• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
MBWEMBWE: Kigogo Chiellini ana noti za kukausha bahari nzima

MBWEMBWE: Kigogo Chiellini ana noti za kukausha bahari nzima

Na CHRIS ADUNGO

MWANASOKA Giorgio Chiellini ni nahodha na difenda mzoefu wa Italia, ambaye kwa sasa anasakatia Juventus katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Licha ya umri wake mkubwa wa miaka 36, aliongoza Italia kupepeta Uingereza kupitia penalti kwenye fainali ya Euro 2020, na kuzoa taji la kipute hicho mnamo Julai.

Ufanisi huo ulichochea Juventus kumpa Chiellini kandarasi mpya ya miaka miwili wiki iliyopita.

Sogora huyo amesaidia Juventus kunyanyua mataji 14 ya haiba kubwa katika kipindi cha miaka 16 iliyopita.

Kati ya makombe hayo ni mataji tisa ya Serie A, ambayo Juventus ilizoa kwa mfululizo kati ya 2011-12 na 2019-20.

Chiellini ni miongoni mwa wachezaji wenye miguso ya kutamanika katika safu ya ulinzi.

Ana uwezo wa kutamba katika nafasi yoyote kwenye safu ya nyuma uwanjani.

Baada ya kuvalia jezi ya Livorno na AS Roma kati ya 1990 na 2003, umaarufu ulianza kumwandama alipounga kikosi cha kwanza cha Fiorentina mwaka 2004.

Ushawishi wake katika klabu hiyo ya jijini Florence, Italia – ambayo ilijivunia huduma zake tangu akiwa chipukizi wa miaka 16 – ni miongoni mwa sababu ambazo zilichochea Juventus kumtia rasmi katika sajili yao mnamo 2005.

Utajiri

Ukwasi wa Chiellini kwa sasa unakadiriwa kufikia Sh6.4 bilioni. Kiini kikubwa ni mshahara wa Sh28 milioni aliokuwa akipokezwa na Juventus hadi kufikia mwisho wa muhula wa 2020-21.

Awali, Fiorentina walikuwa wakimdumisha kwa ujira wa Sh20 milioni kila wiki hadi kufikia msimu 2004-05 kabla yake kuondoka.

Mbali na mshahara huo mnono, Chiellini hupata fedha za ziada kutokana na matangazo ya kibiashara na kuwa balozi wa bidhaa na huduma za kampuni mbalimbali.

Amekuwa balozi wa kuvumisha umaarufu wa bidhaa za kampuni ya Electronic Arts (EA Sports), ambayo humkabidhi takriban Sh14 milioni kwa wiki.

Kwa sasa, Chiellini ni balozi wa Adidas, ambayo humlipa Sh35 milioni kila mwezi.

Kwa kifupi, beki huyu hutia kapuni zaidi ya Sh180 milioni kila mwezi.

Mshahara wake wa sasa unamweka katika kundi moja na Wojciech Szczesny na Juan Cuadrado kambini mwa Juventus, ambao humlipa Cristiano Ronaldo ujira wa juu zaidi.

Majengo

Chiellini huishi katika kasri la Sh640 milioni. Alijinunulia jumba hilo jijini Turin, Italia, mwanzoni mwa 2011.

Anamiliki majengo mengine ya kifahari mjini Pisa, Italia. Moja lililo mjini Livorno la thamani ya Sh450 milioni, alilwajengea wazazi wake 2013.

Magari

Ingawa ana magari mengi ya kifahari, Chiellini anapenda zaidi Ferrari F12 TDF, Audi Q9 na Lamborghini Gran-Turismo. Thamani yazo inakisiwa kufikia Sh107 milioni.

Mkewe, Carolina Bonistalli, huendesha michuma aina ya Wrangler S-SUV na Range Rover; iliyonunuliwa kwa Sh80 milioni mnamo 2018.

Mapenzi na Familia

Chiellini alizaliwa Agosti 14, 1984 viungani mwa mji wa Pisa, Italia. Alilelewa pamoja na kakaye pacha, Claudio, katika eneo la Livorno. Nduguze wengine ni Giulio na Silvia.

Alisomea masuala ya uchumi hadi kiwango cha shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Turin, Italia.

Mnamo Julai 2014, alifunga pingu za maisha na mchumba wake wa muda mrefu, Carolina Bonistalli. Wamejaliwa watoto wawili wa kike.

You can share this post!

IEBC yasema iko tayari kutii mabadiliko yoyote ya kikatiba...

DIMBA: Kiganjo Kings wanatambua bidii ya mchwa itawajenga