• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
MITAMBO: Kifaa cha kubaini ubora wa udongo kuwafaa wakulima

MITAMBO: Kifaa cha kubaini ubora wa udongo kuwafaa wakulima

NA RICHARD MAOSI

GHARAMA kubwa zinazohitajika kununua huduma za kitaaluma na vilevile uhaba wa pembejeo muhimu za kuendesha kilimo endelevu chenye tija, zimefanya wakulima wengi waendelee kushikilia mbinu za kiasili kuendesha kilimo.

Ndiposa inashauriwa mkulima kuelewa afya ya udongo wake kabla ya kuwekeza kwa kuangazia mambo muhimu kama vile kiwango cha unyevu, asidi PH na virutubishi asilia.

Ni kwa sababu hiyo Derrick Ngige ambaye ni mhandisi na mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta amevumbua kifaa cha Farm Assistant ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto za udongo kupoteza rutuba.

“Inawezekana kuwa shughuli za kibinadamu kama vile kutumia mbolea nyingi kupita kiasi, ndiyo sababu inayofanya afya ya udongo kudorora,”asema.

Kwa upande mwingine wakulima wanaoendesha kilimo cha mjini wamekuwa wakisomba udongo kutoka sehemu moja hadi nyingine bila kufanya tathmini , endapo mchanga umepoteza virutubishi au la.

Kulingana na Ngige ambaye ni mzaliwa wa eneo la Naivasha kaunti ndogo ya Nakuru, alifichulia Akilimali kuwa alizaliwa katika familia ya wakulima ingawa wazazi wake hawakuwa wamemakinika kuzingatia swala la afya ya udongo.

Derrick Ngige (kushoto) akionyesha jinsi kifaa cha Farm Assistant kinavyowasaidia wakulima kutoa tathmini ya afya ya udongo. PICHA | RICHARD MAOSI

Aidha aligundua kuwa wakulima wengi wamekuwa wakichukua sampuli ya udongo wao kwa Shirika la Kenya Agricultural Livestock and Research Organisation KALRO, lakini huchukua hadi miezi mitatu kupata matokeo.

Isitoshe ni hali ambayo imekuwa ikiwachosha na kuwakatisha tamaa ikizingatiwa kuwa mchakato mzima ni ghali.

Kupitia kifaa chake cha Farm Assistant anaweza kupima hali ya udongo na mkulima akayapokea matokeo yake baada ya dakika 10.

Kuanzia hapo anaweza kutoa ushauri ama kupendekezea mkulima mifumo ya ukulima ambayo anastahili kutumia.

Ngige ambaye hutoa huduma zake kuanzia Ijumaa hadi Jumapili kila wiki anasema anapopata mwaliko kutoka kwa mkulima, huzuru shamba zima na kuchota sampuli za udongo kutoka sehemu mbalimbali shambani.

Kifaa cha Farm Assistant kinapotundikwa juu ya mchanga, hukusanya taarifa kupitia mifumo ya elektronika na kupitiza ujumbe hadi kwenye databesi yake kutengeneza ufafanuzi.

Anasema maelezo yenyewe huingia kwenye simu ya mkulima kupitia huduma za arafa almaarufu kama SMS, ambapo anaweza kupokea habari kuhusu kiwango cha Phosphorus, potassium na calcium kwenye udongo wake.

Pia anaweza kupata maelezo kuhusu kile anachotakiwa kufanya ili kutibu nakisi ya vitutubishi vinavyopatikana kwenye shamba.

‘Wakati mwingine mkulima anaweza kushauriwa kutumia samadi au mchanganyiko wa mbolea ya mbuzi na makapi ya majani, kutengeneza madini ya calcium udongoni,’alisema.

Mara nyingi Ngige amekuwa akifanya kazi kwa ukaribu na wakulima ambao wameunda vyama vya ushirika ambapo mmoja wao hufanyiwa mafunzo namna ya kuwahudumia wakulima wenzake kupitia kifaa cha Farm Assistant.

Katika kila ekari moja ya shamba Ngige huwatoza wakulima Sh1400, ambapo kufikia sasa anawahudumia wakulima takriban 200.

Isitoshe Ngige amegundua kuwa anapotumia kifaa hiki kuwasaidia wakulima faida zake ni nyingi kwani kiwango cha uzalishaji huongezeka kwa asilimia 36, huku gharama ya kununua pembejeo za ukulima kama vile mbolea ikishuka kwa asilimia 40.

Hata hivyo anasema kuwa wakulima wengi nchini bado hawajakumbatia mifumo ya kuendesha kilimo kidijitali kwa dhana kuwa ni ghali.

Ngige anaomba serikali kuu kwa Ushirikiano na wizara ya kilimo kutumia mbinu hii ya kupima afya ya udongo ili kutambua sehemu ambazo zinaweza kustawisha mimea, ikiwa ni njia mojawapo ya kupigana na umaskini na kutengeneza nafasi nyingi za ajira kwa vijana.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa wavuna baraza la mawaziri

Raia wa Uganda anayeshukiwa kumuua mke-mwenza ndani

T L