• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
MAKALA MAALUM: Majitaka, uchafuzi wa Ziwa Nakuru unavyoangamiza ndege wa Flamingo

MAKALA MAALUM: Majitaka, uchafuzi wa Ziwa Nakuru unavyoangamiza ndege wa Flamingo

Na ERIC MATARA

UVUNDO mkali wa kukera pua unachomoza kutoka kiwanda cha majitaka cha Nakuru Njoro Sewage Treatment Pond, mkabala na Ziwa Nakuru kunakopatikana mbuga maarufu ulimwenguni ya Lake Nakuru.

Ukitazama kutoka mbali utaona maelfu ya Flamingo wametamba kwenye ufuo wa ziwa hilo.

Haya ndiyo makao yao. Hapa ndipo nyumbani kwao wanakopata lishe.

Lakini unapokaribia ziwani mambo yanaanza kubadilika na taswira halisi kujitokeza.

Mamia ya ndege hawa, wenye rangi ya waridi, wamelala kwenye tope wamekufa.

Ziwa Nakuru, linalotambuliwa na shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kama kivutio cha watalii wa nyumbani na kimataifa, limegeuka kuwa mauti kwa ndege wake.

Ziwa hili linasakamwa na uchafuzi na sasa limekuwa sumu kwa wanyama hao.

Unapozuru eneo husika unakumbana na ndege waliokufa wakiwa wamelala kwenye fuo huku wengine wengi wamezikwa kwenye tope.

Wameuawa na maradhi ambayo wanasayansi wanaamini yanasababishwa na uchafuzi kutoka viwandani; uchafuzi ambao umefikia kiwango cha kutisha.

Bw Edward Karanja ni mlinzi wa ngazi za juu katika Shirika la Wanyamapori Kenya (KWS) anayehudumu katika ziwa hilo.

Katika mahojiano na Taifa Leo, alisema kwamba yeye na wataalamu wengine wameanza kufanya uchunguzi kubaini kinachoua flamingo hao.

“Maeneo kadhaa ziwani tumeshuhudia vifo, ikiwemo katika eneo la kiwanda cha kusafisha majitaka. Tumezungumza na kampuni ya maji ya Nakuru Water and Sanitation Services kuhusu suala hilo,” alisema Bw Karanja.

Uchunguzi wao utajumuisha kufanyia ndege hao upasuaji ili kubaini sumu katika mizoga yao.

Mwanamazingira Jackson Kinyanjui, ambaye ni mwanzilishi wa shirika la Climate Change Kenya, alisema kuwa vifo vya ndege hao ni kitendawili lakini “tunashuku ni uchafuzi kutoka kiwanda kilicho karibu cha majitaka.”

Bw Kinyanjui, mtafiti ambaye kwa mwaka mmoja amekuwa akichunguza ongezeko la viwango vya maji katika Bonde la Ufa, alisema mchanganyiko wa majitaka yenye sumu kutoka kwa kiwanda hicho na vingine katika mji pana wa Nakuru huelekezwa ziwani kila siku.

“Kuna uwezekano wanyama pori wanakula chakula na kunywa maji yenye sumu. Ziwa Nakuru lilikuwa maarufu kwa sababu ya urembo wa Flamingo waliopatikana humo kwa wingi, lakini iwapo uchafuzi huu hautasitishwa basi kuna hatari kubwa ya kupoteza rasimali hii muhimu na kivutio cha kimataifa. Serikali ya kaunti na ya kitaifa zinafaa kushirikiana kukomesha uchafuzi wa ziwa hili,” alisema mwanamazingira mwingine Bw James Wakibia.

Kinachosikitisha ni kwamba kiwanda cha majitaka cha Mwariki kinaelekeza maji yake katika ziwa hilo.

Majitaka hayo yanakusanywa kutoka sehemu mbalimbali za Nakuru.

Hali ni mbaya kiasi kwamba majuzi kiwanda kilizama maji ya ziwa hilo kufuatia tukio la maziwa ya Bonde la Ufa kuvunja kingo zao kufuatia ongezeko la viwango vya maji.

Hii inamaanisha kuwa majitaka yamechanganyika na maji ya ziwa hilo.

Mwanaharakati Julius Muli anasema uchafuzi huo unadhihirishwa wazi na uvundo mkali pamoja na sura chafu ya maji ziwani.

Utafiti wa awali ambao ulichunguza kiwango cha uchafuzi ulionyesha kwamba kulikuwa na sumu ya kuua wadudu katika ziwa hilo.

Maji, samaki na mimea ya majini iliyotolewa ziwani na mito inayoelekeza maji humo, zilipatikana kuwa na sumu ya chuma na ile inayotokana na kemikali za kuua wadudu.

Utafiti huo uligundua kwamba sumu iliingia kwa wingi ziwani wakati wa mvua, kumaanisha kwamba maji ya mvua yalikuwa yakiteremsha sumu hadi ndani ya ziwa.

Kiwango cha sumu kiliendelea kuongeka muda ulivyosonga, na kuzama kwa kiwanda cha majitaka kumeharibu mambo hata zaidi.

Afisa Mkuu wa Mazingira wa Kaunti ya Nakuru, Bw Kiogora Muriithi, aliambia Taifa Leo kwenye mahojiano ya awali kwamba kuna haja ya kuhakikisha majitaka pamoja na uchafu wa viwandani zinatupwa kwa njia salama na sawa ili kuhakikisha ni maji yaliyotiwa dawa kuondoa uchafu, ndiyo pekee yanaingia ziwani.

“Ni lazima tufanye hivi, tuendesha kampeni kabambe ya hamasisho kuhusu manufaa ya ziwa hili na kutekeleza sheria zilizopo ili kurekebisha hali. Usafishaji wa kila mara pia utaokoa ziwa hili lililo fahari ya Nakuru,” Bw Kiogora akaeleza.

Kuongezeka kwa viwango vya maji katika maziwa ya Rift Valley; yakiwemo Nakuru, Baringo, Bogoria, Naivasha na Elementatita, yamefanya haki kuwa mbaya zaidi kwa flamingo.

Maji hayo yameharibu maeneo ya lishe kwa ndege hao.

Ziwa Nakuru hupokea maji kutoka kwa mito mitano – Njoro, Makalia, Nderit, Naishi na Larmudiak, ambayo huanzia mharara wa Mau.

Miongo miwili na nusu iliyopita, Flamingo wasiopungua milioni mbili – sawa na thuluthi moja ya ndege hao kote ulimwenguni – walikuwa wakikusanyika katika ziwa hilo kula mimea iliyotiwa rotuba na kinyesi chao.

Hata hivyo, uchafuzi na kuongezeka kwa viwango vya maji kumefanya idadi yao ipungue na baadhi wamehamia kwingineko, kama vile maziwa ya Bogoria, Elementeita, Magadi na Natron nchini Tanzania.

Hii imefanya Flamingo waliobakia Ziwa Nakuru kuwa chini ya 500,000; ikilinganishwa na kati ya milioni mbili na milioni nne waliokuwa wakipamba rasilimali hiyo asili miaka michache iliyopita.

Ziwa hilo ni makao ya mbunga ya kitaifa ya Lake Nakuru National Park, ambako kunapatikana aina tofauti za wanyama pori wakiwemo wanaokabiliwa na hatari ya kutoweka.

Mzoga wa ndege aina ya flamingo aliyeangamia kutokana na uchafuzi wa Ziwa Nakuru unaosababishwa na maji machafu kutoka kwa kiwanda cha majitaka mjini Nakuru. Picha/ Cheboite Kigen

Utafiti uliofanywa na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Moi kati ya 2010 na 2014 ulifichua kwamba, kulikuwa na aina 450 za ndege katika ziwa hilo.

Ziwa hilo pia liliorodheshwa kuwa moja ya maeneo maridadi ya kitalii na tovuti ya safari za ndege ya Conde Nast Traveller.

Mnamo Machi 2019, Waziri wa Utalii Najib Balala aliambia mkutano wa wadau mjini Naivasha kwamba Ziwa Nakuru lilikuwa linadidimia kwa umaarufu kutokana na uhamaji wa flamingo.

Alipendekeza kubuniwe kamati maalum kushughulikia uvamizi katika maziwa ya Nakuru, Naivasha na Elementaita, na kuhimiza wanasayansi wa KWS kuchukua hatua za kulinda flamingo.

You can share this post!

Jinsi tulivyopigana na simba hayawani, nusra atumalize

Wakenya waomboleza rais wa mchezo wa kuogelea Kenya (KSF)...