• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mola Subuhaanahu Wata’ala ndiye mmiliki pekee wa siri za maisha waja wake

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mola Subuhaanahu Wata’ala ndiye mmiliki pekee wa siri za maisha waja wake

Na ALI HASSAN

KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo.

Kwa kudra zake Maulana tumejaaliwa siku hii nyingine aula na tukufu ili kuambizana kuihusu dini yetu tukufu ya Kiislamu.

Twamshukuru, kumpwekesha na kumsifu Mola ambaye ndiye muweza wa kila jambo.

Ndiye pekee anayestahiki kuabudiwa na kuenziwa. Ndiye pekee mwenye kuumba na kuumbua. Sawia, twamtilia dua na kumtakia maombi ya kheri Mtume wetu (SAW).

Maisha ya sasa changa-moto zi tele, mwanzo na hili janga la Corona!

Kila kukicha afadhali ya jana. Kila sekunde wanazaliwa watoto. Tuwatilie dua wadumu kwenye dini.

Kila nukta wapo ndugu zetu wanaoga dunia. Tuzidishe ibada na dua wasamehewa madhambi yao, nasi tuwe na mwisho mwema na tujaaliwe kuingia peponi.

Mada yetu leo hii ndugu zanguni inaendana na methali ya wahenga ambayo husema kuwa hakuna siri ya wawili. Hata mtu binafsi hana siri.

Mmiliki pekee wa siri za maisha yetu ni Mola. Mbona kusema hivi? Hakuna siri machoni pake Mola.

Hata tukajificha wepi, kwenye kiza kipi, kichochori kipi, tukumbuke kuwa yupo malaika anayakili yote.

Hapo ulipo ndugu yangu, pamoja nami, yapo mambo mengi tu ambayo tulidhani kuwa tumeyafanya ki-siri. Kumbe? Yanakuja kuwekwa paruwanja baadaye. Tuchukue nafasi hii kutubia.

Kama zipo siri za maovu ambayo tumeyafanya sisi – hakuna mja mkamilifu – tuombe radhi.Mola wetu mtukufu ni mwingi wa rehema na msamaha.

Gumzo letu leo hii limetokana na baadhi ya siri ambazo zimekuwa zikifanywa na watu, wenye heshima na taadhima, na sasa siri hizo zimefichuka.

Tutangulize kimbele kusema hapa kuwa wanasema Waswahili ukiona mwenziyo ananyolewa, chako kitie maji. Sawa na kauli isemayo kuwa ‘yaseme sana ya watu, chunga yasikufike’.

Ama kwa lugha nyingine ni kuwa hujafa hujaumbika. Hakuna mja mkamilifu.

Kuibuka kwa siri za watu na kisha kuja kuwaathiri, kuwaaibisha na kuwapaka tope, kunatufunza nini? Tunawachukuliaje? Tuishije? Na hasa watu ambao ni viongozi au wamejukumika katika wadhifa fulani.

Cha kuatua moyo sana ni kuwa zinafichuka siri kama hizi zikiwazingira viongozi wa dini.

Ya Rabi tunusuru.

Wiki hii zimefichuka habari kutoka nchini Ufaransa ambapo viongozi wa dini wamekuwa wakiwatesa na kuwadhulumu kingono wanafunzi wapatao laki mbili! Subhannallah!

Hii si mara ya kwanza kufichuka sakata kama hizi ambazo zinawahusu viongozi wa dini. Dunia hii dunia jamani. Ewe Mola tuonee imani na utusamehe.

Ndoa zinafichuliwa na mawi, siri, uhuni na kuvunjika kila leo. Nyingine zikifichuliwa maovu kutokana na mauaji. Tunazipata siri hizi katika vyombo vya habari. Namna mume au mke alivyokula njama na genge la majambazi kumuua mumewe au mkewe.

Vipi kuhusu namna wafanyi-biashara waliokuwa kama chanda na pete, wanavyoishia kuuana. Kisa na mkasa? Mali.

Maskini tumbo. Tamaa mbele mauti nyuma. Unamuua mwenziyo ndio uishi hadi lini jamani?

Visa vya wizi, ufisadi, maovu na kila aina ya dhambi zinafichuliwa kila kukicha katika maisha yetu.

Viongozi mbali mbali wakifichuliwa na siri walizodhani walifanya kizani. Kumbe?

Siku si nyingi baadhi ya viongozi walikutikana na hatia ya ufujaji wa mamilioni ya pesa wakati wa mashindano ya Olimpiki huko Rio, nchini Brazil.

Nani amesahau sasa hivi mitaani na katika vyombo vya habari gumzo ni kuhusu viongozi, wazito, wanavyopora, kukwepa kulipa ushuru na kuyaficha mapeni yao katika akaunti za siri. Nje ya nchi zao!

Hizo sasa hivi zinazungumzwa kote kote duniani kama pandora. Unaweka wepi uso unapokabiliwa na shtuma kama hizi? Kashfa kama hizi utaupata wepi usingizi?

Ama kweli waja tumeumbiwa nyoyo na roho ngumu kweli!

Wapo wasanii, waigizaji na watu mashuhuri pia wametajwa. Inatuhusu sana hiyo. Hata nasi tumo. Nakumbuka msanii/mwigizaji maarufu sana Billy Cosby, ijapo madai hayo ya dhuluma za ngono, yalikuja kufutiliwa mbali, jina lake lilipakwa tope.

Hata akatumikia kifungo korokoroni. Msanii aliyevuma sana R. Kelly, amekutikana na hatia ya kuwadhuluma kingono watoto wadogo mno. Anasubiri hukumu.Afrika Kusini, kutaja moja ya nchi tu barani Afrika, aliyekuwa rais Jacob Zuma yupo taabani. Ufaransa je?Hakuna siri mja mwenzangu.

Ijumaa Mubarak

[email protected]

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Baadhi ya njia ambazo Mu’umin...

Joho aagizwa kuweka wazi kandarasi ya mradi Buxton