• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Makali ya njaa Mathare yanavyosukuma mabinti wachanga kwenye vitanda vya majambazi

Makali ya njaa Mathare yanavyosukuma mabinti wachanga kwenye vitanda vya majambazi

NA FRIDAH OKACHI

Ugumu wa maisha katika mtaa wa Baba Dogo umesukuma wasichana matineja kujipata katika vitanda vya  magenge ya wezi ambao huwalazimisha kufanya nao mapenzi kwa ajili ya kuwapa chakula na mahala pa kuishi.

Msoo ni mama wa watoto wawili pacha. Alipata ujauzito baada ya kujiunga na kundi la wezi akiwa na umri wa miaka 14.

Alipata ujauzito huo baada ya mamake mzazi kumkutanisha na vijana wezi wa mtaani ambao walisisitiza kushiriki ngono naye ili kumpa pesa za matumizi nyumbani.

“Nilikutana na kijana ambaye alikuwa anajihusisha na wizi wa mabavu. Sikujua ilikuwa nia ya mama, wakati wa kuongea naye zaidi akanieleza huwa anapatia familia yangu chakula. Wakati mwingine aligharamikia kulipa karo yangu,” alisema Msoo.

 “Nilipopata mimba ndipo nilifahamu ana wapenzi zaidi ya kumi. Nilikuwa nashangaa mbona amenikodishia nyumba na harejei kila siku. Mwishowe niliachwa pekee yangu,” alisema Msoo.

Christine mwenye umri wa miaka 16 alipata ujauzito akiwa shule na kufukuzwa na mzaziwe ambaye hangeweza kulisha familia ya watoto watano.

“Maisha yamekuwa magumu kwangu, aliyenipa mimba alinikataa. Ujauzito wangu nilikaa nao kwa miezi mitatu bila kumwambia mama. Alipofahamu nina mimba aliniambia niondoke. Mama hakuwa na kazi, kila wakati tulilala njaa. Kuenda kliniki ilikuwa vigumu hata Sh100 sikuwahi pata,” alisema Atieno.

Hali yake ya afya ilizidi kuzorota kutokana na msongo wa mawazo.

“Miezi saba sikuwa nimeenda kliniki hata nilipojifungua sikuwa na mavazi ya mtoto,” alisema.

Afisa wa watoto eneo la Mathare Annisiah Gatwiri ametaka wazazi kuripoti visa vya wasichana wachanga wanaopata ujauzito kabla ya kutimu miaka 18.

“Kumekuwepo na changamoto ya kujua idadi kamili, wengi wakihofia afisi za serikali. Hawa watoto wanadhulumiwa na wanahitaji usaidizi kutoka kwa serikali na jamii. Lakini inakuwa tatizo sababu hatupati kurekodi visa hivi,” alisema Bi Gatwiri

Kulingana na Bi Gatwiri visa vya mimba za mapema vinachangiwa na wazazi ambao huhimiza watoto wao kutafuta pesa kutoka kwa wanaume kutokana na makali ya njaa.

Afisa huyo wa watoto aliambia Taifa Leo wakati mwingine jambazi mmoja anaweza kupachika wasichana 7 mimba ili kuwapa ulinzi.

“Wasichana wengi wanakabiliwa na umasikini zaidi, unapata kuna wale wazazi wanasukuma watoto kushikana na majambazi. Pia, kuna wale wanapata mimba za majambazi. Majambazi hao unapata wamekodishia nyumba saba za hawa wasichana. Wanaamini lazima wazae watoto wengi na wanawake tofauti kama njia ya kujisafisha, sijui kama ni cult,” alisema Bi Gatwiri.

Shirika la Community Voices Network linashugulikia wasichana 50 kwa kuwarejesha shuleni na kuendelea na masomo.

Msimamizi wa mradi huo, Ritah Anido anasema kuwa wanawapa kipao mbele wanaokumbwa na umasikini unaowaelekeza kutafuta pesa kwa njia isiyofaa.

“Wasichana wanaoshikana na majambazi, tunafanya mazungumzo ili kuwafahamisha jinsi ya kuepuka masuala hayo. Tunashirikiana na polisi kwa kuwashtaki wazazi ambao hawafahamu majukumu yao,” alisema Bi Anindo.

Utafiti 2023 umeonyesha Kaunti ya Nairobi ilirekodi mimba za mapema kwa asilimia 10. Utafiti huo ukionyesha umasikini na ukosefu wa masomo ulichangia kwa wasichana waliobalehe kupachikwa mimba za mapema. Wasichana hao wakiwa ni wa umri wa kati ya 15-19.

  • Tags

You can share this post!

Jinsi mkimbiaji Kipchoge alivyopokea shahada ya tunuku ya...

Pasta aliyekwama hotelini aomba asaidiwe na Sh370,000

T L