• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Matokeo ya vipimo vya corona ya Mohamed Salah na timu ya Misri itakayochuana na Harambee Stars haya hapa

Matokeo ya vipimo vya corona ya Mohamed Salah na timu ya Misri itakayochuana na Harambee Stars haya hapa

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI matata wa Liverpool, Mohamed Salah na timu nzima ya Misri iko sawa tayari kwa mechi dhidi ya Kenya ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) hapo Machi 25.

Mafirauni hao waliwasili jijini Nairobi mnamo Machi 24 jioni wakitokea jijini Cairo na kupimwa virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka Misri (EFA), “matokeo ya vipimo hivyo yameonyesha kuwa msafara wote wa Misri hauna virusi hivyo”.

Itakumbukwa kuwa Salah, ambaye anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu Uingereza msimu huu, alikosa michuano miwili iliyopita ya Kundi G dhidi ya Togo baada ya kugunduliwa na virusi hivyo. Yeye ni mmoja wa wachezaji ambao Harambee Stars ya kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee italazimika kukaba ikilenga kuvuan ushindi na kufufua matumaini yake finyu ya kufuzu.

EFA pia imesema kuwa beki Ahmed Hegazy aliungana na timu hiyo akitokea Jeddah nchini Saudi Arabia na kukamilisha kikosi cha wachezaji wake 28.

Misri ya kocha Hossam El Badry inahitaji alama moja tu kutoka michuano yake miwili iliyosalia dhidi ya Kenya na Comoros ili ijikatie tiketi ya kuelekea Cameroon kwa dimba la AFCON.

Inaongoza kwa alama nane, sawa na nambari mbili Comoros nayo Kenya iko alama tano nyuma. Togo inavuta mkia kwa alama moja iliyopata katika sare ya 1-1 dhidi ya Kenya mnamo Novemba 2020. Misri imeratibiwa kufanya mazoezi Jumatano alasiri ugani Kasarani ambao utatumiwa kwa mechi ya hapo Alhamisi usiku.

You can share this post!

MAKALA MAALUM: Mzee Abae ajivunia tajriba ya kutibu nyoka...

AC Milan wavunja benki ili kumsajili beki Fikayo Tomori...