• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Jubilee yazidi kuvuna Mlimani

Jubilee yazidi kuvuna Mlimani

NA WAANDISHI WETU

CHAMA cha Jubilee kinaendelea kujiimarisha kwa kunasa wawaniaji kutoka vyama vinavyounga muungano wa Azimio La Umoja katika eneo la Mlima Kenya.

Chama hicho kinaonekana kuweka mikakati ya kufungia nje wawaniaji wa vyama vingine tanzu katika muungano huo.

Viongozi waliokuwa ndani ya vyama vingine vinavyounga muungano wa Azimio La Umoja, wameanza kuhama vyama vyao na kujiunga na Jubilee. Hii inaonekana kama mbinu ya kuwasimamisha wawaniaji wanaojivunia ufuasi mkubwa dhidi ya wale wa UDA unaoongozwa na Naibu Rais Dkt Willam Ruto.

Katika Kaunti ya Nyeri, aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa benki ya Equity Peter Munyiri anayelenga kiti cha ugavana wa Nyeri, alikihama chama cha PNU kisha kujiunga na kile cha Jubilee ambapo atamenyana na Bw Gachara Kamanga.

Bw Kamanga ambaye pia ni mwenyekiti wa wawaniaji wanaolenga kutumia Jubilee katika kaunti hiyo, alisema bado wanasubiri mwongozo kutoka kwa uongozi wa chama ili kufahamu mbinu itakayotumika wakati wa mchujo.

Alifichua kuwa kuna wawaniaji zaidi ya 100 ambao wanalenga kutumia Jubilee kuwania vyeo mbalimbali katika kaunti hiyo.

Kule Meru, aliyekuwa mbunge wa Tigania Magharibi na mwenyekiti wa PNU David Karithi alihama chama hicho na kujiunga na Jubilee.

“Mwaka huu nitakuwa nawania ubunge kupitia Jubilee. Nilijiunga nacho kwa sababu kiko katika muungano mmoja na PNU na pia kuna mkataba wa ushirikiano kati ya vyama vyote viwili,” akasema Bw Karithi.

Bw Kimathi Amundi ambaye pia ni mwanachama wa PNU alichotumia kuwania ubunge wa Imenti ya Kati mnamo 2017, pia amejiunga na Jubilee kuwania wadhifa huo huo mnamo Agosti 9, 2022.

Kwenye eneobunge jirani la Imenti Kusini mwaniaji wa PNU Jenaro Gatangugi pia amekihama chama hicho na sasa atamuunga mkono Shadrack Mwiti wa Jubilee.

Katika Kaunti ya Laikipia, Gavana Ndiritu Muriithi tayari ambaye alijiunga na PNU, amepokea shinikizo ili ajiunge na Jubilee huku wanasiasa wote waliopo chini ya muungano wa Azimio wakiapa kumuunga mkono kutetea kiti cha ugavana.

Wajumbe waliokutana mjini Nanyuki, walimtaka Bw Muriithi ajiunge na Jubilee huku vyama tanzu vikiahidi kumuunga mkono. Hata hivyo, Mburu

Kamau anayelenga ugavana kupitia Jubilee, amepinga kuidhinishwa kwa Bw Muriithi akisema kuwa ni ukiukaji wa kidemokrasia.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni amesema kuwa Jubilee hakikandamizi vyama vingine chini ya muungano wa Azimio eneo la Mlima Kenya.

Bw Kioni alisema lengo lao ni kuhakikisha kuwa viongozi wengi wanachaguliwa kupitia chama hicho ili kiweze kushughulikia vyema maslahi ya wakazi wa Mlima Kenya kitaifa.

“Kama eneo, lazima tudhihirishe kuwa tupo nyuma ya Rais Kenyatta na ni kupitia kuwachagua viongozi wengi kupitia Jubilee. Tukitwaa viti vingi basi tutakuwa na usemi mkubwa katika siasa za kitaifa,” akasema Bw Kioni.

Kauli yake iliungwa mkono na mbunge wa zamani wa Gatanga Peter Kenneth na Naibu Gavana wa Kirinyaga Peter Ndambiri ambao waliwataka wakazi wa Mlima Kenya wawachague wanasiasa wa Jubilee pekee.

Ripoti Mwangi Muiruri, David Muchui, Mercy Mwende, James Murimi na George Munene

  • Tags

You can share this post!

Kadu-Asili yapata pigo kiongozi wake akihamia PAA

Mbona Uhuru hampigii debe Raila Mlimani?

T L