• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:07 PM
Mchuuzi anayevuna vinono kupitia kilimo cha mananasi

Mchuuzi anayevuna vinono kupitia kilimo cha mananasi

Na SAMMY WAWERU

JITIHADA zake kuwa mwanahabari zilipogonga mwamba kwa sababu ya ukosefu wa karo, Zachariah Makori aliamua kufanya vibarua vya hapa na pale kusukuma gurudumu la maisha.

Licha ya kuzamia kozi ya Uanahabari kwa muda wa miaka miwili katika chuo kimoja Mjini Eldoret, Makori alijituma kuchuuza matunda. Anasema hakuwa na budi kuchukua uamuzi huo anaotaja kuwa ‘chungu’, ikizingatiwa kuwa ndugu zake walitegemea mama yake kukata kiu cha masomo.

Baadhi walikuwa katika shule ya msingi na wengine upili, hivyo basi hakuwa na jingine ila kuwapa fursa wafike alipofika kimasomo. Huo ulikuwa mwaka wa 2010. “Mama alikuwa ameugua, nikashirikiana naye kuwasomesha,” asema barobaro huyu ambaye ni mzaliwa wa Kaunti ya Kilifi.

Makori aliingilia uuzaji wa matunda kama vile matikiti maji, maparachichi – avokado na mananasi. Vile vile alichuuza miwa. Ni biashara iliyomfumbua macho, na 2013 akajaribu mkono wake kwenye kilimo. “Nilianza na matikiti maji, niliyolima kwenye nusu ekari,” aelezea, akifichua kwamba hatua hiyo ilimgharimu mtaji wa Sh30, 000.

Fedha hizo alizoweka akiba kupitia uuzaji wa matunda, ziligharamia kukodi shamba, kuliandaa na pembejeo – mbegu, mbolea/fatalaiza, na dawa kupambana na kero ya magonjwa na wadudu.

Zachariah Makori, mkulima wa mananasi Kilifi, anasema mfumo wa Master pits unasaidia kudhibiti matumizi ya maji na kuyahifadhi kupitia nyasi za boji na kuboresha rutuba…Picha/ SAMMY WAWERU

Alikuwa limbukizi katika kilimo, na Makori anasema hakupata faida kama alivyotarajia. Hakuwa na ujuzi na maarifa katika shughuli za kilimo, anataja, akiongeza kuwa alijituma kufanya utafiti unaojumuisha kuzuru wakulima walioimarika na kwenye mitandao.

Kulingana na Makori, kisomo hicho kilimshinikiza kuchukua breki ya miezi sita. “Nilirejea nikiwa na maarifa chungu nzima na kurekebisha makosa niliyofanya,” afafanua. Baadaye, alijumuisha okra, pilipili mboga na mboga za kienyeji kama mnavu maarufu kama managu au sucha, mchicha (terere) na sageti.

Mwaka wa 2018, anafichua alipanda matikiti maji kwenye ekari 24 japo mazao na vifaa vya kunyunyizia mimea na maji mashamba vyenye thamani zaidi ya Sh3 milioni vikasombwa na mafuriko. Hata ingawa hajapata nafuu ya hasara aliyokadiria kufikia sasa, 2019 Makori aligeukia kilimo cha mananasi.

Anataja kilimo cha zao hilo kama chenye faida na rahisi kupanda na kutunza. Katika kijiji cha Mlunguni, Marafa, Kaunti ya Kilifi kwenye ekari 16 zilizogawanywa kwa makundi mawili ya ekari 5 kila moja, na kundi jingine la ekari 6, tunampata Makori akikagua mananasi ambayo ni tayari kuingia sokoni.

“Mananasi ni zao la msimu mmoja kwa mwaka. Hutegemea maji ya mvua,” adokeza, akisema matunda yake huwa na uzani wa kilo 3 hadi 7.

Teknolojia ya master pit

Katika mazingira tajika kwa uzalishaji wa mananasi, mahindi na mihogo na ambayo ni nusu jangwa, mradi wa mkulima huyu hodari ni wa kipekee. Ukiwa karibu kuwiana na Zai pits, amekumbatia mfumo wa Master pits, teknolojia ya kisasa anayosifia kudhibiti matumizi ya maji hasa katika maeneo kame.

Kila shimo likiwa na kipimo cha urefu wa sentimita 40 (length), upana sentimita 30 (width) na sentimita 45 kina (depth), huweka udongo uliotolewa juu na kuuchanganya na mbolea. “Baada ya maandalizi ya shamba, hutumia mfumo wa Master pits kupanda mbegu – matawi (suckers) ya mananasi,” mkulima huyu aelezea.

Aidha, anasema mfumo huo ni bora katika kudhibiti uvukizi wa maji (evaporation), kupitia nyasi za boji (mulching). “Maji kwenye shimo (pits) hudumu muda mrefu.” Teknolojia hiyo pia huchangia pakubwa katika kuboresha rutuba udongoni, kwa sababu ya matumizi ya nyasi zilizokauka, majani na matawi, ambazo hugeuka kuwa mbolea.

Makori, 29, ni mfugaji wa kuku na hutumia kinyesi cha mifugo wake kufanya upanzi. Kwa sasa, ana karibu kuku 150. “Kwenye mashimo, huandaa vijishimo na kupanda mbegu za mananasi – matawi yenye urefu wa sentimita 30,” asema. Tawi hupandwa hadi urefu wa sentimita 10, nafasi inayosalia inakuwa ya nyasi za boji na maji.

John Mutisya, mtaalamu kutoka Biovision Trust Africa, shirika lisilo la kiserikali Machakos, anasema matumizi ya pits ni faafu kuendeleza shughuli za zaraa hasa maeneo ya jangwa na nusu jangwa. “Sehemu zisizopokea mvua ya kutosha na kiangazi na ukame unaodumu muda mrefu, pits husaidia kuhifadhi maji,” Mutisya afafanua.

Kando na kuboresha rutuba, mtaalamu huyo anasema teknolojia ya pits huboresha hewa udongoni. Mbolea asilia – ya mifugo iliyochanganywa na majani na matawi, hufanya mimea kuwa imara na dhabiti, hivyo basi kuwa na kinga dhidi ya wadudu na magonjwa.

Mbali na kutumia master pits kukuza mananasi, mfumo huo pia unaweza kutumika kulima mboga, nyanya, mahindi, maharagwe, mbaazi, kati ya mazao mengineyo. Kulingana na Makori, chini ya mfumo wa Master pits mananasi hupandwa umbali wa sentimita 45 – 50 kutoka mmea hadi mwingine.

Nafasi ya laini ya mimea hadi nyingine, inapaswa kuwa sentimita 60. “Inapokauka bada ya hupanzi, hurejesha mbegu zingine za matawi,” Makori asema. Mananasi hukomaa miezi 18, sawa na mwaka mmoja na miezi sita baada ya upanzi, Makori akisema huwa makini kuzuia kwekwe kupitia palizi.

Hunawirisha mazao kwa kutumia fatalaiza yenye virutubisho vya Nitrogen, Calcium na Potassium, minanasi ikiwa na umri wa miezi miwili na kati ya miezi 14 hadi 15. Aidha, anasema mananasi hushuhudia changamoto haba za magonjwa na wadudu.

Hata hivyo, anataja fuko, panya na nguchiro kama wanyama waharibifu kwa mazao wasipodhibitiwa. Chini ya vigezo faafu vya kilimo, Makori anakiri ekari moja inazalisha wastani wa matunda 7, 000 ya mananasi kila mwaka. Wateja wake ni wa kijumla, kutoka Malindi, Kilifi, Mombasa na wengine Nairobi, akisisitiza bei yake ni ya langoni.

Kulingana na uzani – uzito, tunda huuza kati ya Sh40 – 100. Minanasi inazaa hadi inapofikisha umri wa miaka mitano mazao yanaanza kupungua, ishara kuwa inapaswa kung’olewa kupanda mingine. Akiridhia kilimo cha matunda hayo matamu, Makori ana wafanyakazi wanne.

Kilifi ikiwa miongoni mwa kaunti kame eneo la Pwani, Zachariah Makori amekumbatia mfumo wa Master pits kukuza mananasi…Picha/ SAMMY WAWERU

You can share this post!

Senegal wapepeta Misri kwa penalti 4-2 na kutwaa taji la...

Kenya Kwanza sasa yacheza siasa na watoto

T L