• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Senegal wapepeta Misri kwa penalti 4-2 na kutwaa taji la AFCON

Senegal wapepeta Misri kwa penalti 4-2 na kutwaa taji la AFCON

Na MASHIRIKA

SUBIRA ya Senegal hatimaye iliwavunia heri ya Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 60 walipokomoa Misri kwa penalti 4-2 mnamo Jumapili usiku ugani Olembe, Cameroon.

Lions of Teranga ya Senegal ilitia kapuni Sh565 milioni kwa kupepeta Misri baada ya kuambulia sare tasa katika muda wa ziada. Mabingwa mara saba wa AFCON, Misri, waliridhika na Sh310.8 milioni kwa kukamilisha kampeni za kipute hicho katika nafasi ya pili.

Makala yajayo ya fainali hizo yatafanyika nchini Ivory Coast mnamo Juni–Julai 2023. Sadio Mane aliyefunga mabao matatu na kuchangia mengine mawili kabla ya fainali, alijaza kimiani penalti ya ushindi. Fowadi huyo wa Liverpool aliyetawazwa Mchezaji Bora wa AFCON 2021, sasa ameingia katika orodha ya wanasoka nguli wa Senegal.

Amehusika moja kwa moja katika mabao tisa (kufunga sita na kuchangia matatu) kati ya 14 yaliyopita ambayo Senegal wamefunga kwenye AFCON. Mohamed Abou Gabal wa Misri aliyepangua penalti mbili aliibuka Mlinda-lango Bora wa fainali huku Edouard Mendy wa Senegal alitawazwa Kipa Bora wa kipute kizima baada ya kutofungwa bao katika mechi tano nchini Cameroon.

Fowadi Vincent Aboubakar wa Cameroon alitwaa Kiatu cha Dhahabu baada ya kupachika wavuni mabao manane, matatu zaidi kuliko mwenzake Karl Toko Ekambi anayesakatia Olympique Lyon ya Ufaransa.

Senegal wameshikilia nafasi ya kwanza barani Afrika kwa miaka mitatu iliyopita. Walizidiwa ujanja na Cameroon kwa penalti 3-2 baada ya sare tasa kwenye fainali ya AFCON 2002 nchini Mali na wakapokezwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Algeria mnamo 2019.

“Ushindi wetu ni zao la bidii. Anayevumilia hula mbivu. Nakosa maneno mazuri matamu ya kuelezea ninavyohisi kwa sababu tumesubiri taji hili kwa miaka 60,” akasema kocha Aliou Cisse wa Senegal aliyepoteza penalti kwenye fainali ya 2002 dhidi ya Cameroon akichezea Lions of Teranga.

Senegal walianza kampeni zao za Kundi B kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Guinea na Malawi. Walipepeta Cape Verde 2-0 katika hatua ya 16-bora kisha kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Equatorial Guinea na Burkina Faso kwenye robo-fainali na nusu-fainali mtawalia.

Mechi zote nne zilizotandazwa na Misri kwenye hatua ya muondoano ziliingia muda wa ziada na walihitaji penalti 5-4 na 3-1 baada ya sare tasa ili kubandua Ivory Coast na Cameroon kwenye hatua ya 16-bora na nusu-fainali mtawalia. Walifungua kampeni za Kundi D kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Nigeria kabla ya kutandika Guinea-Bissau na Sudan 1-0 na kukomoa Morocco 2-1 kwenye robo-fainali.

Chini ya nahodha Mohamed Salah anayechezea Liverpool, Misri watakuwa na fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya Senegal watakapokutana mwezi ujao kwenye mchujo wa mwisho wa michuano ya mikondo miwili ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

“Mane ni kiongozi. Alibeba Senegal mabegani na kuwashindia taji. Senegal ndicho kikosi thabiti zaidi barani kwa sasa na kilistahili kutwaa ubingwa wa AFCON,” akasema mwanasoka wa zamani wa Tottenham Hotspur, Jermaine Jenas.

You can share this post!

Lampard aongoza Everton kupepeta Brentford bila huruma...

Mchuuzi anayevuna vinono kupitia kilimo cha mananasi

T L