• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunaomba Mola atufikishe mwezi mtukufu wa Ramadhan

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Tunaomba Mola atufikishe mwezi mtukufu wa Ramadhan

Na HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mola Azzawajalla, swala na salamu zimwendee Mtume wetu Muhammad.

Imepita miezi, wiki na masiku na hivi sasa umekaribia Mwezi wa Qur‘an, mwezi wa Baraka, mwezi wa ibada za usiku, mwezi wa kukubaliwa dua za waumini. Ewe Allah tufikishe Ramadhani!

Maswahaba walilelewa na madrasa ya Mtume wakihisi hisia hizi za kuwa na shauku ya kuufikia mwezi wa fadhila, wakiishi na dua hii “Ewe Allah tufikishe Ramadhaan!”

Wakawa wakimuomba Allah awafikishe Ramadhani kabla ya miezi sita, na miezi sita mingine wakimuomba Allah akubali ibada zao.

Bila shaka hisia hizi na hali hii haikujengeka kwa Maswahaba isipokuwa kwa kujua fadhila za mwezi huu, na nafasi ya mwezi wa Ramadhani.

Ibaada mbali mbali ikiwemo funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani inahitaji ujuzi na maandalizi, ili tuweze kuzikusanya fadhila mbali mbali zilizomo ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Ikiwemo kufutiwa madhambi, kukubaliwa ibaada hiyo ya funga na mengineyo.

Kukithirisha kumuomba Allah atufikishe katika mwezi wa ramadhani ni sehemu ya maandalizi ya Ramadhani. Mwislamu aseme “Ewe Allah tufikishe Ramadhani”:

Masiku haya ambayo tumeukaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani inatubidi tuzidishe sana kumuomba Allah atufikishe ramadhani. Kwani kufikishwa ramadhani ni moja ya neema za Allah.

Watu wengi watamani kufikishwa mwezi mtukufu wa ramadhani lakini si kila mmoja anayetamani ataufikia.Kuna baadhi ya watu tulikuwa nao ramadhani iliyopita lakini mpaka hivi sasa hatupo nao tena. Kwa hiyo sie tulio ruzukiwa uhai mpaka hivi sasa yatubidi tujitahidi kumuomba Allah atufikishe mwezi huu mtukufu wa ramadhani mwezi wa fadhila.

Yatakiwa pia tujitahidi katika kusoma Qur ani angalau juzu moja kwa siku, ili mpaka unaisha mwezi wa shaabani unakua ushakhitimisha Qur ani japo mara moja. Vile vile yatakiwa kutenga muda maalumu kwa ajili ya kusoma na kuzingatia aya mbali mbali katika Qur ani na wala si kutosheka kwa kuisoma haraka haraka tu.

Vilevile, tuswali ibada za usiku tahajudi na witri; japo rakaa mbili tahajudi na rakaa moja witri. Swali rakaa mbili kwa mazingatio. Kumbuka swala ni mawasiliano kati ya mja na Mola wake. Wakati wa kuswali hisi ya kwamba unazungumza na Allah na anakuona na kukusikia.

Soma suurat al Faatiha na sura baada yake kwa mazingatio na utulivu wa hali ya juu, kwa kufanya hivyo utahisi radha ya ibada isiyo sifika na kuhisi furaha ya maisha ya kweli.

Kwani furaha ya maisha ya kweli inapatikana katika kumtii Allah sub-hanahu wata’ala na kukithirisha ibada mbali mbali.

ikiwemo kuswali na swala za usiku.

Na yule atakaye hisi ya kwamba kumtii Allah na kutekeleza ibaada mbali mbali ni kujibana na kuto yafaidi maisha basi dhana yake hiyo itakuwa ni potofu.

You can share this post!

Hofu mapinduzi yakizuka upya Afrika Magharibi

KIKOLEZO: Mubaba wa chipsfunga!

T L