• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Marion Mwende Muema: Nalenga kuwa nyota gwiji katika uigizaji duniani

Marion Mwende Muema: Nalenga kuwa nyota gwiji katika uigizaji duniani

Na JOHN KIMWERE 

NI ndoto ya kila msanii kuona anaimarika katika kazi zake na kutambulika kote duniani. 

Marion Mwende Muema ni kati yao ambaye kamwe haachwi nyuma licha ya pandashuka ambazo hupitia kwenye shughuli za uigizaji.

Kando na uigizaji, dada huyu aliyezaliwa mwaka 1992 hujishughulisha na biashara ndogo ndogo.

Pia amehitimu kwa shahada ya uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Daystar.

Anaorodheshwa kati ya wasanii wanaokuja wanaolenga kuibuka waigizaji tajika miaka ijayo.

”Napenda uigizaji zaidi maana huwa najihisi nipo huru kuonyesha taaluma yangu,” asema.

Anaongeza kuwa kamwe hawezi kuweka katika kaburi la sahau kuwa filamu iitwayo ‘Country Queen‘ ilimtia motisha zaidi kujiunga na jukwaa la maigizo.

Kati ya waigizaji wa filamu hiyo waliomvutia kwa uhondo wao akiwa Melissa Kiplang’at na Mkamzee Mwatela.

Anashikilia kuwa anatamani sana kutinga upeo wa wasanii mahiri duniani kama vile Queen Latifa mzawa wa Amerika.

Anadokeza kuwa kazi za msanii huyo huvutia wengi akitoa mfano wa filamu iitwayo ‘Equalizer.’

Latifa pia ameshiriki filamu nyingi tu ikiwemo ‘Just Wright,’ ‘Last Holiday,’ ‘Joyful Noise,’ na ‘Set it off,’ kati ya zingine.

Chipukizi huyu anajivunia kushiriki filamu kama ‘Njoro wa Uba,’ ‘Selina,’ na ‘County 49’ kati ya zingine.

Anasema kuwa tangia akiwa mtoto alidhamiria kuwa mhandishi.

“Kusema ukweli nikiwa mtoto nilikuwa na ndoto ya kutengeneza barabara na daraja.”

Anasema hakuna msanii asiyependa kufanya vizuri.

Kwa hivyo anatamani sana kufanya kazi na waigizaji mahiri duniani kama Thuso Mbedu (Afrika Kusini), aliyeshiriki filamu kama ‘Thunzi, na ‘Underground railroad.

Pia angependa kujikuta kwenye jukwaa moja na Jackie Appia (Ghana) ambaye ameshiriki ‘Perfect picture,’ na ‘Divine love,’ kati ya zingine.

Kwa wasanii wa humu nchini angependa kufanya kazi nao Mumbi Maina ambaye ameshiriki filamu kama ‘Mali’ (NTV) na Salem (Maisha Magic).

Mwingine akiwa Catherine Kamau anayejivunia filamu kama ‘Disconnect 1&2′ (Netflix,’ na ‘Sue na Johnnie,’ (Maisha magic).

Msanii chipukizi Marion Mwende Muema. Picha / John Kimwere

Anashikilia kuwa ndani ya miaka mitano ijayo, analenga kutimiza mambo kadhaa yakiwemo kufanya matangazo makubwa kadha wa kadha.

Pia analenga sana kushiriki filamu fupi fupi nyingi kwenye juhudi za kukuza talanta yake zaidi kwa ajili ya kufanya filamu kubwa siku za baadaye.

Anashauri maprodusa wa filamu wajifunze kufanya utafiti kufahamu yanayoendelea katika sekta ya uigizaji.

”Huwa sio picha nzuri wakati tunazalisha filamu ambayo pengine ilifanywa na wengine maana hali hiyo hufanya wafuasi wetu kukosa motisha kuitazama,” akasema wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Changamoto  

Anasema wengi wao hupitia pandashuka nyingi kwa sababu ya maumbile yao.

”Wakati mwingine sisi wenye mwili mkubwa kiasi hukosa nafasi za uigizaji wala sina shaka kusema kuwa maprodusa wetu wakomeshe mtindo huo,” akasema.

Anasema kuwa serikali za kaunti zinastahili kutilia mkazo sekta ya uigizaji maana ina uwezo kuajiri wavulana na wasichana wengi tu na kupunguza ukosefu wa ajira nchini.

Hali kadhalika, anashauri maprodusa wa humu nchini kuwa wabunifu kwenye jitihada kuhakikisha wanafanya kazi nzuri ya kuvutia wapenzi wa burudani katika mataifa ya kigeni.

Isitoshe, anashauri wenzake kuwa nyakati zote wanastahili kutia bidii na kutovunjika moyo kwenye juhudi kusaka ajira ya uigizaji.

Pia anasema kuwa anafahamu kwa kumwaminia Mungu wakati utakapofika wa milango kufunguliwa hamna atakayezuia.

  • Tags

You can share this post!

Gavana Timammy afokea wachafuzi wa bahari

Kajala akiri kuchumbia mwanasiasa

T L