• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 12:43 PM
Joho aagizwa kuweka wazi kandarasi ya mradi Buxton

Joho aagizwa kuweka wazi kandarasi ya mradi Buxton

Na PHILIP MUYANGA

GAVANA wa Mombasa, Bw Hassan Joho, pamoja na maafisa wakuu wa kaunti hiyo wameagizwa na mahakama wafichue kandarasi na makubaliano kuhusu ujenzi wa majumba mapya mtaani Buxton.

Ujenzi huo unaoendelezwa na kampuni ya Buxton Point Appartments inayohusishwa na mwanasiasa anayepanga kuwania ugavana Mombasa, Bw Suleiman Shahbal, umekuwa ukikumbwa na migogoro tangu mradi ulipoanzishwa.

Jaji Eric Ogola alimwagiza Bw Joho, Katibu wa Kaunti, na Waziri wa Ardhi, Makao na Mipango ya Ujenzi katika kaunti, Bw Tawfiq Balala kuwasilisha stakabadhi hizo kwa mashirika matatu ya kijamii kabla ya siku 30 kukamilika.

Mashirika ya kutetea haki za kijamii ya Legal Advice Centre, Haki Yetu St Patrick’s na Transparency International yalikuwa yamewasilisha ombi mahakamani kutaka kandarasi na makubaliano kati ya kaunti na kampuni hiyo ya Bw Shahbal ziekwe wazi kwa umma.

“Baada ya kuzingatia utetezi wa washtakiwa, sijaridhishwa kuwa wana nia njema kuhusiana na masuala ya kuwasilisha maelezo ya makubaliano yanayohusu mradi wa Buxton,” akasema Jaji Ogola.

Jaji alisema, badala ya kuwasilisha maelezo yaliyotakikana jinsi walivyoagizwa awali, washtakiwa waliamua kulaumu walalamishi.

“Kwa msingi huo, washtakiwa walikaidi agizo lililokuwa limetolewa na mahakama Desemba 12, 2016,” akasema Jaji Ogola.

Alizidi kusema kuwa, takriban mwaka mmoja baada ya kampuni na kaunti kuweka makubaliano, Bw Balala alidanganya na kupotosha mahakama kuwa shughuli ya utoaji zabuni kuhusiana na mradi wa ujenzi Buxton ilikuwa haijakamilishwa na hivyo basi maombi ya kutaka maelezo kuhusu zabuni hiyo hayangeweza kutekelezwa.

Kupitia kwa wakili Willis Oluga, mashirika hayo matatu yaliwasilisha ombi kutaka maafisa hao wa kaunti waitwe mahakamani kuonyesha kwa nini wasifungwe jela kwa miezi sita kwa kutotii agizo la mahakama.

Mashirika ya Legal Advice Centre, Haki Yetu St Patrick’s na Transparency International yalikashifu maafisa wa kaunti kwa kuanza kutekeleza ujenzi bila kutii agizo lililohitaji wapewe maelezo kuhusu mradi huo.

Katika mwaka wa 2016, mashirika hayo yalikuwa yamewasilisha kesi mahakamani kupinga utekelezaji wa ujenzi wa nyumba hizo za kisasa yakisema hapakuwa na juhudi za kuhusisha umma inavyotakikana kisheria.

Kesi hiyo sasa itatajwa Novemba 11, 2021, ambapo mahakama inatarajiwa kuthibitisha kama maagizo yaliyotolewa yatakuwa yametekelezwa, au maagizo zaidi yatahitajika.

You can share this post!

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Mola Subuhaanahu Wata’ala ndiye...

Watumishi wa Kaunti kugoma ‘wasipothaminiwa’