• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Malkia wa Chapati Nandi Hills anayepika unga 12 kwa siku na kujiingizia kibunda cha kuridhisha

Malkia wa Chapati Nandi Hills anayepika unga 12 kwa siku na kujiingizia kibunda cha kuridhisha

NA FRIDAH OKACHI

Ukosefu wa ajira ni changamoto miongoni mwa vijana na kusababisha baadhi yao kutegemea wazazi au walezi wao.

Vijana wengi baada ya kumaliza Kidato cha Nne au hata vyuo huwa na matarajio ya kupata ajira nzuri na kukwepa sekta ya jua kali ambayo inaweza kuleta faida kubwa, lakini kwa Nisha Jepkoech ni hali tofauti.

Bi Jepkoech,23, amejitosa katika biashara ya chapati ambayo inampa ya riziki ya kila siku na kumwezesha kukidhi mahitaji yake ya kimsingi na pia kusaidia wazazi wake.

Akiwa kwenye duka lake analotumia kufanya biashara yake huko Nandi Hills, Bi Jepkoech alisema kuwa aliazimia kuingia katika biashara ya chapati baada ya kukamilisha masomo kama njia ya kuepuka uvivu na kuwa tegemezi kwa wazazi wake, akibainisha wanawake wana mahitaji fulani ambayo wazazi hawawezi kutimiza.

“Kama msichana mwingine yeyote, nina mahitaji mengi, ndio sababu natia bidii kufanya kazi ili kupata riziki badala ya kuwategemea wazazi wangu. Biashara hii imedumu kwa miaka miwili, nina uwezo wa kupata mahitaji yangu ya binafsi. Kama mwanamke nalipa kodi ya Sh5,000 na kupata chakula cha kila siku,” alisema Bi Jepkoech.

Bi Jepkoech alianza na pakiti moja ya kilo 2 ya unga wa ngano. Anasema hadi sasa hupika na kuuza bunda zima kwa siku na kupata Sh4,500 kwa siku. Mbali na chapati, pia anauza chai na vibazi vinavyompa Sh5,500 kwa siku. Aidha, kutokana na wateja wengi amefanikiwa kuajiri wanawake wawili wanaomsaidia kwenye duka lake na pia kusambaza chapati kwa wateja wake wakubwa wanaotaka kuhudumiwa sehemu zao za kazi, sokoni na biashara.

“Nimeajiri wanawake wawili wanaonisaidia na ninawalipa Sh300 kwa siku. Wananisaidia kupeleka oda kwa wateja wangu nikiwa na kazi ya kupika, najua wakiondoka eneo hili watakuwa wamepata ujuzi wa upishi wa chapati ambao pia nilijifunza kutoka kwa mamangu,” alieleza.

Mfanyabiashara huyo ana ndoto ya kumiliki mkahawa mkubwa siku zijazo. Anasema huamka saa kumi na moja asubuhi ili kuhakikisha ifikapo saa kumi na mbili asubuhi chapati ziwe tayari kuwahudumia wateja asubuhi na hufunga kibanda chake cha chapati saa nne usiku kila siku isipokuwa Jumapilia mbayo ni siku yake ya ibada.

Kulingana na Bi Jepkoech, wateja wake ni kati ya watu wanaofanya kazi kwenye ofisi karibu na kazi yake pia, wanaoendesha bodaboda, wafanyabiashara, wanafunzi miongoni mwa wengine.

Bi Jepkoech alibainisha vijana wengi huishia kwenye msongo wa mawazo kutokana na kukosa nafasi za kazi lakini wana uwezo wa kujitengenezea biashara zao na kuongeza kuwa biashara nyingi zinazohitaji mtaji na ujuzi wa kuanzia kama vile chapati, mayai ya kuchemsha, kuchoma mahindi miongoni mwa mengine ambayo vijana wanapaswa kutumia ili kujitegemea kifedha.

“Sasa hivi na huu uchumi, vijana wanapaswa kujituma katika sekta ya juakali huku wakitafuta kazi nzuri zinazolipa. Vijana, hasa wanawake wanapaswa kuongeza juhudi zao ili kujitegemea,” alishauri.

  • Tags

You can share this post!

Polisi wawili kusotea jela kwa kujaribu kuzuia kukamatwa...

Mbunge wa Ghana aliyedhihaki Maguire akimlaumu kuwa...

T L