• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mama asimulia kortini jinsi jirani yake mwendeshaji bodaboda alimuua bintiye akidai ni shetani

Mama asimulia kortini jinsi jirani yake mwendeshaji bodaboda alimuua bintiye akidai ni shetani

Na JOSEPH OPENDA

Katika mpangilio uliodumu miezi sita, Lilian Waswa alimuacha bintiye wa miaka miwili na nusu, Marion Pendo, chini ya usimamizi wa Alice Wanyonyi alipoenda kazini.

Alizoea kumchukua mwanawe jioni alipotoka kazini na kumlipa Bi Wanyonyi Sh70 kila siku kwa huduma ya kumchunga mtoto Pendo.

Kila kitu kilikuwa shwari huku mtoto Pendo akiingiliana vyema na familia ya jirani wao. Hata hivyo, mnamo Disemba 30, 2022 mtoto huyo aliaga dunia katika njia tatanishi.

Siku hiyo, Bi Waswa, mwalimu wa shule ya msingi alienda nyumbani kwa Bi Wanyonyi kama desturi kumchukua mtoto wake.

Pendo alikuwa akicheza na mume wa Bi Wanyonyi, Joab Murunga, mwendeshaji bodaboda katika mtaa wa Nakuru Rhonda. Bi Waswa aliona mwanawe hakutaka kuondoka wakati huo na kuonelea kuenda nyumbani kuanza kupika chajio.

Aliporejea baada ya dakika 30 kuchukua sufuria kutoka nyumbani mwa Bi Wanyonyi, alimsikia Bw Murunga akimtaka mkewe aitwe mara moja huku akidai kumuua jini aliyekuwa nyumbani mwao.

Maneno yake Bw Murunga yalimshutua sana Bi Waswa ambaye hakujua iwapo kulikuwepo na jini lolote nyumbani humo. Alipojaribu kuingia, Bw Murunga alimzuia huku akitishia vita.

Kwa kuogopea usalama wa mwanawe, Bi Waswa alichungulia ndani na kumuona bintiye akiwa kwenye sakafu iliyojaa damu.

“Niliogopea usalama wa binti yangu aliposema, ‘ile jini imekuwa ikitusumbua nimeiua leo,” alieleza korti ya Nakuru alipokuwa akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Samuel Mohochi kuhusu mauaji ya bintiye.

Alisema kuwa Bw Murunga alimweleza kuwa yeye alikuwa ameliua jini wala sio mwanawe.

“Beryl, jirani, pia alichungulia na kumuona mwanangu akiwa kwenye sakafu iliyojaa damu huku viungo ndani ya ubongo vikiwa vimetapakaa. Mshukiwa bado alikuwa ameziba mlango,” akaelezea Bi Waswa.

Bi Vivian Atieno, jirani mwingine aliyetoa ushahidi kortini alisema kuwa aliisikia sauti ya Bw Murunga akiomba sana. Hali kadhalika, jirani mwingine alipoingia nyumba hiyo, alitoka akipiga nduru na kuelezea jamii ukweli.

Kundi la watu lilijumuika likitaka kumshambulia Murunga lakini polisi kutoka Rhonda walifika na kumuokoa kisha kuchukua mwili wa mtoto Pendo.

Mtaalamu wa uchunguzi wa serikali, Dkt Titus Ngulungu, alifanya uchunguzi na kugundua kuwa mtoto Pendo alifariki baada ya majeraha mengi ya kichwa, mpasuko mkubwa wa fuvu, na kukatwa ngozi.

Uchunguzi huo pia ulionyesha ishara za majeraha makubwa ya ubongo, kichwa kuvimba, na kuwa na majeraha ya michubuko katika sehemu mbalimbali.

Bw Murunga alikabiliwa na mashtaka ya mauaji na alipandishwa kizimbani mahakamani Januari, 19th 2023. Uchunguzi wa kiakili ulitupilia mbali uwezekano wa wazimu, ukithibitisha kuwa Bw Murunga alikuwa na uwezo wa kusimama kizimbani.

Tukio hilo la kutisha liliacha jamii katika mshtuko, likiibua maswali kuhusu usalama wa watoto na imani iliyowekwa katika mazingira yanayoonekana kuwa ya kawaida. Utaratibu wa kusikiliza kesi utaendelea tarehe 12 Februari, 2024.

  • Tags

You can share this post!

Ndoa yake ni ya machozi, yangu pia vilevile. Tunaweza...

Mbunge Maalum aacha wengi na mshangao kudai uchumi wa Kenya...

T L