• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Mbunge Maalum aacha wengi na mshangao kudai uchumi wa Kenya ‘umeanguka kuliko maziwa yake’

Mbunge Maalum aacha wengi na mshangao kudai uchumi wa Kenya ‘umeanguka kuliko maziwa yake’

NA MERCY KOSKEI

Mbunge Maalum Irene Mayaka, aliwaacha wabunge wenzake kwa mshangao baada ya kudai kuwa uchumi wa Kenya umeanguka kuliko maziwa yake.

Akizungumza wakati wa hafla ya Bunge Novemba 14, 2023 wakati wa kuchambua hotuba ya Rais William Ruto, Mayaka alisikitika kuwa uchumi unazorota kila uchao licha ya Rais kuahidi Wakenya kuwa mambo yatakua sawa baada ya kuchukua usukani.

Akiwasilisha hoja yake, mbunge huyo alitaka kujua ni kwa nini licha ya mafanikio mengi yaliyoorodheshwa na Rais kwa hotuba yake, gharama ya maisha bado ilikuwa ikipanda juu.

Akikashifu hotuba hiyo, alisema kuwa ushuru, Shilingi ya Kenya na gharama ya maisha imetoka chini kwenda juu, akisema kuwa ajenda ya Rais ya kuleta pamoja Wakenya walio chini ilikuwa ya kuhadaa watu.

Mayaka alisema kuwa gharama ya juu ya maisha, ongezeko la ushuru na bei ya mafuta ni doa kwa utawala wa Kenya Kwanza.

Kulingana na Mayaka, Rais anafaa kufahamu kuwa Wakenya wanalemewa na gharama ya juu ya maisha na pia kuelewa kuwa kuongeza ushuru ni hatua ya kufanya maisha kuwa magumu kwa raia.

“Nilitarajia kusikia mengi kuhusu masuala ya uchumi kutoka kwa Rais kwani tuko katika kiwango kibaya kiuchumi. Wakenya wanakumbwa na ushuru mpya kila kukicha. Tulitaka Rais atoe picha wazi ya vile hali ilivyo. Mambo ni mabaya sana katika nchi hii,” alisema.

Bi Mayaka pia alikosoa malipo mapya yaliyoletwa kwa pasipoti na kitambulisho akisema kuwa ni pigo kwa watu ambao tayari wanahangaika.

Mbunge huyo alishangaa vipi Wakenya watalipia Sh1,000 ili waweze kupata kitambulisho ilhali huduma hizi zimekuwa bila malipo tangu uhuru.

“Hiki ni kielelezo cha siku zijazo zenye wasiwasi, wanasiasa tutakuwa na hali mgumu mwaka wa 2027 tutakaporudi kuomba kura kwa wanachi kwani tutalazimika kujibu maswali magumu kutoka kwao,” alisema.

“Tutalazimika kulipa wapiga kura ili waende wachukue vitambulisho ndio waweze kutupigia kura,” akahitimisha.

  • Tags

You can share this post!

Mama asimulia kortini jinsi jirani yake mwendeshaji...

Jinsi wenye maduka Toi Market, Kibera wamejipanga kwa mkasa...

T L