• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 8:55 PM
Disko Matanga sasa marufuku Kilifi kuzima kuchafuliwa kwa vigoli

Disko Matanga sasa marufuku Kilifi kuzima kuchafuliwa kwa vigoli

KNA na LABAAN SHABAAN

KAMATI ya Usalama wa Kaunti ya Kilifi imezima maombolezi ya Disko Matanga kwa kuhusishwa na unajisi wa wasichana na mimba za utotoni eneo hilo.

Tangazo hili linajiri wakati kuna suitafahamu ya nani wa kusema kuhusu ufaafu wa disko matanga kwa sababu inaungwa mkono na wanasiasa.

Kwa mfano, Waziri wa Jinsia na Utamaduni Aisha Jumwa ambaye ni mmoja wa viongozi wa Kilifi,  amekuwa akipigia debe desturi hii kwa muda mrefu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Josephat Biwott amehusisha utamaduni huu na unyanyasaji wa wasichana kingono unaoishia kuleta mimba za udogoni.

Bw Biwott ametoa onyo kali dhidi ya familia zinazoomboleza endapo zitaruhusu disko hizi wakati wa maombolezi.

“Tumesema hakuna disko matanga. Tutawakamata wanafamilia wanaoendeleza mazishi pamoja na disko matanga kwa sababu ni wao wanaowaumiza watoto wetu,” alionya Bw Biwott aliyezungumza katika Sherehe za Mashujaa Ijumaa Oktoba 20, 2023.

“Tutamshtaki yeyote ambaye ana disko matanga nyumbani mwake. Ninaamuru maafisa wote wa usalama kutoka leo kuwa hatutakubali wasichana wetu wapate mimba za mapema kwa sababu wengine wanataka kupata pesa kupitia disko hizi,” aliongeza.

Kwa moto uo huo, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Kilifi, Fatuma Hadi, alikariri uamuzi huu dhidi ya burudani ya usiku na mchana yenye kupalilia maovu.

“Changamoto yetu imekuwa visa vingi vya unajisi.  Wengi wamefungwa jela. Juma lililopita mmoja alifungwa jela miaka 30. Tulikaa chini na kujua sababu ya visa hivi kuongezeka ni disko matanga,” alisema.

Zaidi ya wanaume 40 kutoka Kaloleni wametiwa ndani katika miezi michache iliyopita kwa sababu ya makosa ya unajisi.

Mwaka uliopita, Waziri Jumwa alikashifu serikali ya Kaunti ya Kilifi akisema iliharibu biashara ya burudani kwa kupiga marufuku disko matanga.

Desturi hii huwa maarufu kwa utumizi wa vyombo vya muziki kupiga muziki wa sauti ya juu siku chache kabla ya mazishi.

Familia zilizofiwa hutumia hafla hizi kuchanga pesa kabla ya mazishi.

Watu wa jamii wakijumuisha watoto hukutana hapo kwa burudani bila malipo hasaa usiku.

  • Tags

You can share this post!

Haitawezekana wahubiri kuwa na digrii – Maina Njenga

Matumaini ya stima kuacha kupotea Kisii washukiwa wa wizi...

T L