• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 5:04 PM
Matineja waliopata mimba za mapema Kanduyi waingia ukahaba na madereva wa malori

Matineja waliopata mimba za mapema Kanduyi waingia ukahaba na madereva wa malori

NA JESSE CHENGE

Eneobunge la Kanduyi ndilo linaloongoza katika Kaunti ya Bungoma kwa mimba za matineja, ambazo zinawalazimisha baadhi yao kujihusisha na ukahaba ili kujikimu kimaisha.

Kanduyi, ambayo ina barabara kuu ya kuelekea Bonde la Ufa, kwa mtazamo wa kwanza ni mji mzuri kwa biashara. Hata hivyo, chini ya harakati zake na msongamano wa watu, ina idadi kubwa zaidi ya mimba za wasichana wachanga katika eneo hilo.

Ili kujikimu, baadhi ya matineja waliozaa na wanaozongwa na umasikini na ugumu wa maisha wamezama katika ukahaba, yaani biashara ya ngono na madereva wa malori ya masafa marefu ambao huwa wamejaa pesa.

Katika kijiji cha Mechimeru, Taifa Leo inakutana na mama tineja mwenye umri wa miaka 19, ambaye tutamwita Mary.

Anakumbuka jinsi mpenzi wake aliyekuwa mwanafunzi mwenzake alivyokuwa anapitia nyumbani kwao, akizungumza naye na kumwambia kuwa anampenda. Baada ya miezi kadhaa, alimwomba wakutane sokoni, ambapo aliishia kumpeleka nyumbani kwake.

“Sikuwa tayari kufanya mapenzi na yeye, na nilimsihi asubiri kidogo hadi nimalize mtihani wangu wa KCPE. Hakukubali na aliendelea kunirai hadi hatimaye nikakubali. Halafu pia hakutumia kinga. Baada ya mwezi mmoja na nusu, nilianza kuvimba na kuhisi usingizi mwingi. Mamangu alishuku hali yangu, kwa hivyo alinipeleka kliniki ya Mechimeru kufanya kipimo cha mimba, ambapo ilithibitishwa kuwa nilikuwa mjamzito,” anahadithia.

“Tuliporudi nyumbani na baba akasikia habari hizo, walinifukuza kwa hasira. Nilikwenda kwa mpenzi wangu, ambaye pia aliniambia nitafute mahali pengine pa kwenda. Nikiwa nimekwama, nilianza kuwaza kuhusu kutoa mimba, lakini nilibadili mawazo yangu nilipogundua kuwa mimi ndiye niliyekosea na mtoto hakuwa na hatia,” anaelezea Mary.

Wakati huo alikuwa Darasa la Nane, na alilazimika kuacha shule kumlea na kumtunza mtoto wake kwa muda. Baada ya kujifungua, wazazi wake walimkubali tena, na hivi karibuni alirudi shuleni kuendelea na masomo. Hata hivyo, kulikuwa na sharti: lazima mpenzi wake amuoe wakimaliza shule.

Ili kuhakikisha anamaliza shule bila mimba nyingine, mamake alimshauri apate sindano ya kupanga uzazi ya miaka mitatu. Hata hivyo anasisitiza hashiriki tena ngono na mpenzi wake.

Mary anasema ameona zaidi ya wasichana 20 katika kijiji chake wakipata mimba na kuacha shule. Hatimaye, kwa shinikizo la gharama kubwa ya maisha, wanaishia kutafuta kazi ya ujakazi huku wengine wakijikuta mitaani.

Katika kaunti ambayo ina kiwango cha mimba za utotoni cha asilimia 19, ambacho ni cha juu kuliko wastani wa nchi wa asilimia 15, Wilaya ya Kanduyi ina mengi ya kulaumiwa kwa matatizo yake.

Kwanza, ina idadi kubwa ya watu, ikisababishwa na makazi mabaya zaidi katika kaunti hiyo. Kutokana na umaskini, madereva wa malori ya umbali mrefu, ambao hupumzika katika mji huo, hutoa chanzo rahisi cha pesa katika biashara ya ukahaba ambayo hufanywa kwa saa 24.

Haya ni kwa mujibu wa Jesse Wamocho, Mratibu wa Afya ya Vijana na Watoto wa Kaunti ya Bungoma. Anasema kuwa hali hiyo imesababisha kuongezeka kwa mzigo wa Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika eneo hilo, ambalo linarekodi maambukizi mapya 98 kwa wiki miongoni mwa vijana.

“Idadi inaongezeka. Tuna matatizo ya watoto kuacha shule kwa kiwango kikubwa, viwango vya vifo vya juu miongoni mwa vijana na kuongezeka kwa idadi ya wafanyakazi wa ngono miongoni mwa vijana. Kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha wanafunzi kuacha shule na masuala ya kiuchumi, wengi wao wanajiunga na biashara ya ukahaba,” alisema.

“Katika kaunti yetu, wafanyakazi wa ngono sasa wanawajumuisha wadogo. Kwa hiyo, mteja anapofika, anapewa huduma za ngono za wadogo,” alisema Wamocho.

Mwaka 2022, Wizara ya Afya ilitoa ripoti ya maambukizi mapya ya 92 kati ya watu wenye umri kati ya miaka 10 na 19 katika Kaunti ya Bungoma, na maambukizi 249 kati ya wale wenye umri kati ya miaka 15 na 24. Kati ya wale wenye umri kati ya miaka 10 na 19, vifo 43 vilirekodiwa.

Wamocho anaeleza kuwa upokeaji wa njia kupanga uzazi, ambazo zingekuwa suluhisho bora katika kuzuia mimba za udogoni, umekwamishwa na changamoto kama sera zinazohitaji idhini ya mtu mzima au mzazi kwa kijana kupata huduma hizo. Hii huwalazimu kutafuta njia za uzazi wa mpango katika maduka ya dawa kwenye masoko wazi.

“Ningependa kuwepo sera ambayo inaweza kuingilia kati na kusawazisha hili. Sera ya sasa inasema mtoto chini ya miaka 18 hawezi kupata njia za kupanga uzazi isipokuwa kama kuna mtu mzima anayeweza kutoa idhini.”

“Ili kijana aweze kuzipata, wanalazimika kusimama katika foleni ndefu, labda pamoja na majirani zao ambao wanaweza kuwafichua. Kwa sasa, vituo vya huduma kwa vijana vimejumuishwa pia, kwa hiyo, vijana hawawezi kwa urahisi kufikia vituo hivyo. Vituo hivyo pia hufanya kazi kutoka Jumatatu hadi Ijumaa wakati wao wapo shuleni. Jumamosi, ambapo vijana wanapatikana, vituo hivyo vimefungwa,” anaelezea.

  • Tags

You can share this post!

Olunga kupigania tuzo na masupastaa Ronaldo, Benzema ukanda...

Diamond afunguka kuhusu madai ya kupunja wasanii wa Wasafi

T L