• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MARY WANGARI: Kenya na Somalia zitafute njia ya kutatua mzozo huu wa kidiplomasia

MARY WANGARI: Kenya na Somalia zitafute njia ya kutatua mzozo huu wa kidiplomasia

Na MARY WANGARI

MWISHONI mwa mwaka uliopita, Somalia ilitangaza kwamba imekatiza uhusiano wake na Kenya, hatua ambayo ilivutia mjadala mkali.

Somalia iliishutumu Kenya dhidi ya “kuingilia kila mara masuala yake ya ndani na kuhujumu hadhi yake kama taifa,” huku ikiwapa wajumbe wa Kenya muda wa siku saba kuondoka nchini humo.Uamuzi huo uliashiria uhasama ambao umekuwa ukitokota kwa muda sasa kati ya mataifa hayo mawili ya Bara la Afrika Mashariki.

Hatua hiyo ni mwanzo wa uhasama kidiplomasia ambao huenda ukasababisha athari hasi na hatari katika bara hili endapo hautasuluhishwa kikamilifu kwa dharura.

Uhalisia ni kuwa, mataifa haya mawili hayako tayari kwa gharama ya kuzorota kwa uhusiano kati yake ikizingatiwa kwamba Kenya na Somalia zinashiriki sehemu kubwa ya mpaka pasipo kutaja mahusiano ya kijamii na kiuchumi.

Maelfu ya wakimbizi kutoka Somalia wamekimbilia usalama wao na kupata makao na hifadhi nchini Kenya bila kusahau raia wengi wa asili ya Kisomali wanaoendelea kunawiri kibiashara nchini.

Hatuwezi kusahau jinsi Kenya ilivyowekeza pakubwa katika kuhakikisha amani imerejea Somalia kwa kuandaa na kushiriki vikao kadhaa muhimu vilivyowezesha taifa hilo kujisimamisha tena.

Isitoshe, Kenya ni miongoni mwa mataifa ambayo yametuma wanajeshi wake katika Oparesheni ya Umoja wa Afrika Somalia (AMISOM) kwa lengo la kuangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Shabab, ambao wamekuwa kero na tishio kwa usalama katika bara hili.

Kenya pia haijaachwa mikono mitupu kwa sababu raia wake wameweza kuingia Somalia kirahisi na kufanya kazi huku wakichangia pakubwa katika sekta mbalimbali nchini humo.Mambo yamekuwa yakiendelea shwari kiasi cha Somalia kuwa na mpango mahsusi wa kutoa vyeti vya usafiri kwa raia wa Kenya wanaowasili nchini humo kwa shughuli za kikazi, hadi yalipobadilika ghafla Desemba.

Ni kweli kuna masuala nyeti yanayovuruga uhusiano kati ya nchi hizi yakiongozwa na mvutano kuhusu mipaka ya maji pamoja na vituo vya mafuta na gesi katika Bahari Hindi.

Mzozo kuhusu mipaka ya maji ambao uamuzi wa kesi yake katika Mahakama ya Haki Kimataifa unatazamiwa kutolewa mnamo Machi, umechangia pakubwa kuzorota kwa uhusiano kati ya Nairobi na Mogadishu.Licha ya tofauti zote hizo, ni dhahiri kwamba serikali za mataifa haya zinahitajiana ili kuhakikisha ufanisi na usalama wa raia wake.

Bado kuna muda wa kuchagua mkondo wa amani na kidiplomasia katika kurejesha na kuimarisha uhusiano kwa kushirikisha mazungumzo.

You can share this post!

WANTO WARUI: Huenda wanafunzi wengi wakakosa mitihani ya...

Kwa kila tone la mvua, wakazi wahofia usalama wao