• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:57 PM
Mijeledi ya John Michuki ilivyolainisha sekta ya matatu

Mijeledi ya John Michuki ilivyolainisha sekta ya matatu

KWA HISANI YA KYB

UAMINIFU wake kwa Rais Mwai Kibaki haukuyumba. John Michuki alikuwa tayari kulinda serikali baada ya visa vilivyozua utata alipokuwa akihudumu katika Baraza la Mawaziri ikiwemo shambulizi lililoshutumiwa mno katika kampuni ya habari ya Standard Group.

Akijibu wanahabari kuhusu kisa hicho, Michuki alisema: “Ukichokoza nyoka, lazima uwe tayari kuumwa.”

Kauli yake hiyo ilikashifiwa vikali.Alikuwa mwenye haraka ya kusaidia Kibaki aliyekuwa ameingia uongozini kufufua uchumi na kurejesha nidhamu iliyokuwa imetawala sekta ya uchukuzi.

Wakati huo, magari mengi ya uchukuzi wa umma (yanayojulikana kama matatu) yalikuwa yakihudumu nchini ya chama cha wamiliki wa matatu (Matatu Owners Association), ambacho kilikuwa kimechukua nafasi ya Matatu Vehicle Owners Association kilichoundwa 1982 kutengea matatu maeneo ya kuhudumu lakini kikaharamishwa 1987 baada ya kuitisha mgomo wa kitaifa.

Michuki aligundua kuwa wamiliki wa matatu walikuwa wakipoteza mabilioni ya pesa kwa mitandao ya matapeli na wanachama wa kundi la Mungiki lililokuwa limeteka vituo, barabara na mitaa ambayo matatu zilihudumu Nairobi.

Vile vile, alikabiliana na makundi mengine yaliyofanana na Mungiki kama Taliban, Jeshi la Mzee na Kamjeshi – ambayo yalikuwa yakiitisha wakazi pesa kwa vitisho na kutoka kwa wamiliki wa matatu kuwalinda.

Magari ya waliokataa kulipa yalichomwa na wamiliki wake kuuawa. Hii ndiyo hali ambayo Michuki alirithi katika wizara ya uchukuzi.

Sekta ya Matatu

Aliambia Bunge kwamba sekta ya matatu sio tofauti kutoka sekta nyingine, ambazo umiliki, ukiwemo wa ardhi au mali nyingine, umehakikishwa.

Michuki aliyezaliwa mwaka wa 1939, Iyego, Wilaya ya Murang’a alinawiri akihudumu kama afisa wa utawala tangu alipojiunga na utumishi wa umma miaka ya mwisho ya utawala wa kikoloni, kwanza akiwa karani kabla ya kuteuliwa Mkuu wa Tarafa kaunti ya Busia.

Akiwa na umri wa miaka 27, aliteuliwa kuwa mkuu wa kwanza mwafrika wa wilaya ya Nyeri mwaka wa 1961. Hii ilikuwa siku chache baada ya kufunzu kutoka chuo cha Worcester College, sehemu ya chuo kikuu chaOxford, Uingereza alikosomea usimamizi wa umma na uchumi.

Baada ya Kenya kupata uhuru 1963, Michuki alikuwa mmoja wa maafisa wa utawala na usimamizi walioteuliwa na Rais Jomo Kenyatta.

Walikuwa katika umri wa miaka 20s na 30s na walijumuisha mtaalamu wa uchumi Mwai Kibaki, Kenneth Matiba, Duncan Ndegwa, Tom Mboya, Peter Shiyukah, Geoffrey Kariithi, John Koitie na Julius Kiano.

Michuki aliteuliwa katibu wa wizara ya fedha kwa mara ya kwanza Julai 1, 1965 na alihudumu serikalini kwa miaka mingi kabla ya kujiunga na siasa.

Wakati wa kupigania vyama vingi vya kisiasa miaka ya 1990s, Michuki ambaye alihudumu kama mbunge wa Kangema kwa muhula mmoja (1983 hadi 1988) alimuunga Kenneth Matiba, mwanzilishi wa FORD-Asili na mgombea urais wa chama hicho.

Kibaki alikuwa ameunda chama kingine cha upinzani cha Democratic Party. Hata hivyo, hii haikuharibu uhusiano wake na Kibaki.

Haikuwa hadi 2002 alipojiunga na National Rainbow Coalition (NARC) na akawa sehemu ya kundi lililoondoa Kanu mamlakani.Baada ya miaka miwili aliyofaulu mno katika Wizara ya Uchukuzi,Michuki aliteuliwa Waziri wa Utawala wa Mikoa na Usalama wa ndani, akibadilishana majukumu na Chris Murungaru.

Michuki alitangaza vita dhidi ya Mungiki na makundi mengine na akayaonya yakomeshe shughuli zao au yakabiliwe na nguvu zote za serikali.

“Tutawanyorosha… Nyinyi mtakuwa mkisikia mazishi ya fulani ni ya kesho,” alinukuliwa akisema na kukasirisha wanaharakati wa haki za binadamu.

Baada ya uchaguzi mkuu uliokubwa na ghasia wa 2008, Michuki aliteuliwa waziri wa Mazingira na Mali Asili katika serikali ya muungano wa kitaifa na miongoni mwa mambo aliyofanya katika mazingira ni kuagiza maskwota kuondoka msitu wa Mau hatua iliyozua mzozo kati yake na wabunge kutoka Rift Valley.

Pia alianza juhudi za kuokoa mto Nairobi na alituzwa na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa kwa juhudi zake.

Hata hivyo, kujitolea kwake kukabiliana na kurekebisha masuala ya mazingira zilitatizwa afya yake ilipoanza kudhoofika. Alifariki Februari 21 2012 akiwa na umri wa miaka 79.

  • Tags

You can share this post!

Baraka za Joho kwa Nassir zinaashiria nini?

Rigathi Gachagua na Moses Kuria wakabana koo kuhusu...

T L