuongezewa fedha za kujengea madawati.

Tukio jingine lililoshuhudiwa katika sekta hiyo ni kuongezeka kwa madeni yanayodaiwa vyuo vikuu vya umma.Kulingana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Bajeti, vyuo hivyo vina madeni ya zaidi ya Sh50 bilioni.

Ni hali iliyovifanya baadhi ya vyuo kama vile Moi, Egerton, Kisii, Kenyatta, Naorobi kati ya vingine kuwafuta baadhi ya wafanyakazi wake ili kupunguza gharama ya matumizi ya fedha.

Kwa wakati mmoja, Chuo Kikuu cha Moi kilifungwa kutokana na matatizo ya kifedha.Suala jingine kuu lililoshuhudiwa katika sekta hiyo na linalotarajiwa kuanza kutekelezwa mwezi huu Januari ni ahadi ya serikali kuwaajiri zaidi ya walimu 30,000.

Wadadisi wanasema suala kuu kwa sasa ni kungoja kuona ikiwa serikali itatimiza ahadi hiyo.

  • Tags

You can share this post!

BORESHA AFYA: Mlo wako iwapo unanyonyesha

PSG wapoteza mechi kwa mara ya kwanza tangu Machi 2022

T L