• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 3:58 PM
Matumaini ya stima kuacha kupotea Kisii washukiwa wa wizi wa transfoma wakitiwa mbaroni

Matumaini ya stima kuacha kupotea Kisii washukiwa wa wizi wa transfoma wakitiwa mbaroni

NA WYCLIFFE NYABERI 

Polisi mjini Kisii wamemkamata mwanamke mmoja na wanaume wawili wanaoshukiwa kuharibu transfoma katika eneo hilo.

Kulingana na taarifa kutoka kwa kampuni ya usambazaji nguvu za umeme ya Kenya Power, watatu hao walikamatwa katika maeneo ya Mosocho, Oyugis na Nyakoe wakati wa operesheni kali ya mashirika mbalimbali iliyolenga waharibifu wa miundombinu hiyo muhimu.

Wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kisii Central.

“Mshukiwa mmoja, mwanamke, alipatikana na mafuta yanayoshukiwa kuwa ya lita 10 za mafuta ya transfoma na mita ya kulipia ya Kenya Power iliyoibwa. Mshukiwa mwingine wa kiume alikamatwa na vifaa vinavyoshukiwa kuwa ni vya wizi vya Kenya Power huku wa tatu akiwa mfanyabiashara wa vyuma chakavu viliyopatikana na nyaya za shaba aina mbalimbali,” sehemu ya taarifa kutoka kwa kampuni hiyo ilisema.

Wanatarajiwa kufikishwa Mahakama Jumatano Oktoba 25 kujibu mashtaka mbalimbali kulingana na Sheria ya Nishati.

Zaidi ya mwezi mmoja uliopita, ongezeko la wizi wa transfoma katika eneo la Marani huko Kitutu Chache Kaskazini lilizua wasiwasi miongoni mwa wakazi kuhusu kukatika kwa umeme kwa mara kwa mara.

Kama njia mojawapo ya kushughulikia hali hiyo, Kamishna wa Kaunti ya Kisii Tom Anjere, aliwaongoza wanachama wengine wa Kikosi cha Usalama cha Kaunti kupanga mikakati ya kukabiliana na uharibifu huo.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini, Japheth Nyakundi, ambaye alitoa wito kwa kila mtu kuungana na maafisa wa usalama ili kwa pamoja kukabiliana na wizi huo.

Kamishna huyo aliamuru machifu na manaibu wao kuendesha mikutano ya kila wiki, ambayo itatathmini hali katika maeneo wanayosimamia kwa kujumuisha vijana na viongozi wa bodaboda.

“Tumewaomba machifu na wasaidizi wao kufanya mikutano ya kila wiki katika maeneo yao. Tumewataka wahusishe vijana na viongozi wa bodaboda kwa sababu watu hawa kila mara hupata habari moja kwa moja na mapema,” Bw Anjere alisema.

Bw Anjere aliongeza kuwa kuendelea mbele, wataongeza doria za polisi katika eneo hilo. Alitoa onyo kwamba wale watakaopatikana na hatia watakamatwa na kufikishwa mahakamani.

Kulingana na mbunge Nyakundi, takriban transfoma 12 zimeharibiwa siku za hivi karibuni huko Marani. Hii alisema imeathiri usambazaji wa umeme kwa hospitali, shule na makazi.

Mbunge huyo alitoa wito kwa maafisa wa polisi kujibidiisha na kukabiliana na mtu yeyote anayeharibu vifaa hivyo bila huruma.

  • Tags

You can share this post!

Disko Matanga sasa marufuku Kilifi kuzima kuchafuliwa kwa...

Slayqueen aachwa kwa mataa sponsa aliporudi kwa mkewe

T L