• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Wanasiasa wavuna baraza la mawaziri

Wanasiasa wavuna baraza la mawaziri

NA MARY WANGARI

RAIS William Ruto jana Jumanne aliteua idadi kubwa ya wanasiasa kuendesha serikali katika wadhifa wa waziri.

Kati ya mawaziri 22 ambao aliteua Jumanne, na ambao sasa watapigwa msasa na bunge kabla ya kuapishwa, Rais Ruto aliwateua wanasiasa 17.

Ni waziri mteule wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rebecca Miano, Njuguna Ndung’u (Fedha), Davis Chirchir (Kawi), Zacharia Mwangi (Ardhi) na Simon Chelugui (Vyama vya ushirika) ambao sio wanasiasa.

Kwenye uteuzi huo, Rais Ruto aliwarudishia mkono waliotembea naye katika safari ya kuingia Ikulu, ambayo aliitaja Jumanne kama iliyokuwa na vikwazo vingi.

Pia rais alitengea viti zaidi maeneo ya Mlima Kenya na Rift Valley, ambako alizoa idadi kubwa zaidi ya kura zilizomwezesha kushinda kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Eneo la Mlima Kenya lilitengewa nyadhifa tisa katika baraza la mawaziri huku Rift Valley ikipata vitano.Walioteuliwa kutoka Mlima Kenya ni Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani), Njuguna Ndung’u (Fedha), Alice Wahome (Maji), Moses Kuria (Biashara), Rebecca Miano (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Zachariah Mwangi Njeru (Ardhi) na Mithika Linturi (Kilimo).

Wengine ni Justin Muturi (Mwanasheria Mkuu) na Mercy Wanjau (Katibu wa Baraza la Mawaziri).

Katika ngome yake ya Rift Valley, Rais Ruto aliteua Kipchumba Murkomen (Barabara na Uchukuzi), Soipan Tuya (Mazingira na Misitu), Bw Chirchir, Bw Chelugui na Florence Bore (Leba).

Magharibi nayo ilipata teuzi tatu za Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri), Ababu Namwamba (Vijana) na Susan Wafula (Afya).Maeneo mengine ambayo yalipata uteuzi ni Pwani (2) likiwakilishwa na Salim Mvurya (Madini) na Aisha Jumwa (Huduma za Umma na Jinsia).

Eneo la Ukambani nalo lilipata watatu ambao ni Alfred Mutua (Mashauri ya Kigeni), Peninah Malonza (Utalii) na Monicah Juma (Mshauri wa Masuala ya Usalama).

Wengine walioteuliwa ni Eliud Owalo (ICT, Nyanza), Ezekiel Machogu (Elimu, Kisii) na Aden Duale (Ulinzi, Kaskazini Mashariki).

Mawaziri wawili waliohudumu katika utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta walijipata katika baraza la mawaziri la Dkt Ruto, hao wakiwa ni Bw Chelugui na Dkt Juma.

Rais aliasema majukumu ya naibu wake Rigathi Gachagua yatakuwa mengi ikiwa ni pamoja na kushirikisha shughuli za serikali, taasisi na ukaguzi wa miradi.

Bw Mudavadi naye alitengewa majukumu makubwa na wadhifa wake ndio wa tatu kimamlaka baada ya rais na naibu wake.

Rais alisema teuzi zingine kama vile za makatibu wa wizara zitafuatia hivi karibuni.

Kabla ya kutangaza uteuzi wa baraza lake Jumanne, Rais Ruto alifanya kikao na mawaziri ambao walihudumu chini ya utawala wa mtangulizi wake Uhuru Kenyatta.

Kati ya mawaziri hao ni wale ambao walikuwa katika mstari wa mbele kumzuia kuingia Ikulu wakiongozwa na Dkt Fred Matiang’i (Usalama), Joe Mucheru (Teknolojia ya Mawasiliano), Keriako Tobiko (Mazingira), Peter Munya (Kilimo), Ukur Yatani (Fedha) na Eugene Wamalwa (Ulinzi).

Wakati wa kampeni, Rais Ruto aliwashutumu Dkt Matiang’i na Bw Mucheru akidai kuwa walipanga kuiba kura zake.Dkt Matiang’i wakati wa kampeni hakuwa akificha upinzani wake kwa Rais Ruto kuongoza taifa.

Bw Mucheru naye mwaka 2021 alimshambulia vikali Rais Ruto akidai alikuwa akipotosha vijana kwa kampeni zake kuhusu uchumi, pamoja na kutumia michango yake kanisani kutafuta uungwaji mkono.

Bw Tobiko naye mnamo 2020 alimwita Rais Ruto kuwa “karani wa kawaida wa rais”, Bw Munya akadai alikuwa amepora mali ya umma naye Bw Wamalwa akamtaja kama “mtu mwongo”.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ateua Koome kurithi Mutyambai, Kinoti ajiuzulu DCI

MITAMBO: Kifaa cha kubaini ubora wa udongo kuwafaa wakulima

T L