• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 6:07 PM
Masaibu ya afya: Mama asiyeshuhudia hedhi alivyojifungua watoto wanne  

Masaibu ya afya: Mama asiyeshuhudia hedhi alivyojifungua watoto wanne  

NA FRIDAH OKACHI

KILA jua linapochomoza, Zipporah Nyambura anazidi kulemewa na msongo wa mawazo kufuatia tatizo lake la kiafya.

Nyambura ameishi miaka 24 bila kuona hedhi.

Hedhi, ni kipindi maalumu katika mzunguko wa mwanamke mwenye umri wa kuzaa ambacho kwa kawaida kinarudi kila baada ya mwezi mmoja hivi na hutokwa na damu kwenye uke.

Licha ya changamoto ya kiafya anayopitia, Nyambura amefanikiwa kupata watoto wanne.

Mara ya mwisho kuona hedhi ikiwa ni mwaka 1999, anasema ana watoto wawili wenye tatizo la kuzungumza na kusikia.

Nyambura katika ujana wake alifahamu hedhi zake huja kwa muda wa saa mbili au tatu, akidhania hali hiyo itabadilika miaka ilivyosonga.

Akiwa shule ya msingi alishangaa jinsi wenzake walivyokuwa wakitumia sodo kila mwezi.

Aidha, akiwa na umri wa miaka 17 alishuhudia hedhi yake ya kwanza.

Kwenye masimulizi, anakiri siku hiyo ilikuwa yenye furaha isiyomithilika kwake.

Hata hivyo, tabasamu hiyo ilifikia kikomo saa tatu baadaye hedhi ilipoisha.

Miaka mitano baadaye, alifunga ndoa akiwa na matumaini kuwa angeona damu ya mwezi – hedhi.

Muda ulivyosonga, matarajio yake yalififia.

Anasimulia kwamba alipata uja uzito ambao hakuwa ameupangia.

Alipotembelea kituo cha afya na kufanyiwa vipimo, alifahamu yupo kwenye kundi la damu la O hasi (O-).

Zipporah Nyambura akiwa na baadhi ya wanawe. PICHA|FRIDAH OKACHI

Hakufahamishwa na yeyote kuwa alihitaji kudungwa sindano ya kupunguza makali kueneza chembechembe za damu kwa mwanawe.

Muda wake wa kupata mtoto ulipotimia, alijifungua na kuondoka hospitalini.

“Daktari alinieleza nisitumie mbinu yoyote ile ya uzazi kwa kuwa sina mayai. Onyo la pili lilikuwa nisipate ujauzito mwingine kwa kuwa nipo kwenye hatari ya kupoteza maisha au kupoteza ujauzito kila wakati,” alielezea wakati wa mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Licha ya onyo hayo, miezi minne baadaye alishika mimba nyingine.

Ujauzito huo wa pili ulimshinikiza kutembelea hospitali tatu kufahamu zaidi kuhusu hali yake.

Wakati wa kujifungua katika hospitali ya Pumwani, alitenganishwa na mwanawe.

Muda huo, wauguzi na daktari walikuwa katika harakati za kutafuta dawa ambazo zilimgharimu Sh14, 000.

Umaskini uliosababisha kukosa hela ulichangia kudungwa baada ya saa 72 na kuruhusiwa kumnyonyesha mwanawe.

“Wakati huo, niliondoka Pumwani nikijua nitatumia sindano ya upangaji uzazi ya miaka mitano. Baada ya siku nane, nilitembelea kituo cha afya kuwekwa lakini nikapatikana na ujauzito tena siku chache baadaye,” Nyambura alisimulia.

Mama huyu anashangaa alivyoshika mimba bila hedhi kwa muda wa miaka 24.

Kutia msumari moto kwenye kidonda, wanawe wawili wana tatizo la kuzungumza na kusikia.

Licha ya kuwepo na changamoto ya mawasiliano nyumbani kwake, Nyambura anasema kuwa watoto wake wanne ni miujiza.

Aidha, wamejaaliwa vipaji vya kipekee.

“Wanaelewa masuala ya stima sambamba,” akasema wakati wa mahojiano nyumbani kwake Kabiria, Dagoretti.

Jackson Mutinda, ambaye ni daktari wa masuala ya uzazi, anasema kati ya wanawake 100 wanaomtembelea kwa minajili ya huduma, hupatana na mmoja anayepitia hali kama ya Nyambura.

“Kubadilika kwa Homoni, kula chakula kisicho na madini ya kutosha ni miongoni mwa visababishi vya hedhi kupotea,” Dkt Mutinda anasema.

Kulingana na mtaalamu huyu, si ajabu mwanamke kukosa hedhi na atunge ujauzito anaposhiriki mapenzi bila kinga.

“Mayai ya uzazi yanaweza kuwa tayari kushika mimba bila ufahamu wa mwanamke.”

  • Tags

You can share this post!

Masoko Nairobi na Kiambu yanayouzia wateja mbegu za avocado...

Embarambamba: Makabila yote Kenya yananipenda, Kisii pekee...

T L